Sunday, August 3, 2014

Safari ya Bitchuka na muziki wa Tanzania-2

Safari ya Bitchuka na muziki wa Tanzania-2
**Aliajiriwa Msondo akiwa ziarani

NA JIMMY CHIKA
WASTAHIKI wasomaji wa makala haya, wiki iliyopita tulianza kuona safari ya mwimbaji nguli wa muziki wa dansi Hassan Rehani Bitchuka.
Kwa uchache tuligusia safari yake iliyomtoa Arusha na kuja jijini Dar na kujiunga na bendi ya NUTA.
Tumepata maoni mengi kutoka kwa wasomaji, hasa wale waliotujulisha safari nyingine ya mwimbaji huyo, hususan alipowahi kufanya muziki kabla ya kuwepo Arusha na NUTA Jazz.
Kwetu tunaamini kwamba mwimbaji huyo, kwa hakika ameitumia nafasi yake kwa weledi na muda mrefu, na kwamba si rahisi kupagusa kila alipopita.
Kwa uchache huu tutaangalia yale tuliyobahatika kuyagusa, na pia tutaendelea kupokea ushauri, maoni na hata pongezi kama zipo.


Naam, usiku wa takriban saa nne hivi ikiwa bendi ya NUTA imeshatumbuiza nyimbo kama tatu hivi, hatimaye mwimbaji wake (Marehemu) Muhidin Gurumo anatangaza ujio wa mwanamuziki chipukizi, Hassan Bitchuka, hiyo ilikuwa mwaka 1973.
Hatimaye Bitchika anakabidhiwa kopaza sauti na kuimba wimbo ninaoukumbuka kwa mameno.
"Ukiwa kama hunitaki dada"
Ukumbi ulitamalaki, watu wakapagawa, na mifuko yake ikafurika tuzo, kwa ujumla aliimba kwa ufasaha mkiubwa na sauti ya kughani.
Viongozi wa NUTA Jazz kwa umoja wao wakiwa na wanamuziki kama Kiiza Hussein, Ahmad Omar, Mabruk Khalfan, Joseph Lusungu, Mnenge Ramadhani, Abel Baltaza na Muhidin Gurumo wakafurahi kuliko ilivyokuwa kwa mashabiki.
Hapo ndipo ilipopigwa simu jijini Dar es Salaam katika ofisi za Jumuia ya Wafanyazi enzi hizo NUTA kutaja kijana huyo afungulie ajira mara moja.
Bitchuka aliporea jijini alikuwa na kazi moja tu ya kutia saini faili lake na ndipo maisha mapya na matamu ndani ya NUTA jazz yalipoanza.

AIBUKA NA MSONDO WA NUTA
Siku chache baada ya kuzoeana na wanamuziki, hasa Ahmed Omar anayemsifu kwamba alikuwa akifahamu vizuri lugha ya Kishwahili, Bitchuka akaibuka na wimbo uitwao Msondo wa NUTA.
Kati ya nyimbo zilizolete mabadiliko makubwa katika bendi hiyo ni pamoja na huo, ambao ni utunzi wake wa kwanza Hassan Bitchuka kabla ya Mpenzi Zalina na Aziza.

Katika hali nyingine ujio wake ulimuunganisha vizuri na mkongwe Gurumo ambaye aliridhia kuacha kuimba sauti ya kwanza na kumuachia rasmi kijana huyo enzi hizo huku yeye akihamia rasmi sauti za chini, yani ya pili na ya tatu.

Ukipata nafasi ya kusikiliza wimbo uitwao Mume wangu, utaona jinsi magwiji hawa kwa pamoja walivyoziichea sauti zao kwa ujuzi wa hali ya juu.

Habu ukumuke kidogo wimbo huu.
Mume wangu nirudishe kwetu kwa baba na mama.
Sababu watoto wako sielewani nao, kila nisemaloo wasema mimi mama wa kambo.
Kumbuka nilikueleza usimuache mama wato wako, watoto wengi mmekwisha zaa naye mrudie mama wato wako...

Hayo ni baadhi ya maneno yaliyomo kwenye wimbo huo ambao ndani yake una sauti mbili yani ya Bitchuka na Gurumo.

Umaarufu wa Bitchuka sasa ulianza kusambaa na hadi kutoka nje ya jukwaa.
Kwani marafiki waliongezeka na hasa wafanyakazi wa ngazi mbalimbali katika jumuia ya wafanyakazi nao walijisogeza karibu yake.
Mialiko mbalimbali iliyoambatana na posho za hapa na pale havikukauka kwa mwanamuziki huyo.
Vilevile ndani ya bendi walijikuta wakiunda 'upacha' wa sauti kati yake na Gurumo, pia wapiga magitaa wakahusudu sana kuikia sauti yake kila wanapotengeneza wimbo mpya.
Kuanzia hapo Bitchuka alikuwa ni yeye na Msondo.
Lakini kila panano mazuri na mabaya yapo, ukaribu wa yeye na Gurumo hatimaye ulifikia tamani, wakaachana, hawakuwa pamoja tena, ule uipacha ukapotelea gizani, unajua ni kwa nini..Fuatilia makala hii Jumapili ijayo.
&&&&

No comments:

Post a Comment

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NI TISHIO KWA AFYA YA MAMA NA MTOTO NCHINI

                         Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii  Serikali imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kwa ...