Na
Veronica Simba – Aliyekuwa Dodoma
Tanzania inatarajiwa
kuwa kitovu cha uunganishaji wa umeme uliopo Kaskazini na Kusini mwa Afrika
mapema mwakani baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme wa
Kilovoti 400 yenye urefu wa Kilomita 670 kutoka Iringa hadi Shinyanga.
Mradi huo unaojulikana
kama Backbone na uliopangwa
kukamilika mwezi Aprili mwakani, unatarajiwa kuzinduliwa na Rais Jakaya Kikwete
Novemba mwaka huu na utagharimu takribani Dola za Marekani Milioni 455 sawa na
shilingi bilioni 760 za kitanzania.
Hayo yalibainika
mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo aliyoifanya kwa lengo la kukagua maendeleo ya
utekelezaji wa mradi huo katika vijiji vya Mlowa, Nala na Mbwanga mkoani
Dodoma.
Akihitimisha ziara
hiyo, Waziri Muhongo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mradi wa Backbone
utakapokamilika utaziunganisha gridi za nchi za Kenya kwa upande wa Kaskazini
na Zambia upande wa Kusini Magharibi. Kwa kuunganisha gridi hizo, kutaifanya
Tanzania kuwa “kitovu cha uunganishaji wa umeme uliopo Kaskazini na Kusini mwa Afrika (East and Southern Africa Power Pool).”
Alisema, mradi huo
pia utahusika kusambaza umeme katika vijiji vilivyo kando kando ya njia kuu ya
umeme ambayo itaunganisha upande wa Kusini mwa nchi ambako kunatarajiwa kuwa na
vyanzo vingi vya umeme kama Kiwira, Mpanga, Ruhudji, Mchuchuma na Rumakali.
Aidha, alisema kuwa mradi
wa Backbone utaunganisha upande wa
Kaskazini wenye matumizi makubwa ya umeme yanayotokana na kuwepo kwa migodi ya
madini na viwanda mbalimbali.
Vilevile, Profesa
Muhongo alisema Backbone itaongeza
upatikanaji wa umeme wa uhakika upande wa Kaskazini na Magharibi mwa Tanzania
na kuwezesha watu wengi kufungiwa umeme hasa vijijini na hivyo kuharakisha
mpango wa taifa wa kuinua uchumi na kupunguza umaskini.
Akizungumzia
maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, Profesa Muhongo alisema ameridhishwa na
utekelezaji wake na kuongeza kwamba ana imani mradi utakamilika kwa wakati na kwa
ubora unaotakiwa.
“Serikali tunaposema
tumedhamiria kuzalisha umeme mwingi na wa uhakika hatutanii. Mradi umeanza
vizuri na nina imani utakamilika kama ulivyopangwa,” alisisitiza.
Naye Kamishna
Msaidizi wa Nishati, Sehemu ya Umeme, Mhandisi Innocent Luoga alisema
utekelezaji wa mradi wa Backbone
umegawanyika katika sehemu nne. Sehemu hizo ni pamoja na ujenzi wa njia ya
umeme wa Kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 225
ambayo inajengwa na Mkandarasi KEC International Limited na ujenzi wa njia ya
umeme wa Kilovolti 400 kutoka Dodoma hadi Singida yenye urefu wa kilomita 217
inayojengwa na Mkandarasi Jyoti Structures Limited.
Alizitaja sehemu
nyingine kuwa ni njia ya umeme wa Kilovolti 400 kutoka Singida hadi Shinyanga
yenye urefu wa kilomita 228 inayojengwa na KEC International Limited pamoja na
upanuzi wa vituo vya kupoozea umeme vya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga,
vinavyojengwa na GSE&C & HYOSUNG.
Mhandisi Luoga
alisema ujenzi wa mradi huo umefadhiliwa kwa mkopo kutoka Washirika wa
Maendeleo wa Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika
la ushirikiano la Japani (JICA), Benki ya Jumuiya ya Ulaya (EIB) na Benki ya
Korea kupitia EDCF.
Kuhusu ulipaji fidia
kwa wananchi waliopitiwa na mradi, Mhandisi Luoga alisema mchakato wa kutambua
sehemu ambapo njia kuu ya umeme itapita na kuangalia watu watakaoathiriwa na
mradi ulishafanyika.
Alisema serikali
ililipa jumla ya shilingi bilioni 22.5 kama fidia kwa wananchi husika, zoezi
ambalo lilifanyika kati ya mwaka 2009 na 2010. Aidha, alisema kuwa serikali
inatekeleza ujenzi wa majengo mapya ya kisasa kwa taasisi na mashirika ya dini
yaliyopitiwa na mradi kama ofisi za serikali za vijiji, shule, misikiti,
makanisa, vituo vya polisi na majosho ya ng’ombe.
Aidha, Mhandisi Luoga
alisema mradi pia utajenga njia za umeme wa msongo wa kilovolti 33 kwa ajili ya
wananchi wanaoishi kando kando na njia kuu ya umeme kwa ufadhili wa NORAD, SIDA
na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Aliongeza kuwa mradi
huo utatekelezwa na REA pamoja na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ambapo
jumla ya vijiji 91 vitafaidika na mpango huo.
Mradi wa Backbone
ulianza kutekelezwa Novemba 2013 chini ya Mshauri Mwelekezi (OISF) – Fitchner
kutoka Ujerumani kwa kushirikiana bega kwa bega na Wahandisi wa TANESCO.
--