Tuesday, December 16, 2014

Hans Van Der Pluijm, Aanza kwa kishindo Yanga

YANGA imekata mzizi wa fitina baada ya kumshusha nchini kocha Mdachi, Hans Van Der Pluijm, mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika kwa miaka 14 na kumwonyesha mlango wa kutokea Mbrazil Marcio Maximo.
Yanga iko katika hatua za mwisho kumalizana na kocha huyo ambaye aliwahi kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu, kabla ya kutimkia Uarabuni.
 Pluijm alitua nchini saa 8:30 usiku wa kuamkia jana Jumanne, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na moja kwa moja alielekea katika hoteli ya TANSOMA, iliyopo eneo la Gerezani, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kabla ya kufanya mazungumzo na mabosi wa timu hiyo jioni.
Pamoja na kwamba bado hajaingia rasmi mkataba wa kukinoa kikosi cha Wanajangwani hao, lakini tayari amekwishaanza mambo akiwa nje ya mkataba.
Katika mahojiano maalumu na DIMBA Jumatano yaliyofanyika hotelini alikofikia, Pluijm alisema bado ana imani kuwa Yanga itafanya vizuri siku zijazo.
Alisema bado hajakubaliana mambo kadhaa na viongozi wa Yanga, lakini leo Jumatano asubuhi atakutana nao tena kumalizana nao kila kitu.
"Bado kuna vitu havijakaa sawa, kesho (leo Jumatano) tunakutana tena kumalizia baadhi ya vitu, baada ya hapo mambo yatakuwa safi," alisema Pluijm.
Alisema amekuja na mipango na mikakati mingi, kwa hivi sasa yupo kwenye mazungumzo hayo ya mwisho na Yanga na kwamba baada ya kukamilisha suala la mkataba ataweka bayana mikakati yake yote ya kazi.
Ingawa hakufafanua ni nini atakachokifanya, lakini kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa Yanga, kocha huyo amewaahidi mambo matatu makubwa ya msingi atakayoyafanya, akianza na soka safi, kurejesha ubingwa Jangwani na kuifikisha timu mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka barani Afrika hapo mwakani.
Amesisitiza kuwa ingawa ni mapema mno kueleza nini atakifanya kwa ajili ya kuifanya Yanga kuwa timu bora Tanzania na nje ya mipaka, lakini suala kubwa lililopo mbele yake ni kutaka kuiona timu hiyo ikiwa bora.
"Unajua Yanga ni timu kubwa, lakini ina falsafa zake ambazo binafsi nimeweza kuzifahamu kwa undani, lakini ukweli uliopo ni kwamba bado ni mapema kusema lolote kubwa kwa kuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kati yangu na viongozi wangu wa Yanga.
"Kuna mambo ya kufanya kabla, ila hivi sasa naweza kuweka kiporo hadi baada ya baadhi ya mambo yakamilike, nadhani baada ya siku mbili au tatu kila kitu kitakuwa wazi, ingawa nataka niwaambie Wanayanga na wapenzi wa soka kwamba nitajitahidi kadiri inavyowezekana ili timu iwe bora.
"Mimi sina mengi kwa sasa, lakini sijabadilika, ni yule yule na kwamba kazi yangu nitaanzia pale nilipoiacha Yanga, kwani ni timu ninayoifahamu na kuipenda, pia wachezaji waliopo ni wale niliowaacha,” alisema Kocha huyo, ambaye taarifa zilizopo zinaeleza kuwa ni mwanachama wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Pluijm amekuwa mgumu kumtaja msaidizi anayeona atamfaa hadi hapo baadaye, ingawa taarifa ambazo DIMBA Jumatano linazo ni kwamba chaguo lake la kwanza ni Charles Boniface Mkwasa, ambaye walishafanya naye kazi katika msimu wa mwaka jana.
"Hilo ni jambo la baadaye, lakini kinachotokea ni kwamba atakayekuwepo nitaweza kufanya naye kazi, ingawa nisema kweli kuwa ni mapema kusema lolote kwa wakati huu, naomba tusubiri tukamilishe mazungumzo na uongozi kisha nitasema yote hayo," amesisitiza kocha huyo.
Rekodi ya Pluijm alipoifundisha Yanga kwa mara ya kwanza inaonyesha kwamba aliiongoza timu hiyo katika mechi 18, zikiwemo za Ligi Kuu, Klabu Bingwa Afrika na mechi za kirafiki ambapo kati ya hizo zote alishinda mechi 11, akatoka sare mechi sita na kupoteza mbili.
Kabla ya kujiunga na Yanga kwa mara ya kwanza, Pluijm (65) alishafanya kazi na klabu mbalimbali za Afrika, ikiwemo Belkum Chelsea ya Ghana pamoja na Saint Gorge ya Ethiopia.
Wakati huo huo, aliyekuwa kocha msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema kuwa yeye bado ana mkataba na klabu hiyo, kwani alipoondoka nchini kwenye kufundisha nje ya nchi aliomba likizo ya bila malipo.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwa na fununu kwamba kocha Pluijm yupo kwenye hatua za mwisho za kuingia mkataba wa miaka miwili na Yanga, huku Mkwasa akipewa nafasi kubwa ya kurudia kwenye nafasi yake ya awali.
Mkwasa aliliambia DIMBA Jumatano kwamba iwapo Yanga itaamua kumrudisha kwa ajili ya kuinoa timu hiyo yeye yupo tayari, lakini hadi sasa bado hana taarifa yoyote ya yeye kuhitajika kwenye klabu hiyo.
"Sina taarifa yoyote juu ya kuhitajika Yanga, lakini kama wakinihitaji nipo tayari kurudi kufundisha kwa sababu mimi bado nina mkataba na Yanga, kwa kuwa wakati naondoka niliomba likizo bila malipo,” alisema Mkwasa, ambaye ni kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo.
Yanga imeamua kuvunja benchi la ufundi lililokuwa likiongozwa na kocha Marcio Maximo, baada ya timu hiyo kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao, Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe, iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini pia uongozi wa timu hiyo kutoridhishwa na mwenendo wa kocha huyo wa kujiamulia kila kitu.

*********

No comments:

Post a Comment

MWENGE WA UHURU WAINGIA GAIRO NA KUZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA MILIONI MIASABA NA ZAIDI

 Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe akipokea Mwenge kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Morogoro Regina Chonjo mara ulipofika katika eneo la Ma...