Tuesday, December 16, 2014

Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Weerema ajiuzulu

Jaji Werema ajiuzulu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye ni mmoja wa watuhumiwa katika kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ametangaza kujiuzulu.
Hatua hiyo ya Werema imekuja wakati Watanzania wakiwa bado wanasubiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete,  juu ya maamizio nane ya Bunge yaliyotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyekagua miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika maazimio ya Bunge baadhi ya viongozi ambao chombo hicho kiliona wana makosa na kutaka mamlaka zao za uteuzi ziwachukulie hatua ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaujuka, Jaji Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa ya TANESCO.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana inasema, kutokana na uamuzi wa Jaji Werema, Rais Kikwete amekubali ombi la kujizulu kwa mwanasheria huyo.
Ilisema kuwa, katika barua yake, Jaji Werema amesema ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.
“Kuanzia leo (jana), Desemba 16,  2014 na Rais Jakaya Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Jaji Werema na amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu
Wabunge wafunguka


Sendeka
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mbunge wa Simanjiro, Chripher Ole Sendeka (CCM), alisema hatua ya kujiuzulu kwa Jaji Werema pekee haitoshi ila sheria ichukue mkondo wake kwa watu wote walioliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Kwa alichelewa kufanya hivyo na hii haitoshi kwa Jaji Werema pekee kujiuzulu ila hatua za kisheria zichukuliwe kwa watu wote waliotajwa ikiwemo kwa Rais Kikwete kuwawajibisha wale wote waliotajwa katika kashfa hii na kubainika kama Bunge lilivyopendekeza,” alisema Sendeka.


Maazimio ya Bunge
Novemba 29, mwaka huu Bunge lilipitisha maazimio manane baada ya maridhiano kati ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kambi ya Upinzani, upande wa wabunge wa chama tawala CCM pamoja na Serikali.
Baadhi ya maazimio hayo ni lile lililosema “ Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;
Kwa kuwa , Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;
Hhivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo,”.
Pia lilipitisha azimio la kuwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge ambao ni Victor Mwambalaswa (Kamati ya Nishati na Madini), William Ngeleja (Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Kamati ya Bajeti).
Chenge na Ngeleja wametajwa kunufaika na mgawo wa fedha hizo ambapo Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani wa Serikali alipewa mgawo wa Sh bilioni 1.6  huku Ngeleja akipewa Sh milioni 40.2.

No comments:

Post a Comment

MWENGE WA UHURU WAINGIA GAIRO NA KUZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA MILIONI MIASABA NA ZAIDI

 Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe akipokea Mwenge kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Morogoro Regina Chonjo mara ulipofika katika eneo la Ma...