Friday, February 20, 2015

MELI NYINGINE KUBWA YENYE UREFU WA MITA 209 YATIA NANGA BANDARI YA MTWARA
Mabadiliko ya teknolojia pamoja na kuboreshwa kwa bandari zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) zimeanza kuzaa matunda baada ya meli nyingine kubwa yenye urefu wa mita 209 kutia nanga Bandari ya Mtwara.


Ujio wa meli hiyo iliyotia nanga katika Bandari ya Mtwara ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini baada ya Bandari ya Dar es Salaam na Tanga umefanya jumla ya meli kubwa na za kisasa zilizotia nanga katika bandari zetu nchini kufikia tatu.


Meli nyingine kubwa na ya kisasa kuja nchini kwa mara ya kwanza ilikuwa ni Maersk Cubango mali ya Maersk Line iliyokuwa na urefu wa mita 250 na upana wa mita 38 ikiwa na uwezo wa kubeba kontena 4,500.


Kabla ya ujio wa meli hiyo, Meli kubwa nyingine ni MSC Martina yenye urefu wa mita 244 na upana wa mita 32.2 ikiwa na uwezo wa kubeba makontena 2,411 pia ilifanikiwa kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni.


Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Bandari ya Mtwara kupokea meli kubwa yenye urefu wa mita 209 ikilinganishwa na meli ambayo iliwahi kutia nanga katika Bandari ya Mtwara ambayo ilikuwa na urefu wa mita 205. 


Meli hii kubwa iliingia Bandarini Mtwara tarehe Februari 04, 2015 ikiwa na jumla ya Makontena 1,240 ambayo yalishushwa na kupakia Makontena 1,027 yaliyosheheni Korosho. 


Kitu pekee kilichokuwa kivutio wakati wa kuingia kwa meli hiyo ni umaridadi wa Kapteni wa Bandari ya Mtwara Kapteni Hussein Kasugulu kuingiza meli kwa kutumia ‘Tug’ moja tu ambapo ni vitu adimu kwa Bandari nyingine kufanyika. Kwa kawaida meli huingizwa katika bandari kwa kutumia ‘Tug’ mbili.


Meli hiyo inatarajiwa kuondoka Bandarini hapa baada ya siku tano, ikishasheheni shehena ya mzigo wa korosho ambalo ni zao kuu la biashara katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania, haswa Mtwara.

No comments:

Post a Comment

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NI TISHIO KWA AFYA YA MAMA NA MTOTO NCHINI

                         Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii  Serikali imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kwa ...