Saturday, March 28, 2015

Gwajima alivyojisalimisha kituo cha Polisi

 Askofu gwajima akishuka ndani ya gari
 Askofu gwajima akiongozana na wanasheria wake kuelekea Polisi akitokea mtaa wa Samora

ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tano kuhusu kauli kali alizozitoa dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Gwajima alifika kituo cha polisi majira ya saa 8:22 mchana akitembea kwa miguu na kueleza kuwa amechelewa kwa sababu ya foleni kali iliyokuwepo barabarani.
Wakati akiingia kituoni hapo, Askofu Gwajima alikuwa ameongozana na Mwanasheria wake, John Malya pamoja na baadhi ya waumini wa kanisa analoliongoza.

Kabla ya kuingia ndani kwa ajili ya mahojiano, Askofu Gwajima alizungumza na waandishi na habari na kueleza kuwa ameshangazwa na wito alioupata kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alimtuhumu kumtukana na kumkashafu Kardinali Pengo wakati alikuwa akitekeleza kazi ya kitume.

Askofu Gwajima aliwaambia waandishi wa habari kuwa kauli yake ambayo imesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii aliitoa baada ya Kardinali Pengo kuwageuka wenzake katika Baraza la Maaskofu Tanzania linalounganisha maaskofu wa Kanisa Katoliki, Pentekoste na Jumuiya ya Kikristo Tanzania.

“Maaskofu wote kwa pamoja tulikubaliana kuwa hawataki Mahakama ya Kadhi na tulisaini tamko na alikubali lakini nashangaa alitugeuka.

“Mimi kama kiongozi wa kiroho nikaona nimkemee kiongozi mwenzangu wa kiroho aache mambo ambayo si mazuri. Hakuna maneno ya kashfa ambayo nimeyatoa. Niliyoyatoa ni maneno ya Mungu yanayotumiwa kumwongoza mtumishi wa Mungu,” alisema Gwajima.

Baada ya Askofu Gwajima kuingia polisi, Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa ametii amri ya jeshi hilo kama alivyotakiwa.

Kamanda Kova alitafanyiwa mahojiano katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP, Costantine Massawe.

Alizitaja tuhuma zinazomkabili Askofu Gwajima kuwa ni kumkashfu na kumtukana hadharani kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Kardinali Pengo.

“Taratibu za kuhojiwa zinafanyika kwa mujibu wa sheria na mtuhumiwa atapewa haki zote anazostahili ikiwemo kuwa na ndugu yake wa karibu, rafiki anayemwamini au wakili wake.

“Kama ilivyo kawaida utakusanywa ushahidi kutoka pande zote za shauri hilo ili kubaini ukweli wa jinsi tukio hilo lilivyotokea,” alisema Kova.

Kova alisema baada ya kukamilika taratibu za awali, zitafuata taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya kitaalamu na ya kisheria ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka.

“Ili ufanisi upatikane katika upelelezi wa shauri hili ni muhimu kupata ushirikiano kutoka kwa kila atakayetakiwa kulisaidia Jeshi la Polisi kukamilisha haraka upelelezi wa shauri hili ambalo limepata mvuto mkubwa kwenye jamii,” alisema Kova.

Kwa takribani wiki moja sasa Askofu Gwajima amekuwa akisikika katika mitandao mbalimbali ya kijamii akitoa lugha kali dhidi ya Kardinali Pengo anayemtuhumu kuwasaliti maaskofu wenzake dhidi ya msimamo walioufukia kwa pamoja kuhusu upigaji kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Askofu Gwajima katika matamshi yake anamtuhumu Kardinali Pengo kusaliti Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kuwataka waumini waisome Katiba Inayopendekezwa kisha wapewe uhuru wa kupiga kura ya ndiyo au hapana tofauti na azimio la pamoja la maaskofu hao. waandishi mbalimbali wa habari wakijaribu kutafuta picha za tukio hilo

 Gwajima akihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari kabla ya kuingia ukumbini

 wafuasi wake waliokuwa nje

No comments:

Post a Comment

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NI TISHIO KWA AFYA YA MAMA NA MTOTO NCHINI

                         Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii  Serikali imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kwa ...