YALIYOFANYIKA KITAIFA MKOANI MOROGORO
TAREHE 8 MACHI, 2015
Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Waheshimiwa Wabunge;
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro na Viongozi Wengine
wa Vyama vya Siasa na Mashirika ya Dini;
Waheshimiwa Viongozi na Watendaji wa Serikali;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Waheshimiwa Viongozi na Watendaji wa Serikali;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri
Sophia Simba kwa kunialika na kunishirikisha katika sherehe za mwaka huu za
Siku ya Wanawake Duniani. Nakupongeza
sana wewe na wenzako wote Wizarani na Mkoani Morogoro kwa maandalizi mazuri ya
sherehe hizi. Hakika mambo yamefana sana. Niruhusuni
pia nitoe shukrani maalumu kwa ndugu zetu wa Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa
Mkoa, Dkt. Rajabu Rutengwe kwa mapokezi mazuri na ukarimu wenu. Vile vile nawapongeza kwa kukubali kubeba
mzigo huu wa kuwa wenyeji wa sherehe hizi.
Natambua kuwa si kazi rahisi lakini mmeweza kufanikisha kwa kiwango cha hali
ya juu sana. Maonyesho ni mazuri na
ukichanganya na jinsi wanawake walivyojitokeza kwa wingi tena wakiwa na nyuso zenye
bashasha tele na kuvalia vizuri, kama ilivyo sifa ya wanawake wa Tanzania,
hakika mmetia fora. Mmezikonga nyoyo
zetu kiasi cha kutufanya tutamani kuja tena Morogoro. Nawapeni pole kwa maafa
yaliyotokea. Nawapongeza kwa jinsi
mlivyojijenga upya haraka. Nitakuja
kuwatembelea baadea ya sherehe.
Ndugu Wananchi;
Leo ni siku adhimu kwa wanawake wa
Tanzania na wanawake wote duniani. Ni
siku yenu maalumu ya kuifurahia na kushangilia mafanikio mliyopata na kuweka
msimamo kuhusu namna ya kukabili changamoto zilizowakabili sasa na
zitakazojitokeza siku za usoni. Shamrashamra za akina mama waliojitokeza kwa
wingi zinajieleza zenyewe kuwa leo ni siku ya furaha, siku ya kujipongeza na
kusherehekea mafanikio ya wanawake wa Tanzania.
Hakika wanawake wa Tanzania wanayo kila sababu ya kusherehekea maana
tumepiga hatua kubwa na ya kutia moyo katika jitihada za ukombozi na maendeleo
ya mwanamke nchini. Kwa niaba yenu nawashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa
Mashirika ya Kimataifa kuja kujiunga nasi siku ya leo.
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya
Wanawake Duniani yana mambo mawili muhimu yanayoenda nayo sambamba. Kwanza, kwamba huu ni mwaka wa 20 tangu
kutolewa kwa Tamko la Beijing kuhusu Maendeleo ya Wanawake duniani. Kama mjuavyo nchi yetu ilipata heshima katika
mkutano ule wa 1995 pale Beijing kubwa kwa Mama Getrude Mongela kuwa Mwenyekiti
wake. Hivyo basi, maadhimisho ya mwaka
huu ni fursa nzuri ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Tamko la Beijing miaka
20 baadae.
Pili kwamba, maadhimisho
ya mwaka huu ni fursa ya kujadili namna nchi yetu itakavyojipanga kutekeleza
uamuzi wa Umoja wa Afrika kuhusu uwezeshaji wa wanawake kimaendeleo kuelekea
Ajenda ya Afrika ya mwaka 2063. Katika
mkutano uliopita wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika tuliazimia kuwa
mwaka 2015 uwe ni wa kutoa msukumo maalum kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake
Kimaendeleo. Waziri Sophia Simba
alishiriki mkutano maalumu wa Mawaziri kuandaa agenda hiyo ya kikao cha Wakuu
wa Nchi. Nilimwambia pale Addis Ababa
kuwa, atakaporudi aongoze katika kupanga mikakati na mipango ya kutekeleza azma
hiyo ya Afrika hapa nchini. Naamini kazi
hiyo imeanza. Bila ya shaka ndiyo maana
basi kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Uwezeshaji Wanawake;
Tekeleza, Wakati ni Sasa”.
Utekelezaji wa Tamko la Beijing
Ndugu Wananchi;
Kama
nilivyokwishagusia awali, mwaka huu, Tanzania inajiunga na mataifa mengine
duniani kuadhimisha miaka 20 ya utekelezaji wa Tamko la Beijing na Mpango Mkakati
wa utekelezaji wa tamko hilo. Tamko la
Beijing lilisheheni mambo mengi yanayohusu haki, hadhi na maendeleo ya mwanamke kwa lengo la kutoa
fursa sawa kwa wanawake na kulinda utu wao dhidi ya dhuluma na ukandamizwaji wa
mfumo dume.
Mwaka huu, kila nchi inatakiwa kuwasilisha
taarifa ya utekelezaji wake katika mkutano utakaofanyika tarehe 09 - 20 Machi,
2015 kule New York, Marekani. (59th Commission on the Status of
Women Agenda Beijing +20) Nafurahi
kuwaarifu kuwa Tanzania itakwenda kwenye mkutano huo kifua mbele. Tumetekeleza Tamko la Beijing kwa mafanikio
makubwa hasa kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi; Haki za Kisheria za Wanawake; Afya za
Wanawake; na Usawa Katika Elimu, Mafunzo, Ajira na Nafasi za Uongozi na Uamuzi. Ripoti ya nchi yetu iliyoandaliwa na Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ikishirikiana na wadau wengine imeyaeleza mafanikio
haya kinagaubaga. Bila ya shaka
tumemsikia Waziri Sophia Simba akiyazungumzia baadhi ya mambo. Nikuombe tu utafute wasaa mzuri uyafafanue
vizuri kupitia vyombo vya habari ili watu wasikie. Tuelezee yale tuliyofanikiwa na yale ambayo
tunawajibika kuongeza nguvu na kasi zaidi.
Sema usikike vinginevyo unaacha ombwe la wasiotutakia mema kupotosha
ukweli.
Uwezeshaji Kiuchumi
Ndugu Wananchi;
Uwezeshaji wa
wanawake kiuchumi ni jambo ambalo hapa Tanzania tumelipa kipaumbele cha
juu. Imekuwa hivyo kabla na baada ya Azimio
la Ulingo wa Beijing. Napenda kuanza kwa
kutambua jitihada za makusudi za kuwawezesha wanawake kupata fursa za mikopo
tulizofanya. Mfuko wa Maendeleo ya
Wanawake (WDF) ulianzishwa kwa madhumuni hayo.
Hali kadhalika, Serikali ilihimiza kuanzishwa kwa Vyama vya Kuweka na
Kukopa (SACCOS), VICOBA na asasi mbalimbali za micro-finance ambazo
zimenufaisha wanawake wengi. Hali
kadhalika, Serikali imesaidia katika uanzishwaji wa Benki ya Wanawake Tanzania mwaka
2009. Benki ya Wanawake imepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kweke. Akaunti zimefikia 33,615, ina matawi mawili
Dar es Salaam na vituo 81 vya mikopo na mafunzo Dar es Salaam, Dodoma,
Iringa, Njombe, Ruvuma, Mara na Mwanza. Kati
ya Januari 2011 na Machi, 2014, Benki hii imetoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 24,342,382,000 kwa watu
11,754 ambapo asilimia 88 ya watu hao ni wanawake.
Aidha, Benki hii imewafikia wateja wanawake 19,000 kati ya mwaka 2009 na 2013.
Kwa Benki ya umri wa miaka mitano, huu ni mwanzo mzuri. Sisi katika Serikali tutaendelea kuiwezesha
benki hii kwa kuiongezea mtaji ili iweze kupanua shughuli zake na kuongeza matawi
yake nchini. Lengo letu ni kuiwezesha
kuwafikia wanawake wengi kadri inavyowezekana.
Tunataka wanawake wajue kuwa Benki hii ni yao na ipo kwa ajili yao. Kwa
jumla, hatua hizo zimewawezesha wanawake wengi kupata mikopo waliyoitumia
kufanya shughuli za kuboresha mapato yao na hali zao za maisha yao na familia
zao.
Kwa hakika yapo mambo
mengi yanayothibitisha kuwa tumepiga hatua ya kutia moyo katika uwezeshaji wa
wanawake kiuchumi. Upo ushahidi, kwamba,
ushiriki wa wanawake katika sekta ya biashara ndogo na kati (SME) umeongezeka
sana. Katika ripoti ya Mapitio ya Sera
ya Biashara za Kati na Ndogo ya mwaka 2013, kwa mfano, inaonyesha kuwa wanawake
wanamiliki asilimia 64 ya biashara
hizo nchini. Nyingi zipo kwenye sekta
isiyo rasmi. Aidha, utafiti wa hali ya
uchumi ya mwaka 2010 (THDS) unaonyesha kuwa asilimia 23 ya wanawake wana kipato kinachozidi au kulingana na
waume zao.
Wanawake wanaoshiriki kwenye maonyesho ya
kibiashara wameongezeka kutoka 2,000 mwaka
2005 hadi 5,000 mwaka 2013. Wakati
mwingine huhitaji hata takwimu kujua ukweli huu. Ukitembelea mabanda ya maonyesho ya bidhaa,
maduka na masoko utaziona bidhaa nyingi za usindikaji zinazozalishwa na akina
mama.
Ndugu Wananchi;
Siku hizi akina mama wanaokwenda
kununua bidhaa nje ya nchi hasa Dubai, China, Hong Kong, Bankok, Uturuki na
kwingineko wamekuwa wengi sana. Takwimu
zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2014 wanawake 2,243
walikwenda China kununua bidhaa mbalimbali.
Zamani haikuwa hivyo. Hivi sasa wanawake
siyo tu wanao uwezo wa kiuchumi bali pia hawana woga wa kusafiri masafa ya
mbali. Leo hii familia nyingi
zinaendeshwa na akina mama wajasiriamali. Huu ni ukweli ulio wazi. Sishangai kusikia kwamba baadhi ya wanaume
wanaanza kutishika hata kusababisha kusikika kuwana mawazo ya kuanzisha vyama
vya kutetea haki za wanaume. Kina mama kazeni buti, msirudi nyuma. Mnafanikiwa.
Wanaume wanaolalama waacheni walalame.
Ndugu Wananchi;
Hapana ubishi kuwa
ukiwawezesha wanawake kiuchumi unaondoa umaskini katika familia. Familia ambazo mama na baba wana kipato hali
yao ya maisha ni bora zaidi. Sisi
Tanzania, asilimia 51 ya Watanzania
ni wanawake. Bahati mbaya sana kwa
sababu ya mila zetu na hasa ukatili na uonevu wa mfumo dume unaotawala sasa,
wanawake wanaongoza kwa idadi ya kuwa maskini.
Hivyo basi, kuwawezesha wanawake kiuchumi ndio ngazi ya kupandia katika
kupunguza umaskini wa wananchi na nchi kupata maendeleo. Ndiyo sababu, kwa upande wetu, Serikalini
uwezeshaji wa wanaweke si jambo la kisera tu, bali ni la kimkakati na lipo
kwenye mipango. Katika kufikia shabaha
za Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa 2025 ya kuwa taifa la uchumi wa kati, nafasi
ya wanawake imetambuliwa. Ni sera ya
msingi ya Serikali yetu kuendelea kuwawezesha wanawake hadi atakapokombolewa
mwanamke wa mwisho kutoka kwenye lindi la umaskini.
Ndugu Wananchi;
Naomba mtambue kuwa, tunapofanya hivi
hatufanyi upendeleo kwa wanawake kwa ajili ya kujifurahisha wala kulipa fadhila,
bali tunatimiza wajibu wetu wa msingi wa kutenda haki kwa kila raia. Tunawarudishia wanawake haki yao na stahili
yao, ambayo jamii iliwapokonya kwa muda mrefu.
Wanawake na wanaume ni sawa katika ubinadamu na utu wao. Kwa ajili hiyo wanawake hawastahili
kubaguliwa, kudhulumiwa na kufanyiwa uonevu na ukatili wa aina yo yote..
Haki za Kisheria za Wanawake
Ndugu Wananchi;
Tumepiga hatua kubwa kwa upande wa
kuweka mazingira mazuri ya kisheria ya kulinda utu wa wanawake, heshima na
fursa za kiuchumi na kijamii. Tangu
mwaka 1995, baada ya Tamko la Beijing, tumetunga Sheria nyingi zenye kuwapa
haki wanawake dhidi ya mila na desturi potofu na zilizo kandamizi kwao. Kwa mfano, mwaka 1998 tulitunga Sheria ya
Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ambayo imeainisha adhabu kali ikiwemo kifungo cha
miaka 30 kwa makosa ya ubakaji, kutembea na wanafunzi na udhalilishaji mwingine
wa kijinsia.
Jambo lingine lililowekewa Sheria ni
kuhusu wanawake kumiliki ardhi. Sheria
ya Ardhi Namba 4 na Sheria ya Ardhi ya Kijiji Namba 5 za mwaka 1999 zimeleta
mapinduzi makubwa kwa kuwapa wanawake haki ya kumiliki ardhi. Sheria ile ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002
chini ya Sheria Na.2 kwa kuunda Mabaraza ya Ardhi ambayo lazima Wajumbe wasiopungua
watatu, kati ya saba, wawe wanawake ili kuwapa sauti kwenye uamuzi uhusuo
ardhi.
Mwaka 2008 tukatunga Sheria nyingine
mbili muhimu nazo ni ile ya Mikopo ya Nyumba (Mortgage Finance Special Provision
Act) na ile ya umiliki wa kitalu au nyumba (Unit Titles Act). Sheria hizi mbili zinasaidia kuwakinga wanawake
dhidi ya dhuluma pale ambapo mume atauza ardhi au nyumba ambayo wamechuma
pamoja bila idhini ya mkewe.
Ndugu Wananchi;
Katika Katiba Inayopendekezwa haki ya wanawake
kumiliki ardhi imetambuliwa rasmi na kuingizwa.
Hivyo basi, Katiba Inayopendekezwa ikipita itakuwa ni ukombozi wa aina
yake kwa wanawake. Aidha, imekomelea
masuala mengine muhimu kwa haki za wanawake.
Miongoni mwayo ni lile suala la usawa katika vyombo vya uamuzi ambako
sasa inapendekezwa kuwa Bungeni idadi ya Wabunge wanawake na wanaume iwe nusu
kwa nusu (fifty fifty). Masuala haya
mawili na mengineyo ni muhimu kwa maslahi na maendeleo ya wanawake sasa yatakuwako
kikatiba na sio tu kisheria pekee kama Katiba Inayopendekezwa itapita.
Ndugu Wananchi;
Ni vyema kutambua pia kuwa haya yamewezekana
kutokana na ushiriki mpana na mzuri wa wanawake kwenye mchakato wa Katiba
unaotarajiwa kuhitimishwa kwa Kura ya Maoni mwezi ujao. Katika Tume ya Marekebisho ya Katiba, wanawake
walikuwa asilimia 30, na katika
Bunge Maalumu la Katiba wanawake walikuwa 256
kati ya Wajumbe 620 wa Bunge hilo,
yaani walikuwa asilimia 41.2. Aidha, kulikuwa na mtandao wa Wanawake na
Katiba uliohusisha asasi 110.
Ombi langu kwenu akina mama,
jitokezeni nyote mjiandikishe kupiga kura na siku hiyo ikifika muweze kuipigia
kura ya NDIYO Katiba Inayopendekezwa. Itakuwa
Katiba mkombozi wa wanawake. Itaondoa
vikwazo vyote vikubwa kwa maendeleo na ustawi wa wanawake nchini. Msikubali kuachwa nyuma mkapoteza fursa hii
ya aina yake.
Afya kwa Wanawake
Ndugu Wananchi;
Tumepiga hatua ya
kutia moyo kwa upande wa haki ya wanawake kupata huduma ya afya katika miaka 20
ya uhai wa Tamko la Ulingo wa Beijing. Ni
ukweli ulio dhahiri kuwa hali ya afya ya wanawake ni bora zaidi leo kuliko
ilivyokuwa miaka 20 iliyopita. Ninyi ni
mashahidi wa juhudi zetu za kupambana na mila potofu na hasi kama vile ukeketaji,
ndoa za utotoni na mengineyo. Mafanikio
yameanza kuonekana. Tumesimamia na
kuhimiza sana kuhusu uzazi wa mpango ambao unatoa fursa kwa mwanamke kupanga
uzazi wake.
Mageuzi makubwa
katika huduma ya afya nchini yamejumuisha afya ya wanawake. Tumeyafanya hivyo kupitia
Mpango wa Taifa wa Miaka Kumi wa Afya ya Msingi (MMAM 2007 – 2010) na Progamu
kadhaa maalumu. Kipaumbele cha juu
kimetolewa kwa afya ya mama na mtoto. Upanuzi mkubwa na uboreshaji wa huduma ya afya
ya msingi pamoja na ya uzazi kusogezwa karibu na wanapoishi watu imesaidia sana
kuboresha afya ya wanawake na watoto na kuokoa maisha yao. Vituo vya afya na zahanati nyingi na mpya
zimejengwa na kuboresha zilizopo. Hiyo
imeongeza na kuboresha huduma ya afya kwa wanawake vimejengwa na watoto. Kwa ajili hiyo, vyumba vya kujifungulia kwa
kina mama vilijengwa katika vituo vya afya na zahanati zilizokuwa hazina. Kwa sababu ya umbali wa kwenda kujifungulia
kupungua, idadi ya wanawake wanaojifungua katika mikono salama imeendelea
kuongezeka na kufikia asilimia 51 mwaka
2014. Ndiyo maana na vifo vya akina mama
vinavyotokana na uzazi nchini vimeendelea kupungua.
Mwaka 2005 wanawake 578 walifariki
kwa kila uzazi salama 100,000 na kupungua hadi 432 mwaka 2012. Juhudi zetu na matokeo haya yanawakilisha
dhamira yetu ya kumfikia kila mwanamke na huduma hizi za afya mahsusi kwa
wanawake. Hata hivyo, bado ni vifo vingi
mno, hatuna budi kuongeza bidii.
Tunataka hata mwanamke mmoja asipoteze maisha katika tendo la kumpa uhai
mwanadamu mwingine. Tutaendelea kuboresha
huduma ya afya kwa wanawake ili hatimaye wanawake wote wanufaike na kunusurika
na vifo vinavyoweza kuzuilika.
Wanawake Katika Uongozi na Ngazi ya Uamuzi
Ndugu Wananchi;
Jambo ambalo hatujalifanyia
ajizi ni kuwezesha wanawake kuingia kwenye uongozi na ngazi za uamuzi. Tanzania ni mojawapo ya nchi 20 duniani na ya tano Afrika zenye
Wabunge wanawake zaidi ya asilimia 30. Sisi tunao Wabunge wanawake 126 kati ya 356 sawa na asilimia 36. Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
wanawake ni 29 kati ya 80 sawa na asilimia 36. Aidha, Spika wa
Bunge letu ambaye ni kiongozi wa mmoja wa mhimili mkuu wa dola ni mwanamke,
dada yantu Anna Semamba Makinda. Kwa
upande wa Mawaziri, idadi yao nao imekuwa ikiongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2004, asilimia 27 mwaka 2009, na asilimia 31 mwaka 2013. Hali
kadhalika, kwa upande wa Majaji wa Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu ambao idadi
yao wote ni 97 kati yao 30 ni wanawake. Hii ni sawa na asilimia 39.2. Haya ni mageuzi makubwa sana katika
Mahakama.
Kwenye ushiriki wa wanawake katika
nafasi za uamuzi tumefanikiwa sana hata kuliko baadhi ya mataifa makubwa. Kwa mfano Uingereza
wanawake ni asilimia 22 tu ya
Wabunge wote katika Bunge la umri karne saba na nusu.
Ndugu Wananchi;
Kutoa fursa na
nafasi za uongozi na uamuzi kwa wanawake ni matokeo ya mkakati wa makusudi wa Serikali
yetu kwa kutekeleza Sera za Chama Tawala.
Tumefanya hivyo kwenye Katiba, kwenye Sheria na hata Kanuni
mbalimbali. Hata katika utumishi wa umma
kwa mfano, tumeleta mabadiliko makubwa kwa kuingiza kipingele cha 12(4) cha
Kanuni za Utumishi wa Umma za 2013 kisemacho, “Inapotokea mwanamke na mwanaume wametimiza vigezo sawa kwa kulingana,
basi kipaumbele atapewa mwanamke”. Uamuzi
kama huu wa kimapinduzi umesaidia sana kuongeza wingi wa wanawake katika ngazi mbalimbali
za utumishi wa umma. Nina matumaini kuwa
katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu wanawake wengi zaidi watajitokeza kugombea
Udiwani, Uwakilishi, Ubunge na hata Urais.
Wapo wanawake wenye uwezo kwa nafasi hizo zote. Msikubali kuachwa nyuma. Msikubali kutishwa mkatishika.
Ndugu Wananchi;
Tunapofanya tathmini
hii leo, tunaridhika kuwa tumepiga hatua kubwa katika kuendeleza hali, utu na heshima
ya mwanamke nchini. Inatia moyo kuona kuwa
hali hiyo inaonekana katika nyanja zote.
Jitihada zetu za kutoa fursa sawa kwa wote zinafanikiwa. Leo hii, katika elimu ya msingi wasichana ni asilimia 50.6 na wavulana asilimia 49.41, katika elimu ya
sekondari wavulana ni asilimia 52.1 na
wasichana ni asilimia 47.9. Ndio maana haishangazi kuwa katika wanafunzi
10 bora katika mtihani wa mwaka 2013 wa Sekodnari saba ni wanawake. Katika VETA wasichana wameendelea kuongezeka
na kufikia asilimia 38.5 na wavulana
ni asilimia 61.5. Katika vyuo vikuu wasichana sasa ni asilimia 34.6 na wavulana ni asilimia 65.4. Tunaendeleza jitihada za kupanua fursa kwa
wasichana katika vyuo vikuu na VETA ili tufikie nusu kwa nusu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo, baada ya uchaguzi wa
Oktoba, 2015, nitastaafu. Kwa kweli, nitakwenda
kupumzika kwa amani nikijivunia kutenda haki na kutoa fursa nyingi kwa wanawake
nchini. Ninaridhika kuwa nitaacha msingi
imara wa haki za wanawake ambao naamini viongozi wetu wataofuatia watauendeleza
zaidi kama mimi nilivyojenga juu ya msingi uliojengwa na viongozi
walionitangulia. Mimi naamini wanawake wanaweza. Naamini pia kuwa kuwekeza kwenye maendeleo ya
wanawake ni kuwekeza kwenye mustakabali mwema kwa taifa. Napenda kurudia kusema kuwa kuwapa fursa
wanawake sio upendeleo, bali ni kuwapatia kilicho chao na kilicho haki
yao. Haya shime wote tuungane na
kuwawezesha wanawake. Aliwahi kusema
Mwanafalsafa na mshairi Alphonse Lamartine katika karne ya 19, aliyepata kuishi
kule Ufaransa, “kuna mwanamke mwanzoni mwa kila jambo jema na kubwa”. (There
is a women at the beginning of all great things). Nami naamini kuwa nchi yetu itakuwa imeendelea
pale tutakapompa kila mwanamke uhuru wa kujiendeleza. Nguvu kubwa ya wanawake ambayo sasa haitoi
mchango wake ipasavyo, itakapofanya hivyo nchi yetu itapaa
Inawezekana, timiza
wajibu wako.
Mungu Ibariki
Afrika
Mungu Ibariki
Tanzania
Asanteni kwa
kunisikiliza.