Friday, March 6, 2015

Wasira aruhusu uagizaji sukari kutoka nje

Na Humphrey Shao, Dar es Salaam
WAZIRI wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ameruhusu uagizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi ili kukabiliana na upungufu wa bidhaa hiyo nchini
Wasira alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo juu ya tatizo la kupanda ghafla kwa bei ya sukari tangu kusitishwa kwa uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Waziri huyo alisema wenye viwanda vya sukari pekee hawawezi kupewa kibali cha kuagiza sukari bali ni kwa mfanyabiashara yoyote yule ambaye atakidhi vigezo vitakavyowekwa.
“Nimegundua kuna siasa za sukari ambazo zinaendelea hivyo siwezi kukubali kuona wananchi wanaumia kwa ajili ya kundi la watu wachache ambao walisema wanayo sukari ya kutosha lakini tulipowaita waje kujieleza juu ya kiasi walichonacho wanasema hawana sukari hivyo kwangu naona hizi ni siasa kuliko uhalisia wa soko la sukari lililopo” alisema Wasira.
Katika ufafanuzi huo, Wasira alisema ameiagiza Bodi ya sukari kuweka vigezo vya watu watakaoweza kununu sukari kutoka popote pale duniani wafanye hivyo.
“Baada ya kuzuia kuingia kwa sukari ya nje wauzaji wa ndani waliweza kupandisha sukari ikawa bei juu kwa muda mfupi na tulivyo wauliza walisema sukari imewaishia hawana kabisa katika maghala yao” alisema.
Wasira alisisitiza msimamo wa serikali kuwa ni  kuhakikisha sukari inapatikana nchini kwa bei nzuri na kutoa mifano kuwa mtu aliyepo Mwanza hawezi kununu sukari kutoka Kagera kwa bei ya juu wala mtu wa Morogoro hapashwi kununua sukari kwa bei ya Sh. 2,200 kama ilivyo sasa.

Aliongeza kuwa serikali imekwishafanya mazungumzo na Kamishna wa TRA kuhakikisha sukari iliyozuiwa kwenye maghala inalipiwa kodi na kufika kwa wananchi ili kupunguza tatizo la sukari nchini.


No comments:

Post a Comment

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NI TISHIO KWA AFYA YA MAMA NA MTOTO NCHINI

                         Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii  Serikali imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kwa ...