KAMATI YA USIMAMIZI NA
UENDESHAJI YA BODI YA LIGI
Kocha Jackson Mayanja wa
Kagera Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kutoa
lugha ya kashfa kwa maneno na vitendo kwa waamuzi wa mechi yao na Mtibwa Sugar
kuwa walipewa rushwa.
Adhabu dhidi ya Kocha
Mayanja kwenye mechi hiyo namba 136 iliyochezwa Aprili 1, 2015 kwenye Uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu.
Klabu ya Mtibwa Sugar
imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya timu yake kukataa kuingia vyumbani
wakati wa mapumziko katika mechi namba 142 dhidi ya Stand United iliyochezwa
Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo
imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Nayo Simba imepigwa
faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu baada ya timu
yao kugoma kuingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo (changing room) kwenye Uwanja
wa Kambarage mjini Shinyanga wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar. Hatua hiyo
ilisababisha wachezaji wakaguliwe kwenye gari lao.
Pia Simba imepigwa faini
ya sh. 500,000 kwa kuzingatia kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu baada ya vilevile
kugoma kuingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo hiyo namba 146
iliyochezwa Aprili 6, 2015.
Kipa Tony Kavishe wa
Polisi Morogoro amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kosa
la kumpiga ngumi mwamuzi msaidizi namba mbili, Hassan Zani kwa kuzingatia
kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Alifanya kosa hilo kwenye mechi namba 147 dhidi ya
Mgambo Shooting iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
KAMATI YA MASHINDANO TFF
Kamati ya Mashindano ya
TFF ilikutana jana kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) pamoja
na taarifa ya Ligi Daraja la Pili (SDL) iliyomalizika hivi karibuni.
Katika matukio ya SDL,
Kamati imeipiga faini ya sh. 300,000 timu ya JKT Rwamkoma ya Mara kwa
kusababisha mechi yake dhidi ya AFC ya Arusha kuvurugika. Adhabu hiyo kwa mechi
hiyo iliyofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini
Arusha imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 28(4) ya Ligi Daraja la Pili.
Nao makocha wa JKT
Rwamkoma, Hassan Makame na Kamara Kadede wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila
mmoja na kufungiwa mechi sita kwa kumshambulia mwamuzi msaidizi namba moja
katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 9, 2015.
Wachezaji Shafii
Maganga, Saleh Ali, Ismail Salim na Mussa Senyange wa JKT Rwamkoma ambao
wanatuhumiwa kwa kushambulia mwamuzi kwenye mechi hiyo suala lao linapelekwa
kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi.
VPL KUENDELEA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
inatarajiwa kuendelea kesho jumatano katika viwanja viwili nchini, jijini Tanga
wenyeji Maafande wa Mgambo Shooting watawakaribisha timu ya Azam FC kwenye
Uwanja wa Mkwakwani.
Mjini Morogoro wakata miwa wa Mtibwa
Sugar watakua wenyeji wa maafande wa jeshi la Magereza nchini timu ya Tanzania
Prisons kutoka Mbeya, mchezo utakaopigwa katika dimba la Manungu Turiani.
TTF YAFUNGUA SEMINA YA WAAMUZI
VIJANA
Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa
Selestine leo amefungua rasmi semina ya waamuzi vijana wenye umri wa miaka 12-
17, inayofanyika katika hostel za TFF zilizopo Karume.
Akiongea na waandishi wa habari,
Mwesigwa amesema semina hiyo ya vijana imejumuisha vijana 27 kutoka mikoa
mbalimbali nchini kwa lengo la kuwaandaa kuwa waamuzi wa kimataifa baadae.
Vijana hawa mnaowaona hapa wanatoka
katika viuto vya kufundishia waamuzi vijana nchini, wakikua na kufuata misingi
ya kazi baadae watakua waamuzi bor nchini kwa sababu watakua wameanza tangu
wadogo na kufuata maelekezo ya wakufunzi wao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi
nchin Bw. Salum Chama akiongea na wandishi wa habari kabla ya kumkaribisha
katibu mkuu, amesema malengo yao ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na waamuzi wa
kimataifa wengi.
Mwaka huu Tanzania imeshika nafasi
ya pili kwa kutoa waamuzi 18 wenye beji za FIFA barani Afrika, nyuma ya Misri
yenye waamuzi 22, Lengo ni kuhakikisha tunawaanda vijana wengi waje kuwa
waamuzi wa kimataifa.
Semina hiyo ya siku 5 inatarajiwa
kufungwa ijumaa tarehe 17 Mei, 2015 inajumuisha vijana kutoka mikoa ya
Dar es salaam, Tanga, Zanzibar, Mwanza, Arusha na Mbeya, kati ya vijana 37
waamuzi wawili ni wanawake.
Wakufunzi wa semina hiyo ni Soud
Abdi, Riziki Majala na Joan Minja.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO
LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)