Wednesday, April 8, 2015

Okwi aipa mbinu Yanga

STRAIKA wa kimataifa wa Simba Mganda, Emmanuel Okwi, ameamua kuweka kando kinyongo chake kwa Yanga na kuipa mbinu za kuiua Etoile Du Sahel ya Tunisia kuelekea katika mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Itakumbukwa Okwi aliitema Yanga kimafia dakika za mwisho mwaka jana, kabla ya kufungwa kwa pazia la usajili wa msimu huu wa Ligi Kuu na kutimkia Simba.
Straika huyo ambaye aliwahi kuichezea Etoile du Sahel kwa miezi mitatu, ameamua kuisaidia Yanga ambayo ni timu pekee iliyosalia kwenye michuano ya kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuing'ata sikio kuhusu siri zote anazozijua kuhusu Waarabu hao watakaovaana na Yanga katika mechi za mzunguko wa pili wa michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Akizungumza na Mtoto wa Temeke  mara baada ya mchezo baina ya Simba na Kagera Sugar mjini Shinyanga, Okwi alisema, hakuna kinachoshindikana kwa Yanga kuitoa Etoile du Sahel iwapo watajipanga vya kutosha kuwakabili Waarabu hao wenye uzoefu na michuano ya kimataifa.
Timu hizo zitavaana Aprili 18, mwaka huu, ambapo Yanga itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye jijini Tunis.
Alisema, Yanga wanapaswa kuwa makini na Etoile du Sahel, kutokana na aina ya uchezaji wa timu hiyo ambayo inacheza soka la kushambulia mwanzo mwisho, kitu ambacho ni hatari kwa timu isiyokuwa na pumzi na viungo imara.
"Etoile ni wazuri sana, kwa muda niliokuwa kule nilichojifunza ni uchezaji wao wa kushambulia lango la wapinzani wao mwanzo mwisho, kitu ambacho kilikuwa kikitusaidia kupata ushindi mara pale unapokutana na timu ambayo haina viungo imara wenye uwezo wa kukabiliana na kasi yetu," alisema Okwi.
Mganda huyo alieleza, licha ya Etoile kuwa imara uwanjani, pia ni wajuzi wa mbinu chafu za nje ya uwanja katika kuwavuruga kisaikolojia wapinzani wao, wakitegemea zaidi sapoti ya mashabiki wao.
"Etoile ni moja ya timu kubwa barani Afrika ambazo licha ya uwezo wao kisoka, pia ni wajuzi wa mbinu chafu nje ya uwanja, jambo kubwa kwa Yanga ni wao wasijipange kukabiliana ndani pekee," alifafanua Mganda huyo.
Yanga imefuzu hatua hiyo baada ya kuifungisha virago FC Platinum ya Zimbabwe kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2, baada ya kushinda nyumbani 5-1 kabla ya kufungwa 1-0 ugenini, wakati Waarabu hao waliitoa Benfica ya Angola kwa kulazimisha sare ya 1-1 ugenini, hivyo kusonga mbele kwa mabao 2-1, kufuatia ushindi wa 1-0 katika mechi yao ya kwanza.
Okwi aliuzwa na Simba kwenda Etoile  Januari, 2013, kabla ya straika huyo kuingia kwenye mgogoro na uongozi wa klabu hiyo, akilalamikia kutolipwa malimbikizo ya mishahara yake ya miezi mitatu kabla ya kususa na kutimkia kwao Uganda.   
Okwi anasema kitu kipee ambacho kinaweza kuwasaidia Yanga ni kuhakikisha wanashinda mabao mengi katika Uwanja wa Taifa, kama walivyofanya kwa Platinum, kwani mbali na hapo wanaweza wakajikuta kwenye wakati mgumu ugenini.           
Mganda huyo alisema, Yanga wanapaswa kutofanya makosa kwenye mechi ya nyumbani kwa kuhakikisha wanashinda mabao mengi, kwani itakuwa moja ya silaha muhimu kwao kuelekea kwenye mchezo wa marudiano mjini Tunis.                             
Alifafanua kuwa, timu za Kiarabu zinapokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani zinatumia kila namna kuwafunga wapinzani wao, hivyo ana imani Yanga wanalijua hilo na fursa waliyopewa ya kuanzia Uwanja wa Taifa wanatakiwa waitumie vizuri kupata ushindi mnono.
"Nafikiri hata Yanga wanajua mbinu chafu za Waarabu, ukiwafunga bao moja au mawili uwanja wako wa nyumbani unaweza kuumia, kwani ni wajanja sana wanapokuwa kwao, wanatumia kila mbinu, hata hivyo, Yanga wana kikosi kizuri, wanaweza wakafika mbali," alisema.

No comments:

Post a Comment

ROSEMARY LUHAMO KUTOKA DODOMA AKABIDHIWA MAMILIONI YAKE NA UMOJA SPESHO

 Mshindi wa Shindano la Moja Spesho, Rosemary  Luhamo akiwa na furaha mara baada ya kukabidhiwa pesa zake kupitia Benki ya CRDB na Kampun...