Friday, April 3, 2015

Serikali ya Salim Amri BVRNA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
HATIMAYE Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesitisha kwa muda usiojulikana upigaji kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa uliokuwa umepangwa kufanyika Aprili 30.
NEC imesema imefikia uamuzi kutokana na kushindwa kukamilisha kwa wakati uliopangwa uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura.
Kutokana na hatua hiyo, sasa Katiba hiyo itapigiwa kura baada ya kukamilika uandikishaji katika daftari la kudumu la wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) Julai, mwaka huu.
Kuahirishwa kura ya maoni kumekuja baada ya malalamiko ya watu mbalimbali, wakiwamo wanasiasa na viongozi wa dini kuhusu kusuasua uandikishwaji wapigakura na muda wa kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa kuwa mfinyu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, alisema baada ya kukamilisha uandikishaji, NEC itakutana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa ajili ya kupanga siku ya kupiga kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Alisema NEC imetangaza kuahirishwa kwa upigaji kura kutokana na kusuasua kwa uandikishaji wa daftari hilo mkoani Njombe.
Jaji Lubuva alisema walitegemea uandikishaji wa daftari hilo ungemalizika  Aprili 12, mwaka huu  na upigaji kura za maoni ungefanyika Aprili 30, muda uliolalamikiwa na wadau wengi kuwa hautoshi.
Alisema katika kipindi hiki ambacho kura ya maoni imesitishwa, wananchi wana nafasi kubwa ya kuisoma Katiba hiyo ili waweze kujitokeza na kupiga kura.
“Kwavile kazi ya uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura ni la msingi na bado halijakamilika, tumelazimika kusogeza mbele ili kuhakikisha tunamalizia kazi hii ndipo tuanze kazi ya upigaji wa kura.
“Ili tuweze kurahisisha shughuli hiyo, Serikali imenunua jumla ya vifaa 248 kwa awamu ya pili na awamu ya tatu vifaa 1,600 ambavyo vitatumika mikoa iliyobaki kwa ajili ya kuendelea na zoezi hilo,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema hadi sasa NEC inategemea kumaliza kazi hiyo mkoani Njombe Aprili 18 ili waweze kuendelea na uandikishaji katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mtwara na Lindi kama ilivyopangwa.
Aliwataka wanasiasa kuwahamasisha wananchi kwenye mikoa tajwa wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari hilo ili waweze kuwa na haki ya kupiga kura.
“Tunawaomba wanasiasa washirikiane na NEC ili kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika mikoa iliyotajwa ili waweze kujiandikisha kwenye daftari hilo, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupiga kura kwenye chaguzi mbalimbali zijazo,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema zaidi ya Sh bilioni 11 zimetumika kununua vifaa vitakavyotumika kuendeshea shughuli hiyo, na kwamba Serikali haidaiwi kiasi chochote cha fedha.
“Tumetumia dola za Marekani milioni 72 kununua vifaa vya uandikishaji, tunaamini vifaa vilivyobaki vitakapofika nchini, kazi hii itakuwa rahisi.
“Taarifa kwamba Serikali inadaiwa si za  kweli, vifaa vyote vimelipiwa na kilichobaki vinafika kwa awamu.
 “Taarifa kuwa tulinyimwa vifaa kutoka Kenya na Nigeria hazina ukweli kwa sababu Tanzania na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika (SADC), zina utaratibu wa kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo,” alisema.
Alisema NEC iliomba vifaa hivyo kwa ajili ya kuvitumia kwenye uandikishaji, lakini walishindwa kuvipata kutokana na kutumika kwenye shughuli nyingine.

JOHN CHEYO
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, alisema uamuzi wa NEC kusogeza mbele upigaji kura ya maoni ni wa msingi kwa sababu muda uliopangwa awali ulikuwa hautoshi.
Cheyo alisema NEC ilipaswa kulitangaza suala hilo mapema ili kuondoa malalamiko yaliyojitokeza kwa wanasiasa na wananchi.
Alisema kutokana na hali hiyo, TCD itashirikiana na NEC kuhakikisha wanapunguza malalamiko.
“Tulijua muda uliopangwa awali na NEC hautoshi na tulijaribu kuwaambia wasogeze mbele lakini waligoma, matokeo yake wameamua kutangaza wenyewe.
“Kutokana na hatua hiyo, tunawaunga mkono kwa uamuzi huo kwa sababu umeondoa wingu lililotanda la kuwapo kwa sintofahamu ya kufanyika kwa kura ya maoni kama ilivyokuwa imepangwa,” alisema Cheyo.
Kabla ya kuahirishwa jana, wadau mbalimbali walishauri kusogezwa mbele ili uandikishaji ufanyike kwa weledi kutokana na kusuasua katika hatua za awali mkoani Njombe.

VURUGU BUNGENI
Mapema wiki hii, wabunge wa upinzani walisababisha kuvunjika kwa kikao cha Bunge mjini Dododoma baada ya kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atoe kauli juu ya mustakabali wa uandikishaji wapigakura na hatima ya kura ya maoni.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), ndio waliokuwa vinara wa mjadala huo.

JAJI BOMANI
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani, alionya endapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa italigawa taifa na kusababisha machafuko.
Aliishauri Serikali kusitisha kupiga kura ya maoni Aprili 30 na kuendelea na uboreshaji wa daftari la wapigakura.
Jaji Bomani pia aliitaka Serikali iachane na mfumo wa uandikishaji BVR kwa kuwa ilikurupuka bila ya kufanya maandalizi ya kutosha na fedha na vifaa havitoshi kuendeshea mpango huo.

JAJI WARIOBA
Januari 20, mwaka huu Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alionya muda wa upigaji kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa hautoshi.
Jaji Warioba alisema endapo sheria ingefuatwa kwa muda wa kutoa elimu na kila kitu, basi kura ingepigwa Julai, mwaka huu.
Alisema muda uliokuwa umepangwa ni mdogo, hasa ukizingatia mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu na wakati huo utakuwa muda wa kampeni.
Jaji Warioba alisema kuna mwingiliano unaoleta mkanganyiko katika mchakato wa kuboresha daftari la wapigakura na Sheria ya Kura ya Maoni.

KAULI YA JK
Septemba mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alisisitiza upigaji kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa utafanyika Aprili 30.
Alisema upigaji wa kura utafanyika baada ya elimu na kampeni juu ya kura hiyo kuanza rasmi Machi 30, mwaka huu na kuhitimishwa Aprili 29, kama sheria ya kura ya maoni inavyoelekeza, jambo ambalo halikutimia.

MAASKOFU
Nalo Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) liliendelea kushikilia msimamo wake wa kuwashinikiza waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Jukwaa hilo lilisema Katiba Inayopendekezwa imefika hapo ilipo kwa njia ya ubabe na kukosa uadilifu.


No comments:

Post a Comment

Waziri Dk Kigwangalla ataka wavamizi maeneo yaliyohifadhiwa kuondoka

Mwandishi wetu,Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amewataka wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi nchini,...