Wednesday, April 8, 2015

SIMBA YAANZA KUOTA UBINGWA LIGI KUU BARA

SIMBA imerejea kwenye mbio za ubingwa ambapo Kocha Mkuu wa timu hiyo Mserbia, Goran Kopunovic, amesema bado hajaikatia tamaa timu yake katika kinyang'anyiro hicho cha Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa sababu bado ana mechi tano mkononi.
Akizungumza mara baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar uliomalizika kwa timu yake kushinda mabao 2-1, Kopunovic alisema ana imani na timu yake inaweza kunyakua ubingwa.
Alisema katika mechi tano zilizobaki amepiga hesabu ya kuchukua ubingwa ndani ya dakika 450 katika mechi hizo.
Alisema kwa sasa wanashika nafasi ya tatu kutokana na pointi 35, ikitanguliwa na Azam FC yenye pointi 36 na Yanga ambao ndio vinara imefikisha pointi 40.
Kopunovic alisema pamoja na Yanga na Azam FC kujihakikisha ubingwa, lakini ataendelea na mipango yake ya kuiwezesha Simba kushinda mechi zilizosalia.
"Ninaamini lolote linaweza kutokea na kikosi changu kikafanya vizuri na kunyakua ubingwa, maana ligi hii ngumu, hakuna anayejiamini yupo vizuri hadi siku ya mwisho ya kumaliza msimu,"alisema kocha huyo.
Alisema tangu alipoanza kuifundisha timu hiyo imekuwa ikishinda na kufungwa, ingawa anaamini ubingwa unaweza kupatikana kwa timu nyingine ikifanya vibaya na wao kushinda.
Mechi ambazo Simba haijacheza anazopigia mahesabu kocha huyo ni pamoja na timu ya Mgambo FC, Mbeya City, Azam FC, Ndanda, na Ruvu JKT.
Kopunovic alisema kikosi chake kina vijana wengi ambao kila siku wanazidi kuwa katika kiwango cha juu, kitu ambacho kinawafanya wapambane kwa kila mchezo unaokuja.

No comments:

Post a Comment

MWENGE WA UHURU WAINGIA GAIRO NA KUZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA MILIONI MIASABA NA ZAIDI

 Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe akipokea Mwenge kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Morogoro Regina Chonjo mara ulipofika katika eneo la Ma...