BUTIKU AWATAKA WATANZANIA KUMCHAGUA MGOMBEA AMBAYE SIO MLA RUSHWA



MKURUGENZI  Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema katika muda huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ni vema watanzania watazamane nani ni nani na alifanya nini katika nchi hii.
Aliyasema hayo jana katika mkutano wa amani ulioandaliwa na taasisi hiyo na kufanyika katika ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam ambapo ulihudhuriwa na wananchi mbalimbali wakiongozwa na watoa mada ambao ni pamoja na Butiku, mjumbe wa bodi ya wadhamini wa taasisi hiyo, Getrude Mongela na Humphrey Polepole ambaye ni mjumbe.
Akitolea mfano wa kashfa iliyotokea kwenye serikali inayomaliza muda wake Butiku alisema watu wamekuwa wakijadili kuhusu uwajibikaji na kusema kuwa mtu fulani (hakumtaja jina) aliwajibika ili kumwokoa rais wake na serikali yake lakini bado watu hawafahamu ukweli.
Hata hivyo alisema “ubishi” huo ulitakiwa kuanza mapema na si wakati huu wa uchaguzi ambapo kila mtu anafanya jambo ili aweze kupata madaraka.
“Ubishi huu ulistahili kujitokeza mapema na si sasa hivi” alisema Butiku na kuongeza kuwa uwajibikaji umekuwa si wa viongozi bali ni wa taasisi suala ambalo alipingana nalo kwa kusema viongozi ndio wanaotakiwa kuwajibika.
“Sasa hivi watu wamekuwa wakizungumzia taasisi utasikia CCM (Chama cha Mapinduzi), Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo), NCCR Mageuzi, CUF na vingine lakini viongozi ndio wakuwajibika na hawana namana ya kukwepa ukweli huu.
Alisema viongozi wasikwepe wajibu wao kwasababu wao ndio hukabidhiwa dhamana ya kushughulikia umaskini, rushwa na ufisadi, viongozi wanaochaguliwa katika chaguzi zote zilizopita na huu unaokuja ndio ambao awali waliwahi kukabidhiwa dhamana ya uongozi na baadhi yao ndio leo wanaoomba nafasi za uongozi ili wasaidiane na wananchi kusimamia mambo yote ya wananchi.
“Kukubali kuwajibika ndio badiliko la msingi linalotakiwa sasa, kujaribu kukwepa uwajibikaji ama wa kiongozi binafsi au wa uongozi wa pamoja hasa katika ngazi ya taifa ndiyo dalilili ya uhakika ya kukataa mabadiliko. Falsafa ya uongozi inasema kuongoza ni kuonyesha njia na ili kuongoza ni lazima kuwa mbele na kuonyesha mfano na kiongozi mzuri ni yule anayeonyesha njia. Tujifunze kujua wananchi wanataka nini ili iwe rahisi kuwaongoza,” alisem Butiku.
Alisema mapungufu yaliyopita na yaliyopo katikka kuwahudumia watanzania yanatokana na mapungufu ya viongozi mmoja mmoja na katika umoja wao ambapo aliongeza kuwa uwajibikaji katika mapunguufu hayo ni wa viongozi na si wa chama au serikali.
Aidha aliwataka wananchi kutowaamini watu wanaoomba ridhaa ya kuongoza na wanafanya kila jitihada kukwepa wajibu wao binafsi au wa kundi lao la uongozi wa pamoja na kusema kuwa viongozi wa ain ahiyo hawafai.
Alisema viongozi wengi wamejenga tabia na hulka ya kuwahutubia wananchi badala ya kuwapatia utaalam, zana za kisasa za kilimo, kuwapa ardhi na kuwapimia, kuweka mipango ya kilimo cha umwagiliaji, ufagaji n auvuvi wa kisasa, kujenga viwanda vikubwa na vidogo na hasa vile vya kusindikia mazao ya wakulima ili kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo.
“Hili ni tatizo la uwajibikaji na kukubali ukweli wote kuhusu uwajibikaji. Viongozi waliopita na waliopo kwa miaka yote 54 ya uhuru wa nchi yetu ukiondoa vijana wa miaka 18 iliyopita walikuwepo,” alisema Butiku na kuhoji nani amlaumu nani ikiwa viongozi hao waliokuwepo na waliotoka ndani ya chama hicho wapo?
Aidha alisema hakuna wakumnyooshea kidole mwenzake kwasababu wote walishiriki katika uamuzi na utekelezaji na kwamba hakuna aliyewahi kuwajibika.
“Rushwa na ufisadi umekuwepo kwa miaka mingi kadhalika matatizo ya ardhi, elimu, afya, maji na ajira. Naniu aliwahi kujiuzulu wadhifa wake kwa kutoridhika na utekelezaji ndani ya chama au serikali?” alihoji Butiku.
MONGELA
Kwa upande wake Mongela alianza kutoa mada yake kwa kusema anawashangaa watu wanaosema hawawezi kuongozwa na wazee kama yeye lakini bado kuna wazee wanagombea nafasi ya urais.
Aidha alisisistiza kuwa mabadiliko lazima yaletwe na vijana na si wazee waliochoka midhili yake.
“Kama mnatafuta watu wakuongoza mabadiliko tafuteni vijana, wazee kama sisi tumeshachoka na muda wetu umekwisha,” alisema Mongela.
Akizungumzia suala la amani alisema Tanzania ilikuwa maskini na sasa ni maskini lakini amani bado ipo na kuhoji kama ni sahihi kuwa maskini ambao hawana amani.
“Tulikotoka tulikuwa masikini na tulikuwa na amani, tukaendelea na umasikini haujaisha lakini tupo na amani. Je mnataka hata amani tuipoteze?” alihoji Mongella na kutolea mfano taifa la Misri ambapo alisem awaliandamana na kumtoa kiongozi wao kwa fujo na sasa wanapinduana kwasababu walifanya mabadiliko bila kufikiria.
Kuhusu uchaguzi alisema ndiyo sehemu sahihi ya kufanya mabadiliko lakini akataatharisha kutofanya mabadiliko ya hasira na yasiyo na amani.
“Tunaenda katika uchaguzi na uchaguzi kuna uchungu na wasiwasi wa kutochaguliwa na watu wenye wasiwasi hawana amani na mtu wa namna hiyo hawezi kuwa na heshima. Lazima tuwe na utii wa sheria na kila mtu akitekeleza wajibu wake tutakuwa na uchaguzi wa amani,” alisema Mongella.
TASLIMA
Akichangia mjadala katika mdahalo huo Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Twaha Taslima, alitoa ujumbe wan chi za afrika mashariki na kusema wanaiombea amani Tanzania kwasababu ndiyo nchi iliyopakana nan chi zote za Afrika.
Aidha aliitaka Tume tya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki kwenye uchaguzi ujao kwani kinyume na kufanya hivyo amni iliyopo inaweza kutoweka japo hakun aanyetaka iwe hivyo.
Aidha aliishauri tume kuairisha uchaguzi pale ambapo itaona mambo hayaendi vizuri ili kuinusuru amani iliyopo.
“Nimekuja hapa kuleta ujumbe wa nchi za Afrika Mashariki, wanatuombea amani kwasababu tumezungukwa nan chi zote za Afrika Mashariki n atumekuwa na mchango mkubwa katika kurudisha amni kwenye nchi zao, tunaomba NEC isaidie kuhakikisha amani hii inakuwepo kwa kutenda haki na pale inapoona mambo hayaendi vizuri ni bora wakahairisha uchaguzi sisi tupo tayari,” alisema Taslima.
Kwa upande wake Humphrey Pole pole ambaye ni miongoni mwa washiriki wa taasisi hiyo, alisema kushindwa kuwajibika na kuwambana na ukweli mwisho wake uwendea  uongo na kudai kwamba kufanya hivyo heshima haitakuwapo.
“Ustahimilivu wetu haupo tena, siku hizi ukisema kitu ambacho mwingine hataki kusikiliza na matokeo yake utatolewa lugha chafu tabia ambayo hipo kwenye mitandao ya kijamii,”alisema Pole pole.
Alimnukuu Mwalimu Nyerere kwa kusema kwamba aliubiri siasa safi na uongozi bora na kutolea mfano wa baadhi ya wanachama wa vyama mbalimbali nchini kwa tabia ya kuzomea wengine barabarani na kudai kwamba kwa kufanya hivyo ni kuwanyima uhuru wa maamuzi huku viongozi wakikaa kimya bila ya kukemea jambo hilo.
Alisema hafurahishwi na anayoyaona leo katika maisha yake tabia ya viongozi kumungunya maneno huku wakiendelea kuhubili uongo kwa kudai kwamba haelewi utokea kwa lengo gani.
“Uongo ni adui yetu mkubwa, tulipokuwa tuki yasema hayo hapo awali wenzetu walitutukana tukiwa na mzee  wetu Butiku kuwaeleza kwamba tunamatatizo na kujaribu kuwa uma sikio juu ya hilo.
Alisema kwamba aliwahi kusema kwamba endapo CCM wangemchagua  fisadi angezunguka nchi nzima kupinga jambo hilo na kujaribu kutolea  muktadha wa Mwalimu Nyerere wa mwaka 1995 kwa kudai kwamba kwa wakati huo wananchi walichoka na rushwa na kuongezea kuwa uongozi si utajiri, ukabila, udini na kuwataka wapiga kura kuwatathimini wagombea wao.
“Tuwanze kwa kusema kijiko ni kijiko na bereshi si kijiko kikubwa, nikiona mtu  ndani ya CCM ameyazuia maoni ya wananchi niko lazi kupambana nae.
“Televisheni tatu wamesema Polepole nisiende  kwenye mijadala yao, leo hii kuna magazeti hazitoi makala zangu,”alisema na kuongezea kwamba kushindwa kwa vyama vya upinzani kutekeleza ajenda ya ufisadi ambayo ndio ajenda ya taifa na CCM kujitutumua kwa kufungua mahakama ya ufisadi ndio mabadiliko ambayo kwa upande wa vitabu vya dini tukio hilo linahashiria kuwa ni siku ya mwisho umewadia.
Pia alikemea kauli za kichochezi kwa vyama vyote ambapo alitolea mfano kauli ya ‘Bao la Mkono’ iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa CCM Nape Nnauye, kwenye mkutano wa kampeni Mtwara na ile ya UKAWA, Tanganyika Packers kuwa si nzuri.
“Baada ya kauli ile nilimkanya Nape lakini sikumuona kiongozi aliyejitokeza na kukemea ile kauli ya ikiwa kama uchaguzi utakuwa uhuru na haki CCM ijiandae kukabidhi Ikulu na kama wakikataa watatumia nguvu ya umma kwenda Ikulu
“Kwenda kudai Ikulu kwa nguvu ya umma kwenye sheria ni kitu gani kitatokea?,”alisema Polepole.
Akihitimisha mdahalo huo Butiku aliwatahadharisha vijana kuwaepuka wazee wanaowachonganisha badala ya kuwaeleza ukweli na kudai kuwa wazee wanaohama miji saa za mwisho wanamatatizo.
“Ukiona baba au babu anahangaika saa za mwisho na kuhama mji ujue huyo ana matatizo, wazee si watu wakuchonganisha bali ni watu wakupatanisha sasa wazee wamekuwa wachonganishi badala ya kuwaeleza ukweli,” alisema Butiku.
Alisema vijana wanaweza kuvaa mashati ya vyama lakini watafute ukweli na baada ya kujua ukweli wakafanye uamuzi kwa kuangalia dhamira zao.
“Vaeni mashati ya vyama lakini tafuteni ukweli wa mambo na mkishaujua ukweli mkafanye uamuzi kwa kuangalia dhamira zenu…mtu ukifanya uamuzi bila kuangalia dhamira yako kesho yake usimlaumu mtu,” alisema Butiku.

Post a Comment

Previous Post Next Post