MAMA MARIA NYERERE AFANYA IBADA YA KUMKUMBUKA MWALIMU NYERERE

MJANE wa Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,mama Maria Nyerere,ameshiriki misa ya shukrani katika kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha muasisi wa taifa la Tanzania katika Kanisa Katoriki Parokia ya Butiama huku suala amani kuelekea uchaguzi mkuu likizungumzwa na viongozi wa dini.

Akitoa neno wakati wa misa hiyo,Padri wa Jimbo la Musoma na Katibu wa Askofu wa Jimbo la Mara,William Bahitwa,alisema wakati watanzania wakiwa wanafanya kumbukumbu ya kifo cha mwalimu nyerere wanapaswa kutafakari na kuyafanyia kazi mazuri yote aliyoyafanya na kutanguliza amani hasa katika wakati huu wa uchaguzi.

Alisema Mwalimu Nyerere amelifanyia taifa la Tanzania mambo mengi ambayo yanapaswa kukumbukwa na kila mmoja na kudai iwapo yale yote ambayo amekuwa akipingana nayo na watu wakiamua kufanya watakuwa awamuenzi kwa dhati.

Bahitwa alisema suala la amani limekuwa likihubiliwa na Mwalimu Nyerere kwa kujua iwapo amani itakosekana na kuwa na mtafaraku mambo mengi yatashindwa kufanyika ikiwepo shughuli za kiuchumi katika kujiletea maendeleo kwenye familia na taifa.

Alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kumleta Mwalimu Nyerere katika taifa la Tanzania na ikiwa inahadhimishwa miaka 16 baada ya kifo chake bado ataendelea kukumbukwa na maneno yake bado yanapatikana kwenye vitabu na hotuba zake alizoziacha.

Kiongozi huyo wa dini alisema,Kanisa Katoriki kutokana na mchango wa mwalimu Nyerere katika masuala mbalimbali na imani aliyokuwa nayo,limeamua kuanzisha mchakato wa kumtangaza mtakatifu na kwa sasa tayari ameshatangazwa kama mtumishi wa Mungu Mwalmu Julius Kambarage Nyerere.

“Kanisa limeanza mchakato wa kumtangaza kama mtakatifu,na mchakato una hatua ambazo unapitia na kwa sasa mwalimu anatambulika kama mtumishi wa Mungu na michakato inaendelea ili aitwe mtakatifu.

“Naomba tunapoenda kwenye uchaguzi tuzingatie suala la amani na kila mwana siasa awe tayari kukubaliana na matokeo katika uchaguzi kwani wakati kama huu katika mataifa mengine ndio tumekuwa tukishuhudia uvunjifu wa amani.”alisema Padri Bahitwa.

Akizungumza na Mtanzania kuelekea uchaguzi mkuu,kiongozi wa ukoo wa Mwalimu Nyerere,Chief Japhet Wanzagi,alisema baba wa taifa alikuwa mtu ambaye alikuwa akisisitiza suala la amani wakati wote na kuwaomba watanzania wakati wakielekea kwenye uchaguzi kulipa kipaumbele suala hilo.

Alisema wito wake kwa watanzania ni kujitokeza kupiga kura kwa wagombea wanao wahitaji baada ya kusikiliza mikutano ya kampeni na hakuna sababu ya kufanya matendo ambayo yanaweza kutoa viashilio vya uvunjifu wa amani.

Post a Comment

Previous Post Next Post