WAGOMBEA wa vyama
tofauti waliokuwa wanagombea ubunge Mbagala wameungana kupinga matokeo
yaliyobandikwa katika Kituo cha Shule ya Msingi Majimatitu ambayo yamempa
ushindi mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Issa Mangungu.
Wagombea hao wanaotoka katika chama Cha Wananchi (CUF), ACT-
Wazalendo, AFP, NCCR-Mageuzi, wanayapinga matokeo hayo wakidai si ya halali.
Matokeo yaliyobandikwa katika kituo hicho na kugongwa muhuri
wa Mkurugenzi yanaonyesha mgombea wa CCM, Mangungu ameshinda kwa kura 87,249
akifuatiwa na wa CUF , Kondo Bungo aliyepata kura 77,043.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za
chama hicho, Temeke Dar es Salaam, Bungo
alisema matokeo hayo yamepikwa na ni kinyume na sheria.
"Tunayakataa kwa sababu katika.makubalino yetu.juzi
na.mkurugenzi wa Temeke, Photidas Kagimbo, tulikubaliana uchaguzi umeharibika
na ilikuwa jana atoe tamko lakini hata uhakiki bado haujafanyika.
“Juzi tulibaini kasoro nyingi ikiwamo kasoro ambayo Kata ya
Kijichi ilionyesha nimepata kata moja wakati karatasi za wakala zinaonyesha
nimepata kura 78 na kuna kata ilikuwa na
vituo 94 lakini walileta matokeo ya vituo 80 na mkurugenzi alikiri kasoro
hizo...tunashangaa jana wamebandika na yana muhuri wa mkurugenzi,” alisema
Kondo.
Alisema wameamua kufanya mazungumzo na wanasheria wao kuweza kutoa uamuzi wa pamoja kuhusiana na
matokeo hayo.
Kondo alisema anachoweza kusema ni kuwa wananchi wa Mbagala
wafahamu haki yao imepokwa na wao binafsi kila mmoja atajua jinsi ya kudai haki
yake.
“Wananchi watafakari kila.mmoja dhuluma hii na kila.mtu
atajua hatua za kuchukua,” alisema Kondo.
Vyama vingine vilivyogombea ni TADEA
kilichopata kura 607, AFP 739, CHAUSTA 362, Demokrasia Makini 264, NRA 238
na NCCR Mageuzi 2,156.
Waandishi wa gazeti hili walitembelea kituo hicho cha shule ya Majimatitu na kukuta
ulinzi ukiwa umeimarishwa na baadhi ya maduka yakiwa yamefunguliwa.
MTANZANIA ilifanya jitihada za kumtafuta mkurugenzi Magimbo
kupata ufafanuzi zaidi wa matokeo hayo lakini simu yake ilikuwa haipatikani na pia hakuwapo
ofisini.