Friday, October 23, 2015

Askofu: Wananchi kuhamasishwa kulinda kura ni kuchochea vuruguASKOFU wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphor Mkude, amesema kitendo cha wananchi kuhamasishwa  kulinda kura siku ya uchaguzi ni dalili za uchochezi wa vurugu na uvunjifu wa amani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema kumekuwa na hofu kwa Watanzania juu  ya  upotevu  wa amani  katika  kipindi  hiki cha  uchaguzi.

Alisema kuwa ni  vyema  vyama   vya siasa   vikaiga  mfumo wa timu za mpira  wa miguu  kama  Simba na Yanga  kukubali matokeo  kwa yeyote anayeshinda.

Askofu Mkude alisema  kuwa  timu  hizo hushindana mara nyingi  na yupo  anayekubali  kushindwa  bila  ya  kushika  silaha au kufanya  vurugu.

“Nchi haitakuwa na amani katika  uchaguzi mkuu  utakaofanyika Jumapili wiki hii kama sheria na haki hazitafuatwa,” alisema. 

Alisema kumekuwa  na kauli za uchochezi kutoka  kwa wanasiasa wa  vyama mbalimbali vinavyoshiriki uchaguzi ambazo zinakuwa na tafsiri tofauti kwa  mashabiki na wafuasi wao na  hivyo kusababisha  kuhamasisha uvunjifu wa amani katika jamii.

“Ukiangalia kwa upande wa wanyama kiongozi wao hupatikana kwa mabavu lakini kwa upande wetu sisi binadamu kiongozi hupatikana kwa demokrasia  na si kutumia  nguvu yoyote,” alisema.

Hata hivyo, Askofu Mkude ameonesha kuchukizwa na kauli zinazotolewa  na  wanasiasa za kudai  chama kilichopo madarakani  hakijafanya lolote  kwa kipindi cha miaka 50.

Alisema si kweli kwamba chama hakijafanya lolote  kwa kuwa Tanzania ya mwaka  1960 na  sasa  kuna  tofauti  kubwa.

“Kuna hii kauli ya wanasiasa  kudai kuwa  watashinda  uchaguzi kwa namna yoyote hata kwa  bao la mkono, ni dalili tosha ya kuchochea  vurugu na hakuna  mtu yeyote  aliyetolea  ufafanuzi  kuhusu kauli hiyo,” alisema.

RAIS KIKWETE AMESEMA KAMWE AWEZI KUIINGILIA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NECRais Jakaya Kikwete amesema hawaiingilii Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) bali wanachofanya ni kuiwezesha kupata fedha ili itimize majukumu yake.

Kauli hiyo aliitoa Kisiwani Pemba jana wakati wa kufunga kampeni za CCM zilizofanyika katika Uwanja wa Gombani ya Kale uliopo Mkoa wa Kusini Pemba.

“Matayarisho ya uchaguzi ni kazi ya NEC hatuwaingilii, jukumu letu ni kuwawezesha kupata fedha na tumefanya hivyo ndiyo maana mmeona vifaa vimesambazwa,” alisema Kikwete.
Alisema uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu na kuonya kuwa atakayejaribu kufanya vurugu atachukuliwa hatua.
Naye mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema endapo atachaguliwa tena yale yote aliyoyaahidi yatatekelezwa.
Alisema karafuu haitabinafsishwa bali itaendelea kuboreshwa na kama bei itaongezeka katika soko la dunia na yeye ataiongeza hadi ifike Sh 20,000 kwa kilo badala ya Sh 14,000 ya sasa

SERIKALI YASHINDA KESI YA MITA 200

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson (kushoto), akipongezana na mawakili wenzake baada ya utetezi wa Serikali kushinda katika shauri la tafsiri kisheria kuhusu wananchi kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura baada ya kupiga kura lililopelekwa na mwananchi aitwaye, Amy Kibatala na kukataza mikusanyiko hiyo.

LOWASA, MAGUFULI WAISHI KWA MATUAMAINI KUELEKEA OCTOBA 25
MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema ana uhakika wa kushinda kwa asilimia 80, na kwamba atakuwa rais wa mabadiliko na si maneno.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Kigoda CCM, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
“Kuna watu wanasema nitapita kwa asilimia 50 au 60 hivi, lakini kwa hali niliyoiona vijijini na mijini, naona nitapata asilimia 80. Naomba mfanye kweli nipate hizo asilimia kwa sababu nitakuwa rais, si rais wa maneno, nitakuwa rais wa mabadiliko.
“Nimeongoza haya mabadiliko kwa heshima, nataka niongoze taifa hili kwa heshima pia, ili wajue tunaweza kuwa bora kuliko mataifa mengi duniani na hatimaye tuachane na umasikini ambao mimi nauchukia,” alisema Lowassa.
Ili kuhalalisha ushindi wake huo, aliwataka wafuasi wake kumpigia kura kwa wingi ili hata kama baadhi zitaibwa, aweze kushinda.
“Tumechoka na miaka 54 ya CCM, Tanzania bila CCM inawezekana, tuonyeshe kazi,” alisema Lowassa.
Kuhusu Jeshi la Polisi, alisema kwa sasa wanawakamata ovyo vijana wanaoonyesha mapenzi kwa Chadema, jambo ambalo alisema linaweza kusababisha vurugu nchini.
“Nimeona jana Tanga na maeneo mengine kuna tabia imeanza ya kukamata vijana wa Chadema. Nawaambia Serikali waache, wanachochea fujo, vijana hawa ukiwachokoza utaanzisha fujo.
“Sisi tuna hakika ya kushinda asubuhi kweupe, kwahiyo, hatuna sababu ya kufanya fujo, na waache vitisho vya aina yoyote,” alitahadharisha Lowassa.

SUMAYE
Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, akizungumzia suala la polisi, alisema vijana wanaobeba bendera za Chadema wakionekana wakiwa wamefuatana hata kama ni watatu, wanakamatwa, lakini wanaobeba bendera za CCM, hata wakiwa wengi kiasi gani hawaguswi.
 “CCM hata wakiwa 50 hawakamatwi, waendelee tu kuwapiga, lakini kwenye kura watapiga bomu la machozi?
“Jumapili ndiyo siku ya sisi kuamua kujikomboa na matatizo ama kuendelea nayo maisha yetu yote, hii ndiyo nafasi Mungu aliyotupa, tuitumie vizuri,” alisema Sumaye.
Msafara wa Lowassa ulipokuwa Kilindi, mkoani Tanga, Meneja Kampeni wa Chadema, John Mrema, aliwataka wanawake wasimchague mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kwa sababu hajui matatizo yao.
Alimshangaa Dk. Magufuli kutomtumia mkewe majukwaani kama ambavyo mke wa Lowassa, Regina Lowassa anavyopanda majukwaani kumwombea kura mumewe,” alisema Mrema.

MSAFARA WASIMAMISHWA
Awali wakati magari ya msafara wa Lowassa yakitoka Tanga Mjini kuelekea Handeni, yalisimamishwa na mamia ya wananchi waliokuwa wamesimama eneo la Muheza.
Wananchi hao walisimamisha magari hayo wakidhani yumo Lowassa ambaye alikuwa ametangulia Handeni kwa kutumia helkopta.
Wakati Lowassa akitoka Tanga Mjini kwenye mkutano wa kampeni uliovunjika hivi karibuni kutokana na uwanja kuzidiwa na watu, alifanya mikutano ya kampeni kwenye eneo hilo na kumnadi mgombea ubunge na madiwani.
Lowassa anatarajia kufanya mikutano ya kampeni mkoani Morogoro kabla hajaingia Mkoa wa Pwani akielekea jijini Dar es Salaam atakakofungia kampeni Oktoba 24 katika Viwanja vya Jangwani.
 Mwisho.


Dk. Magufuli asema yeye ndiye mshindi

 NA BAKARI KIMWANGA, CHALINZE
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema anajua yeye ndiye rais wa awamu ya tano na Watanzania wameshamhakikishia watamchagua keshokutwa wakati wa kupiga kura.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, anajua Watanzania wamechoshwa na ahadi za uongo, na kwamba sasa wanahitaji ahadi za vitendo.
Dk. Magufuli aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika Chalinze, Mkoa wa Pwani.
 “Watu wamechoshwa na ahadi za uongo na wanahitaji matumaini mapya, na mimi nasema nichagueni, sitawaangusha na sadaka yangu kwenu ni kufanya kazi kwani kwangu ni kazi tu.
“Nataka nifanye kazi, sitawaangusha kwani nimefanya kazi kwa miaka 20 kwa niaba yenu Watanzania. Nimewahi kulala kwenye madaraja na kila mmoja anajua uchapakazi wangu.
“Nitafanya kazi kwa uadilifu kwa sababu nina hofu ya Mungu na wakati wote nitamuomba ili nisiwaangushe,” alisema Dk. Magufuli.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli alisema anashangazwa na maneno yaliyotolewa na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Amesema kwamba kauli ya Lowassa ya kuhoji fedha za ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kama zilitolewa kwa mkataba haiwezi kukubalika kwa kuwa anapanga kuufuta mkataba huo pindi atakapoingia madarakani.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, kauli ya Lowassa inalenga kuleta chuki kati ya wananchi wa Bagamoyo na Tanga, na kwamba inawezekana aliitoa kwa kuwa anajua Rais Jakaya Kikwete ni mzaliwa wa Bagamoyo.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Magufuli hakutaja jina la Lowassa, lakini maelezo yake yalimlenga mgombea urais huyo wa Chadema kwa kuwa alipokuwa jijini Tanga juzi, alisema ataangalia mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo baada ya kuingia madarakani ili fedha zilizotengwa, zihamishiwe katika ujenzi wa Bandari ya Tanga.
“Mimi sitoki Bagamoyo ila nasema hapa iwe usiku au mchana, Bandari ya Bagamoyo itajengwa kwani inajengwa na watu binafsi kupitia mpango wa pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
“Tutajenga Bandari Mtwara, Tanga na Mwanza na fedha zipo. Hata fedha za Bandari ya Tanga nazo zipo na tutaijenga pia. Msikubali kuchonganishwa na watu kwa maneno ya ubaguzi, kwani wanayasema haya kwa sababu Rais Jakaya Kikwete anatoka Bagamoyo.
“Toeni hoja kuwaeleza watu wa Tanga utawasaidia vipi kuliko kutoa uchonganishi wa ajabu, na adhabu yao kwa Watanzania ni kuwanyima kura kwani pamoja na kujengwa kwa Bandari ya Bagamoyo katika eneo la Mbegani, pia eneo maalumu la kiuchumi la EPZ litaendelezwa,” alisema Dk. Magufuli.
Akizungumzia miundombinu, Dk. Magufuli, alisema Serikali itajenga barabara kubwa ya kisasa ya njia sita kutoka Chalinze hadi jijini Dar es Salaam.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo utakuwa na barabara za juu saba zitakazojengwa kwenye maeneo ya Chalinze, Mlandizi hadi jijini Dar es Salaam.
“Tutajenga ‘Fly over’ saba kuanzia hapa Chalinze hadi Dar es Salaam na tayari fedha za mradi huu zimeshatengwa kiasi cha shilingi trilioni 2.3.
“Kutokana na hali hii, sasa maendeleo yanakuja kwa kasi na ninawaomba sana msiuze ardhi yenu kwani Chalinze na Kibaha mpya yenye maendeleo inakuja kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 pamoja na ile ya matumizi bora ya ardhi.
“Wasije wajanja wakawarubuni kwa kuwakatia maeneo yenu kwa shilingi 50,000 kisha wanakuwa na maeneo makubwa na watakapokuja wawekezaji, wanayauza kwa fedha nyingi,” alisema Dk. Magufuli.
Kuhusu sekta ya elimu, alisema kazi kubwa iliyofanywa na Rais Kikwete ni kujenga madarasa ya kutosha, na kwamba atakapoingia madarakani, ataboresha elimu na masilahi ya walimu.
“Kazi kubwa imefanywa na awamu ya nne na mimi ikiwa mtanichagua Jumapili kwa kura nyingi na kuwa rais wenu, nitaboresha elimu baada ya kujenga shule za kata,” alisema.

Mwisho

TAMASHA LA WASANII WILAYA YA TEMEKE KUPAMBWA NA PATRICIA HILLARY

CHAMA Cha waigizaji Mkoa Temeke  kimeamua kukusanya  waigizaji wote waishio Dar es salaam wilaya ya temeke. Akizungumza n...