Kubenea kutinga na Escrow Bungeni



MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amesema anatarajia kufufua hoja ya kujadiliwa upya kwa ripoti ya fedha zilizokwapuliwa za Tegeta Escrow zaidi ya Sh bilioni 200.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, alisema sababu za kutaka mjadala huo kurejeshwa ni kutaka kujua iwapo fedha hizo ni za umma au ni mali ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Sababu nyingine aliyoitaja Kubenea ni kutaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa sakata hilo, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Mapendekezo ya Taarifa ya PAC
Iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, iliwasilisha bungeni mapendezo zaidi ya 10 likiwemo azimio namba moja la kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kumkamata Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP) Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ukwepaji kodi.
Kamati inaelekeza Serikali kutumia sheria za nchi, ikiwamo sheria ya Proceeds of Crime Act, kuhakikisha kuwa Singh Sethi anarejesha fedha zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG iliyothibitishwa na TAKUKURU, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu binafsi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe, alisema kamati yake ilijiridhisha kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu (BoT).
Historia ya Escrow
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya IPTL.
Fedha hizo zilizua mjadala mkubwa bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka msimamo wa Serikali kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, akisema kuwa fedha hizo hazikuwa za umma na hivyo kuzidisha mjadala.

Post a Comment

Previous Post Next Post