ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Kardinali
Polycarp Pengo amejitokeza kwa mara ya kwanza na kuzungumza juu hali yake.
kardinali Pengo alilazwa JCKI Desemba 31, mwaka jana ambapo
aliushukuru uongozi wa hosptali hiyo kwa matibabu aliyoyapata na kwamba sasa
anaendelea vizuri na anaweza kutoka wakati wowote kuanzia sasa.
“Siku hizi nimepoteza maneno siwezi kuzungumza sana… lakini
napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wahudumu walionisaidia tangu
nilipofikishwa hapa.
“Kwangu imekuwa nafasi nzuri kuifahamu Hospitali ya
Muhimbili, nawaomba waandishi wa habari muwe mnaandika pia na mazuri yaliyoko
hapa maana mimi ni mmoja wa watu niliokuwa naamini kwamba hakuna huduma nzuri,
semeni ukweli,” alisema.
Kardinali Pengo alitoa zawadi ya kadi kwa baadhi ya wakuu
wa vitengo vya hospitali hiyo ikiwamo Idara ya Dharura (Emergence), JCKI na
Idara ya matumbo kama sehemu ya shukurani yake.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa JCKI, Profesa Mohamed Janabi
alisema hali ya Kardinali Pengo inaridhisha kwa sasa na kwamba atapatiwa ruhusa
mwishoni mwa wiki hii.
“Hapa tunashughulikia maradhi ya moyo, Askofu alikuwa
akisumbuliwa na tatizo la moyo na wamelishughulikia hivyo ataruhusiwa mwishoni
mwa wiki hii.
MWISHO