Tuesday, February 23, 2016

ASANTENI KWA KUJAASANTENI kwa kuja. Ndio ujumbe rahisi na wa dharau ambao klabu ya Yanga imeutuma kwa wapinzani wao wakubwa, Simba, siku chache baada ya kuwafunga mabao 2-0 katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam mwisho wa wiki iliyopita.
Picha kamili liko hivi: Matokeo ya juzi yalimaanisha kuwa Yanga imeshinda mechi zake zote mbili dhidi ya Simba msimu huu na katika mapambano yote hayo walishinda kwa mabao 2-0, kitu ambacho tayari kimeanza kuwapa jeuri na kujiona wao ni levo nyingine.
Na hiki ndicho kimewafanya sasa wadiriki kusema kuwa Simba si levo yao tena na watabaki kuwa watani wao wa jadi tu, lakini si wapinzani wao wakubwa kwa sababu viwango vyao ni tofauti kama mbingu na ardhi.
Yanga, ambayo ushindi wake ulitokana na mabao ya mastraika wake wa kimataifa, Donald Ngoma (Zimbabwe) na Amis Tambwe (Burundi), wametoa kauli hizo za dharau dhidi ya Simba kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano, Jerry Muro.
Muro aliliambia BINGWA kuwa wameamua kuvunja rasmi upinzani wao dhidi ya Simba kwa sababu Wekundu hao wa Msimbazi si saizi yao tena na sasa hivi wanahitaji timu nyingine ambayo itawapa upinzani wa kweli ambao Simba wameshindwa kuutoa kwao.
“Tunatangaza rasmi kuvunja upinzani wetu na Simba kutokana na ukweli kuwa sasa hivi hawa jamaa si saizi yetu,” alisema Muro. “Sisi wa kimataifa na saizi yetu lazima wawe wa kimataifa pia, hawa Simba hawana ladha tena, watabaki kuwa watani wetu tu, lakini kamwe hawawezi kuwa wapinzani au washindani wetu kwa sababu si levo yetu.”
Muro aliendelea kutamba kuwa kitendo cha Yanga kuipiga Simba kwenye mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kimethibitisha kuwa miamba hiyo ya Msimbazi si saizi yao tena.
“Kilichobaki sasa hivi tukutane nao kwenye mabonanza ya mchangani, lakini kama kwenye ligi tumemalizana nao au kama kutakuwa na mzunguko wa tatu tupo tayari pia kucheza nao, nasisitiza tena Simba si saizi yetu,” alitamba Muro.
@@@@@

No comments:

Post a Comment

ROSEMARY LUHAMO KUTOKA DODOMA AKABIDHIWA MAMILIONI YAKE NA UMOJA SPESHO

 Mshindi wa Shindano la Moja Spesho, Rosemary  Luhamo akiwa na furaha mara baada ya kukabidhiwa pesa zake kupitia Benki ya CRDB na Kampun...