Saturday, February 6, 2016

DK SLAA KUFUNGA NDOA NCHINI CANADA NA JOSEPHINE MSHUMBUSHI


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, anatarajia kubariki ndoa na mkewe Josephine Mshumbusi siku chache zijazo.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa watu walio karibu na familia ya Dk. Slaa, zimedai kuwa kasisi huyo wa zamani na mkewe Josephine, watabariki ndoa yao nchini Canada kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.
Ingawa taarifa hizo hazikuthibitisha siku ambayo harusi hiyo itafanyika, zimeeleza kuwa maandalizi yako katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuhudhuriwa na watu wachache.
“Dk. Slaa na mkewe Josephine Mshumbusi wapo katika maandalizi ya kubariki ndoa yao huko nchini Canada, taarifa nilizonazo harusi yao wataifunga kabla ya Sikukuu ya Pasaka,” alisema mmoja wa watu walio karibu na familia hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi.
Alipoulizwa Josephine kupitia simu yake ya kiganjani, alithibitisha kuwa taarifa hizo ni za kweli na kwamba wapo katika hatua za mwisho za maandalizi ya tukio hilo.
MTANZANIA Jumapili lilipomuuliza siku ambayo ndoa hiyo inatajiwa kufungwa alicheka kisha akasema atatoa taarifa rasmi siku moja kabla ya harusi.
“Ha ha ha ha… wachawi wengi, okay (sawa) nitakuambia ikiwa imebaki siku moja kabla ya shughuli,” alisema Josephine.
Wawili hao wanaishi pamoja kwa takribani miaka sita sasa na waliwahi kuanza maandalizi ya kufunga ndoa wakiwa hapa nchini, lakini walikwama baada ya mke wa ndoa wa Dk. Slaa, Rose Kamili kupeleka pingamizi mahakamani.
Baada ya pingamizi hilo, wawili hao waliendelea kuishi pamoja hadi hivi karibuni wakiwa uhamishoni Canada zilizopatikana taarifa za kufunga ndoa yao hiyo.
Wakati hayo yakijiri, taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili hivi karibuni zilieleza kuwa Dk. Slaa na Josephine waliondoka nchini mwaka jana na kukimbilia nchini Canada ambao waliomba hifadhi ya kisiasa.
Taarifa hiyo ambayo ilichapwa na gazeti hili toleo la Jumamosi ya wiki iliyopita, ilieleza kuwa Dk. Slaa aliomba hifadhi ya kisiasa nchini Canada kwa sababu ya kuhofia usalama wa maisha yake hapa nchini, baada ya kuanza kutishwa na watu ambao hawajapata kujulikana kutokana na uamuzi wake wa kujiondoa Chadema wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu.
Katikati ya hayo, zipo taarifa za kupigwa mnada kwa nyumba yake iliyopo Mbweni jijini Dar es Salaam baada ya mkewe Josephine anayedaiwa kuitumia kuchukua mkopo benki moja iliyopo maeneo ya Mwenge, kushindwa kuurejesha.
Josephine mwenyewe amekuwa akikanusha madai hayo na mumewe Dk. Slaa ambaye alifanya mahojiano na gazeti hili mapema wiki hii alimuunga mkono kwa kueleza pamoja na mambo mengine kuwa ni umbea.
Katika mahojino hayo, Dk. Slaa alieleza kuwa yeye na mkewe Josephine tangu walipoanza kuishi pamoja hawajapata kuchukua mkopo benki na tangu alipoacha kuwa mbunge hajawahi kuchukua hata senti moja benki ukiachilia mbali propaganda ya kuchukua mkopo wa sh milioni 300.

No comments:

Post a Comment

MWENGE WA UHURU WAINGIA GAIRO NA KUZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA MILIONI MIASABA NA ZAIDI

 Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe akipokea Mwenge kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Morogoro Regina Chonjo mara ulipofika katika eneo la Ma...