Na Benedict John-MAELEZO-Dar es salaam.
………………………………………………..
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simiyu Trasias Kagenzi amekanusha
madai yaliyoandikwa na baadhi ya vyombo vya Habari kuhusiana na taarifa
za kufanyika kwa mgomo unaotarajiwa kufanywa na baadhi ya Madaktari na
Wauguzi katika Hospitali mkoani Simiyu na kusema habari hizo sio za
kweli.
Kauli
hiyo ameitoa leo katika mahoajiano na Mwandishi wa Habari hii juu ya
kuwepo kwa mgomo huo ambapo alifafanua kuwa, taarifa hiyo haina ukweli
wowote kwani siku ya tarehe 02 Februari mwaka huu, alikuwa na kikao na
watumishi wote wa Hospitali hiyo ambapo kati ya mambo walioyajadili ni
stahili na hali ya kazi hospitalini hapo.
”Hapa
wilayani kwetu kuna baadhi ya waandishi ambao hawazingatii maadili ya
kazi zao hasa kwa kuandika habari zisizo na ukweli, nimeshangaa kusikia
taarifa hii kwasababu ukweli ni kwamba mimi nilikaa na watumishi wote
jana wakiwemo madaktari, wauguzi na madereva na moja ya mambo
tuliyojadili ni pamoja na mishahara yao na posho zao, na tulimaliza
kikao chetu kwa amani kabisa, sasa waandishi kama hawa tunawaita
makanjanja maana haina ukweli wowote”, alisema Kagenzi.
Aliongeza
kuwa, kitendo walichokifanya baadhi ya waandishi hao kuandika habari
hiyo sio jambo la busara kwani linaleta mkanganyiko na chuki baina ya
watumishi na viongozi wao na hata kwa serikali yao na amelaani jinsi
waandishi hao wanavyotumia kalamu zao vibaya kwa kupotosha umma wa
watanzania
”Inasikitisha
kwa kweli mtu anakurupuka bila kuwasiliana na Utendaji Mkuu wa
Hospitali na kuanza kuanza kukutana na madaktari anaowajua na kuanza
kuandika taarifa kama hizi na kuzirusha katika vyombo vya habari”,
alisisitiza Kagenzi.
Mkurugenzi
huyo amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi zao ili
waweze kuandika habari ambazo zinatoa picha halisi badala ya
kuwaogopesha wananchi na hivyo kushindwa kwenda kupata huduma.
Kwa
upande wake Afisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bi. Stella Kalinga
alieleza kuwa baada ya kufuatailia taarifa aligundua kuwa siyo za kweli
kwani hakuna dalili yoyote ya mgomo kwa watumishi hao wa afya na wako
kazini wakiendelea na majukumu yao kama kawaida.