Friday, February 19, 2016

MAGUFULI AMUAGIZA NAPE KUICHUKUA COSOTA


Akizungumzia kilio cha wasanii juu ya Chama cha Haki Miliki Tanzania (Cosota), Rais Dk. Magufuli, alisema naye anashangazwa na hatua ya chama hicho kuwa chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, hali ya kuwa wahusika wanasimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuhakikisha anaandika barua kwenda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili achukue hatua zinazohitajika.
Rais alitoa uamuzi huo, baada ya msanii wa kizazi kipya Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, kuwasilisha kilio dhidi ya haki miliki  kuhusu Cosota.
Alisema kutokana na Cosota kuwa chini ya wizara nyingine, wasanii bado wananyonywa haki zao za ubunifu huku wanaofaidika ni watu wengine, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikishindwa kukusanya kodi.
Kutokana na kilio hicho, Rais Dk. Magufuli, aliitaka TRA kuhakikisha wanakusanya mapato kwa kufanya msako kama wanavyofanya kwenye makontena yaliyofichwa.
“Hili la Cosota nimelisikia na nilipokuwa kwenye kampeni, nilisema kwangu ni kazi tu, sasa Waziri Nape kesho (leo), wasilisha barua kwa Waziri Mkuu afadhali naye yupo hapa, kama ni jambo ambalo halihitaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri au kwenda bungeni kwa ajili ya kubadili sheria nitaagiza mara moja Cosota, ikasokotee kwenye wizara yako.
“Huwezi kusimamia watu ambao ndio wahusika ukiwa wizara nyingine na hili tutachukua hatua za haraka,” alisema.
Alisema anataka kuona wasanii wa Tanzania  wananufaika na kazi zao pamoja na ubunifu wao ambao vipaji wamepewa na Mwenyezi Mungu.
“Haiwezekani mtu ambaye hahusiki akafaidika na kazi yako, nitoe wito kwa TRA kama wanaweza kushika makontena yaliyofichwa pia wafanye hivyo kwa kazi za wasanii. Kikubwa niwahakikishie tena ndugu zangu tulianza wote na tutamaliza wote.
“Taifa letu tukiwa wamoja tutasonga mbele  tusitegemee kuna mjomba wala shangazi atakayekuja kutusaidia, Watanzania wanahitaji Serikali iliyo imara,” alisema Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

ROSEMARY LUHAMO KUTOKA DODOMA AKABIDHIWA MAMILIONI YAKE NA UMOJA SPESHO

 Mshindi wa Shindano la Moja Spesho, Rosemary  Luhamo akiwa na furaha mara baada ya kukabidhiwa pesa zake kupitia Benki ya CRDB na Kampun...