KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja, ameamua kuwafungia kazi
wachezaji wake wote `waliopangwa` katika mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara na kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa watani wao
wa jadi, Yanga.
Katika mchezo huo, Simba walianza kwa kasi, huku
viungo wao wakigongeana vyema kabla ya kusambaratika baada ya kutolewa kwa kadi
nyekundu beki wa kati wa timu hiyo, Abdi Banda, baada ya kumfanyia madhambi
straika wa Yanga, Donald Ngoma.
Hali hiyo ilimlazimu Mayanja kumshusha kiungo Justice
Majabvi kusaidiana na Jjuuko Murushid, hivyo kupunguza kasi katika ya safu yake
ya viungo.
Mayanja ameliambia JIJILETU BLOG jijini jana, kwamba
atakutana leo na wachezaji wake katika mazoezi, kikubwa ni kuwaweka sawa
kisaikolojia pamoja na kufanyia kazi mapungufu na makosa yaliyojitokeza katika
mchezo uliopita.
Alisema ameshangazwa na kiwango cha chini
kilichoonyeshwa na wachezaji wake, hivyo anahitaji umakini wa hali ya juu
katika kuhakikisha katika mazoezi yao ya leo anaangalia kila idara na kuwapiga
msasa wachezaji wake.
“Sijaelewa kwanini
vijana wangu wamecheza chini ya kiwango bila ya kutarajia, lakini kwa kupoteza
mechi hiyo hakumaanishi kuwa ndio tumekata tamaa katika mbio za ubingwa kwa
kikosi changu,” alisema.
Mayanja alisema katika mazoezi yao atafanyia kazi
safu yake ya ulinzi, viungo, hasa katika sekta muhimu ya ushambuliaji, ambayo
haikuonyesha uhai wala madhara yoyote kwa wapinzani wao.
“Bado nina imani kubwa na vijana wangu, sasa jambo
lililobaki ni kukaa na vijana nizungumze nao na kuangalia wapi natakiwa tufanyie
kazi, pia suala la ubingwa naona bado sijapoteza matumaini kulingana na
jinsi tulivyopishana pointi,” alisema.
Mayanja alisema katika hatua hiyo ana imani bado
ndoto zake za kuibuka na ubingwa zinaendelea, akiamini vijana wake watafanya vizuri
katika michezo iliyobakia ya mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.