Friday, February 19, 2016

TAFEYOCO LAMTAKA MAGUFULI KUJITAZAMA KWA JICHO LA TATU

 
SHIRIKA linalojishughulisha na masuala ya Wanawake na Vijana katika kutatua changamoto za kiuchumi (TAFEYOCO),  limesema halikubaliani na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kutaka wananchi kuwapa muda mawaziri wake katika utendaji, kwakuwa ni kiongozi pekee aliyechukua muda mrefu kuteua baraza.
Akizungumza jana jijini, Mwenyekiti wa TAFEYOCO,  Elvice Makumbo, alisema kauli ya Rais Magufuli kuomba muda si sawa, kwakuwa kati ya marais wote ni kiongozi pekee aliyechukua muda mrefu kuchagua mawaziri, hivyo ni wazi kuwa alishawapima na akawaamini.
“Rais Magufuli ndiye kiongozi pekee wa nchi aliyechukua muda mrefu kutangaza baraza lake la mawazili kuliko waliomtangulia, tena hata hivyo kuna baadhi ya wizara aliziacha wazi kwasababu alikosa watu sahihi,” alisema Makumbo.
Alisema kwa maandalizi hayo, haiingii akilini kuwa aina hiyo ya mawaziri aliowachagua  wapewe muda wa kujifunza kwakuwa wengine walikuwa mawaziri kwenye Serikali zilizopita.
Alisema kama kuna baadhi ya mawaziri anaona hawaendani na kasi yake kiutendaji ni bora awatumbue majipu na kuwatoa kwani siyo dhambi.
Alisema si sahihi Rais Magufuli au Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuwa watu pekee wa kugundua madudu kwenye taasisi za Serikali wakati wapo mawaziri husika wa maeneo hayo.                                     
Aidha, taasisi hiyo pia imemuomba Rais Magufuli kuzipa nguvu taasisi na mashirika ya umma ili yaweze kufanya kazi kwa ufanisi na bila kupata vitisho kutoka kwa kiongozi yeyote.
 “Rais Magufuli anatakiwa kuzipa nguvu taasisi za umma na mashirika ya umma ili yaweze kufanya kazi kwa ufanisi, anapaswa kuzijengea  nguvu ili zifanye kazi bila hofu wala woga kutoka kwa kiongozi yeyote,” alisema Makumbo.
Alisema taasisi kama Mahakama, Magereza, Mamlaka ya Bandari (TPA) na nyingine zinapaswa kuwekewa mfumo ambao zitawafanya kuwa na nguvu kubwa za mamlaka.
 Alisema endapo atatengeneza mfumo thabiti katika taasisi hizo, itasaidia watu kufanya maamuzi wenyewe bila woga wala mashinikizo kutoka kwa rais wala waziri husika.

No comments:

Post a Comment

MWENGE WA UHURU WAINGIA GAIRO NA KUZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA MILIONI MIASABA NA ZAIDI

 Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe akipokea Mwenge kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Morogoro Regina Chonjo mara ulipofika katika eneo la Ma...