LIPUMBA AMVAA MAGUFULI SAKATA LA SUKARI

 Rais Magufuli alitoa amri ya kuzuia kuagiza sukari toka nchi za nje tarehe 18 Februari wakati alipokuwa anawashukuru waandishi wa habari, wasanii na makundi mbalimbali yaliyoshiriki kwenye kampeni za Mgombea Urais wa CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015. Katika hafla hiyo alieleza viwanda vya sukari vina bidhaa hiyo na wanashindwa kuuza kwa sababu ya sukari iliyoagizwa kutoka nje. Aliwashutumu wafanyabiashara kuwa wanaagiza sukari ambayo inakaribia kwisha muda wake wa kutumiwa na binadamu na wanaileta nchini na kuiweka kwenye viroba vipya. Alimuagiza Waziri Mkuu asimamie zoezi hilo na yeye ndiye atowe vibali vya kuagiza sukari.
Baada ya tamko hilo la Rais, serikali ilitangaza bei elekezi ya shilingi 1800 kwa kilo nchi nzima. Hata hivyo serikali haikufafanua bei ya kiwandania ni shilingi ngapi? Na bei ya jumla katika kila eneo ni shilingi ngapi?
Waziri Mkuu akihitimisha hotuba yake ya Bajeti, alieleza kulingana na takwimu za serikali kuna tani 37,000 zilizomo nchini. Aliagiza Maofisa biashara katika halmashauri za wilaya wafanye ufuatiliaji katika maduka kuona sukari haifichwi na haiuzwi kwa bei ya juu. Bidhaa hii inapaswa kuuzwa kwa bei elekezi ili wananchi wapate sukari wakati wowote watakapoihitaji.
Sukari imeadimika na inauzwa kwa bei ya juu. Vyombo vya habari vimetoa taarifa kuwa kuna maeneo sukari inauzwa zaidi ya shilingi 4000 kwa kilo.
Vyombo vya Habari vimemnukuu Rais Magufuli kuwa “ametangaza kupambana na wafanyabiashara wasiozidi 10 waliohodhi biashara ya sukari, akisema ndiyo wameshiriki kuua viwanda na kujitajirisha.”
Taarifa ya Ikulu ya tarehe 6 Mei 2016 inaeleza “Dkt. Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwafuatilia wafanyabiashara wanaofanya njama za kuficha sukari na kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo, na ameapa kuwa serikali yake itawachukulia hatua kali watakaobainika kufanya hivyo.
Pamoja na kutoa maagizo hayo Rais Magufuli amewaondoa shaka watanzania juu ya upungufu wa sukari, kuwa serikali imeagiza sukari kutoka nje ya nchi ambayo itasambazwa kwa wananchi kwa bei nafuu ili kufidia upungufu uliopo.
"Wale wote waliokuwa wameficha sukari waiachie, wasipoiachia sukari, huwezi kuificha kama sindano, nimeshaagiza vyombo vya dola, vikague magodown yote, atakayekutwa na sukari ameificha, yule ni mhujumu uchumi kama wahujumu wengine, asije akanilaumu, asijee-akanilaumu, na ninasema kwa dhati, wewe mfanyabiashara uliyepata nafasi ya Tanzania kuleta bidha za sukari, halafu unanunua unakwenda kuficha ili kusudi wazee hawa wahangaike, ili mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapoingia watu wakose sukari, dawa yao ninayo" Amesema Rais Magufuli.
Katika Hotuba ya Bajeti Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ameeleza kuwa “mahitaji ya sukari nchini ni wastani wa tani 420,000 kwa matumizi ya kawaida na tani 170,000 kwa matumizi ya viwandani. Hadi kufikia Machi 29, 2016 uzalishaji umefikia tani 290,112 ikilinganishwa na matarajio ya tani 288,802 katika mwaka 2015/2016.” Viwanda vya Tanzania havizalishi sukari ya matumizi katika viwanda vya vinywaji na vyakula. Kwa hiyo sukari iliyotarajiwa kuagizwa toka nje ni tani 131,198 za sukari ya matumizi ya kawaida na tani 170,000 za sukari ya matumizi ya viwandani. Jumla tani 301,198.
Wakati Rais anazungumza na wapiga debe wake wa kampeni alieleza kuwa viwanda vya sukari vinashindwa kuuza sukari kwa sababu ya sukari iliyoagizwa kutoka nje. Hivi sasa viwanda vinaeleza havina sukari. Vitaanza uzalishaji mwezi wa Julai. Rais amesisitiza sukari imefichwa kwenye magodown.
Hata hivyo kitabu cha hotuba ya bajeti ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kinafafanua hali ya sukari ilivyokuwa hadi kufikia tarehe 29 Machi 2016. Wazalishaji walikuwa na tani 17,996. Wasambazaji wakubwa na wa kati tani 14,652. Jumla tani 32,648.
Ikiwa matumizi ya kawaida ya sukari kwa nchi nzima ni tani 420,000 kwa mwaka maana yake kila mwezi tunatumia tani 35,000. Ili pasiwepo na ukosefu wa sukari, wafanya biashara wa sukari wanatarajiwa wawe na alau hifadhi ya sukari ya kutosha mwezi mmoja wa mahitaji huku wakisubiri sukari nyingine kutoka viwandani au nje ya nchi.
Msimu wa uzalishaji sukari viwandani umemalizika. Mtibwa Estate walifunga Kiwanda tarehe 16/01/2016,  Kilombero tarehe 26/02/2016, TPC tarehe 15/03/2016, Kagera Sugar tarehe 11/04/2016.
Ikiwa mwezi Aprili, nchi imetumia tani 35,000, akiba ya sukari iliyokuwepo mwishoni mwa mwezi Machi itakuwa imemalizika. Sukari itakayokuwepo ni ile iliyoagizwa kutoka nje na kuingia nchini.
Kwa kutambua hali hii ya upungufu wa sukari nchini, mwishoni mwa mwezi Machi 2016, Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilimuomba Rais Magufuli kuruhusu kutoa vibali vya kuagiza sukari ili kukabiliana na upungufu wa bidhaa hiyo.
Lakini Rais ameishaeleza viwanda vyetu vuna sukari nyingi. Sukari isiagizwe toka nje.  Ni wazi Maafisa wa Bandari, Bodi ya Sukari na Mamlaka ya Kodi watasita kuruhusu upakuaji wa sukari iliyoagizwa hata kabla ya tamko la Rais.
Wakuu wa mikoa, Wakuu wa Wilaya, Polisi Takukuru wote wanashiriki kwenda kubaini sukari iliyofichwa. Wanaenda na vyombo vya habari. Shehena kubwa iliyokamatwa ilikuwa tani 5000. Hata hivyo “licha ya kukamatwa sukari inayodaiwa kufichwa, imebainika kuwa baadhi ya waliohifadhi hawakuwa wameificha, bali walikuwa wanakamilisha taratibu za kodi na vibali.”
Pamoja na msako mkali sukari iliyokamatwa nchi nzima haifiki tani 10,000. Lakini kwa kuwa Rais ameishasema sukari imefichwa, viongozi nao wanarudia kauli hiyo kuwa sukari imefichwa yasije yakawakuta yaliyomsibu Mama Anna Kilango Malecela.
Soko la Dunia
Bei ya sukari katika soko la dunia mwezi Agosti 2015 ilikuwa dola za Marekani 250 kwa tani moja. Kama dola moja ni shilingi 2000, tani moja ya sukari iliuzwa shilingi laki tano, sawa na shilingi 500 kwa kilo moja. Ukiongeza gharama za usafiri kilo moja ya sukari itafika Dar es Salaam kwa gharama isiyozidi shilingi 600 kwa kilo. Ukiweka ushuru wa forodha na VAT pamoja na faida ya wauzaji, kilo moja ingeweza kuuzwa chini ya shilingi 1000.
Bei imepanda kidogo. Mwezi Aprili tani moja ilikuwa inauzwa kwa wastani wa dola za Marekani 340. Tukichukua thamani ya dola ni shilingi 2200 na gharama za usafiri ni asilimia 20. Gharama ya tani moja ya sukari ni mpaka Dar es Salaam ni shilingi 763,000 kwa tani. Gharama ya kuagiza sukari pamoja na kulipa ushuru wa fordha na VAT haitazidi shilingi 1100. Sukari ya kutoka nje inaweza kuuzwa kwa shilingi 1250/- – 1500/-
Shirika la Chakula Duniani – FAO na Shirika la Uchumi na Uhirikiano wa Maendeleo - OECD linakadiria bei ya sukari katika soko la dunia itakuwa kati ya dola 350 na 390 kwa tani moja katika miaka ya 2016 – 2024.  Hivi sasa viwanda vyetu vina gharama kubwa za uzalishaji. Haviwezi kuhimili ushindani wa bei ya sukari inayozalishwa Brazil. Isitoshe soko la sukari la Ulaya na Japan linalindwa na nchi hizo kuwannfaisha wakulima.  Bei ya sukari nchini Hata Marekani inalinda soko lake la sukari haidhuru kwa kiasi kidogo ukilinganisha na Japan na Ulaya.
Taratibu za kodi au kuweka quota ya sukari itakayoagizwa toka nje zinaweza kutumiwa kulinda viwanda vya ndani. Serikali iwaeleze wananchi ukweli kuwa gharama ya kulinda viwanda vya ndani ni bei ya juu ya sukari ukilinganisha na bei ya soko la dunia. Kwa sababu ya tofauti kubwa ya bei kuagiza sukari toka nje na kuiuza nchini kuna faida kubwa.
Kugawa vibali vya kuagiza sukari bure kunaweka mianya ya rushwa. Serikali inaweza ikauza kwa mnada leseni za kuagiza kiasi cha sukari ya kuziba pengo la uzalishaji wa ndani. Kampuni zinazozalisha sukari zinaweza kushiriki katika mnada huo. Makampuni yaliyoshinda mnada na kapata leseni ndiyo peke yake yatakayoruhusiwa kuagiza sukari.
Maamuzi ya Rais
Taarifa ya Wizara ya Kilimo ya Hali halisi ya sukari inaonesha wazi hapakuwa na sababu za msako wa sukari iliyofichwa. Nina wasiwasi Rais hakushauriana na watendaji wake Bodi ya Sukari na Wizara ya Kilimo kabla ya kuamua kuzuia uagizaji wa sukari toka nje wakati akizungumza na wapiga debe wake wa kampeni. Hafla ile haikustahiki kutolea maamuzi kuhusu masuala ya sukari. Ni vyema Rais awape fursa taasisi na Wizara husika kutekeleza majukumu yao badala ya yeye kufanya maamuzi katika majukwaa ya siasa.
Sheria haimpi mamlaka Rais au serikali kupanga bei ya sukari. Bei elekezi haina nguvu za kisheria lakini pia inawachanganya wananchi na wafanya biashara. Kama bei elekezi ni bei ya reja reja nchi nzima, bei elekezi ya viwandani na ya jumla ni ipi?
Vitisho na viapo vya Rais dhidi ya Wafanya biashara havijengi taswira ya serikali kuithamini na kuishawishi sekta binafsi kuwekeza nchini Tanzania. Kauli za Rais zilisisitiza kuwa sukari iko nyingi nchini na imefichwa na wafanya biashara wachache. Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwepo kwa uhaba wa sukari.
Vitisho na ubabe wa Rais vinaweza kuwaogopesha Mawaziri na Watendaji serikalini wasimueleze bayana hali halisi. Kauli za kufichwa kwa sukari zinarudiwa na Wakuu wa Mikoa na hata vyombo vya habari pamoja na kwamba hakuna ushahidi wa kufichwa kwa sukari. Sukari kuwekwa kwenye hakumaanishi kuwa umefichwa.
Rais Magufuli aombe ushauri kuhusu changamoto na taratibu za kujenga uchumi wa soko shirikishi. Uzoefu wa Rais Mkapa wa kujenga utawala wa serikali unaweza ukamsaidia.
Mimi binafsi nilivutiwa na hotuba ya Rais alipozindua Bunge. Nia yake ya matumizi mazuri ya fedha umma, ukusanyaji wa mapato na mapambano dhidi ya rushwa ni mambo yamewavutia Watanzania wengi. Hata hivyo taratibu za kiutendaji na maamuzi ya sera kwenye majukwaa ya siasa vinanipa wasiwasi mkubwa. Ninakumbuka andiko la mwana habari maarufu baada ya uteuzi wa Mhe. John Pombe Magufuli kuwa Mgombea Urais wa CCM aliyeuliza Nani atakayemfunga gavana Rais Magufuli?


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu suala la kuadimika kwa sukari nchini. Kulia ni Mjumbe wa Baraza Kuu CUF Taifa, Bonifasia Mapunda na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdull Kambaya

Post a Comment

Previous Post Next Post