NECTA RICHARD: NATAKA KUWA MHANDISI NISAIDIE NCHI YANGU




 Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
 
WASICHANA wengi nchini wamekuwa wakiyaona masomo ya sayansi kuwa ni magumu na mzigo mkubwa kwao hali inayotoa nafasi kwa wavulana kuchangamkia masomo hayo ambayo yanatajwa kuwa na fursa nyingi za kiuchumi.
Tumesikia matamko mbalimbali ya viongozi wa ngazi za juu wa serikali wakiwahimiza wasichana kuachana na mtizamo huo hasi kwa kuanza kuyapenda na kujifunza masomo ya sayansi ili nao waje kuwa wataalamu wa fani tofauti tofauti hapo baadae.
Necta Richard ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Jangwani ni miongoni mwa wasichana walioamua kuitikia wito huo wa kusoma masomo ya sayansi.
Anasema amejipanga kuhakikisha kuwa anafikia ndoto yake ya kuwa Injinia mkubwa wa baadae nchini pindi Mungu atakapomuwezesha kuhitimu masomo yake.
MTANZANIA lilipata fursa ya kuzungumza na Necta punde baada ya kumaliza kuwasilisha hotuba mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani Julai 11, mwaka huu kwa niaba ya wanafunzi wenzake 150.
Akizungumza, Necta anasema tangu akiwa mdogo amekuwa akitamani kuja kuwa injinia, na kwamba alipoanza kusoma aliweka juhudi katika kujifunza masomo ya sayansi ili kufikia ndoto yake hiyo.
Anasema kwa kuwa aliyapenda masomo hayo kila siku amekuwa akijifunza kwa bidii na kuwasikiliza kwa makini walimu wake ili aweze kupata uelewa mpana zaidi.
“Nataka kuwa injinia mkubwa ili kuisaidia nchi yangu, nimepanga kusoma fani ya ‘Mechatronics’. Hii ni fani inayojumuisha mambo mawili kwa pamoja yaani ‘Mechanical’ na ‘Enginearing’ ambapo nitaweza kupata ujuzi wa vitu vingi kwa wakati mmoja kupitia fani hiyo, nitaweza kujua namna ya kutengeneza magari, kuwa injinia wa masuala ya umeme, kutengeneza vyuma na vitu mbalimbali vya aina hizo,” anasema.
Necta anasema wasichana wanapaswa kuachana na uwoga wa kusoma masomo ya sayansi kwa sababu kuna fursa nyingi za kujikomboa kichumi katika maisha yao ya baadae.
“Sijui kwanini wanaogopa na kuyakimbia masomo ya sayansi, lakini hakuna jambo gumu kikubwa ni kuwekeza katika kujifunza ili kujijengea msingi mzuri wa baadae kwa sababu masomo haya usipoweka msingi hapa awali huko mbele lazima utayaona magumu kwako.
“Nimeambiwa wasichana wengi wanaikimbia fani hii ya ‘Mechatronics’, ndio maana wanaofanikiwa kumaliza ni wanaume peke yao, mimi nataka nivunje rekodi hiyo ya kuwa msichana wa kwanza kusoma fani hiyo,” anasema kwa kujiamini.
Anasema anataka kuvunja rekodi hiyo na kuwa msichana wa kwanza kusoma fani hiyo kwani licha ya wavulana kuisoma hata hivyo bado kuna wataalamu wachache nchini. 
“Kwa msingi huo utaona namna ambavyo fani hii ina fursa nyingi za ajira. Nawashauri wasichana wenzangu wasiyakimbie masomo ya sayansi bali wayapende na kutia juhudi ya kujifunza ili waje kujikomboa kiuchumi hapo baadae,” Anasema.
Pamoja na hayo, Necta anasema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawasaidia watoto wao hasa wa kike katika kukabiliana na changamoto mbalimabali wanazokumbana nazo kila siku.
“Mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto nyingi kuliko mtoto wa kiume na hili lipo wazi, kwa mfano kuna suala la unyanyasaji wa kijinsia, ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni ambazo kiukweli imekuwa ikiwafanya wengi washindwe kutimiza ndoto zao.
“Hivyo wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wana walinda watoto wa kike dhidi ya unyanyasaji wa kila aina ili wafikie malengo yao kama ilivyo kwa watoto wa kiume, serikali nayo inapaswa iweke mazingira rafiki kwa watoto wa kike na kuweka sheria za kuwalinda,” anasema.
Anasema serikali inapaswa kukomesha na kuziondoa kabisa mila potofu dhidi ya mtoto wa kike ambazo zimekuwa zikikandamiza haki zao za msingi pamoja na sheria zinazokandamiza haki zao.
“Kwa mfano ile sheria ya ndoa ni vyema wakiifanyia marekebisho kwamba mtoto aolewe angalau akifikisha miaka 18 na si 14 kama ambavyo inasema hivi sasa,” anasema.
Necta anasema anaishukuru serikali na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kuwezesha ziara ambayo yeye na wenzake 150 waliifanya kwa kuzunguka katika maeneo mbalimbali kujionea shughuli za kiuchumi.
“Tuliweza kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), kikundi cha kina mama wajasiriamali Kimara ambako kwa kweli tulijifunza vitu vingi vya kitaaluma na kiuchumi ambavyo vilitufungua ufahamu wetu.
"Nawashauri wasichana wenzangu waje wajiunge na katika 'organization yetu ya apps' ambapo watajifunza jinsi ya kutengeneza application mbalimbali ikiwamo website hasa wale walio na umri wa miaka 13 hadi 18 ofisi zetu zipo Kisutu Sekondari au wanipigie kwa namba 0787 106 744,” anasema.

Post a Comment

Previous Post Next Post