JOKATE AJENGA UWANJA JANGWANI

Na Mwandishi wetu
Mrembo mwenye vipaji lukuki, Jokate Mwegelo kupitia kampeni yake yake ya kuchangia jamii ijulikanayo kwa jina la “Be Kidotified” amejenga uwanja utakaotumika kwa ajili ya michezo ya mpira wa kikapu na Pete (netiboli) kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana wa Jangwani.
Uwanja huo ulizinduliwa jijini jana katika hafla fupi iliyofanyika kwenye shule hiyo na kuhudhuriwa na wanafunzi, walimu na viongozi mbalimbali wa serikali. Ujenzi wa uwanja huo umemgharimu Jokate kiasi cha Sh 50 milioni.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Jokate alisema kuwa ameamua kuonyesha mfano kupitia ‘Kidoti Brand’ kuchangia maendeleo ya michezo nchini hasa kwa katika shule ambazo ni kiini cha maendeleo ya sekta hiyo hapa nchini. Mbali ya michezo, pia Kidoti Brand inajihusisha zaidi na maendeleo ya elimu hapa nchini.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano ya Tanzania imeadhimia kuondoa changamoto nyingi katika elimu na yeye kuamua kuanzia katika masuala ya michezo ambayo uchangia ufaulu darasani na kuibua vipaji ambavyo vitamwezesha mshiriki kupata ajira.
Alisema kuwa moja ya changamoto kubwa zinazorudisha nyuma maendeleo ya michezo nchini ni ukosefu wa viwanja bora ambavyo ukwamisha wachezaji chipukizi kuonyesha vipaji vyao ipasavyo.
Kwa mujibu waJokate, alipokuwa anasoma, alikutana na changamoto hizo, lakini alipiga moyo konde na kujihusisha na shughuli mbalimbali za nje ya darasa ikiwa pamoja na michezo na kujifunza mengi.
“Mimi ni mjasiriamali mchanga sana hapa nchini, nimehamasisha kwa kile kidogo nilichonacho na kwa msaada wa wadhamini niliyotafuta kuhitimisha ujenzi wa uwanja huu ambao utatumika si kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Jangwani pekee, bali hata kwa mechi za shule nyingine, ”
“Nawapongeza wadhamini walioniunga mkono katika mpango huu kama Mo Dewji Foundation, na wadau ambao walikuwa nyuma yangu katika kuhakikisha kampeni ya ‘Be Kidotified’ inaanza kwa mafanikio makubwa na kuendelea kwa shule nyingine za hapa jijini,” alisema Jokate.
Alisema kuwa chapa ya Kidoti ni miongoni mwa chama zinazoongoza hapa nchini katika mitindo, urembo na burudani kabla ya kuamua kupanua wigo kwa upande wa michezo tofauti na mpira wa miguu.
Alifafanua kuwa   alianza kwa kuanzisha kampuni ya Kidoti (Kidoti Company) na kuchangia katika soko la ajira nchini na baadaye kuanzisha   “kidoti brand’ akiwa na lengo la kuhamasisha vijana kujihusisha katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili kuweza kukabiliana na maisha ya kila siku.

Post a Comment

Previous Post Next Post