Tamko Rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu HALI YA NCHI Dar Es salaa, Jumanne, 06 Septemba 2016


  1. Utangulizi
               Jana Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa Kuhusu Hali ya Nchi; Kuidhinisha Makatibu wa Mikoa mbali mbali ya kichama nchini, kupokea taarifa ya Fedha ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG na masuala mbalimbali ya kinidhamu ndani ya Chama.  Taarifa hii sasa inatolewa rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali ya kiuchumi, umoja wa kitaifa na hitimisho. 

  1. Hali ya Kisiasa 
Kamati Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania. 

Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi. Kisiasa, tunatambua kwamba Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa wanamsukuma Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya Chama cha Mapinduzi mbele ya umma. 


Kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Kamati Kuu ya chama chetu imeazimia yafuatayo:
  1. Tunalaani na kupinga kwa nguvu zetu zote hatua za Serikali ya Chama cha Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa sheria.
  2. Tunapinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya kujaribu kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya utawala wa sheria.
  3. Tutasimama imara, na tutaungana na vyama vingine vya siasa pamoja na taasisi zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu.

  1. Hali ya Kiuchumi 
              Katika miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji huu wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipato cha chini. Awamu ya tano ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili ndilo tulitegemea Serikali mpya ishughulike nalo. 

             Kamati Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa mfano:
  1. Taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba - Desemba 2015) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari - Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%! 

  1. Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii inamaanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani.

  1. Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ulikuwa ni 13.8% lakini ukuaji wa sekta hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka. 

  1. Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama ntilie wanaowauzia chakula.

Kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu:
a)    Tunaitaka serikali izingatie ‘’sayansi ya uchumi’’ katika kuendesha uchumi wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi badala ya washauri wa uchumi kumshauri yeye, itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi. 
b)    Inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria. Juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi. Tusiruhusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake. 

  1. Umoja wa Kitaifa
               Nchi yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na baadaye vyama vya siasa tunaishi bila kukamiana wala kuhasimiana. Juhudi za dhati za kupambana na ubaguzi ndiyo umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa Kitaifa na amani tunayojivunia. 

Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM, kupitia Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungano, umeanza kwa juhudi na kasi kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja wetu. Sasa tunaye Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na wapi.

Vijana waliosoma kwa bidii katika mazingira ya shule zilizotelekezwa na serikali ya CCM anawaita VILAZA. Katikati ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar Rais wetu amefunga safari, sio kwenda kujaribu kutibu majeraha yaliyosababishwa na kuchezewa kwa sanduku la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa vyombo vyetu vya dola vyenye jukumu la kulinda na kudumisha amani. Sasa Rais wetu, kupitia kauli zake, ameanza kuubomoa muungano wetu uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu. Kila asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha Rais wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano na undugu wetu kama taifa.

Yote haya yakitokea chama chake cha CCM ama kimekaa kimya au kinachekelea. Inasikitikitisha kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere kinamruhusu kiongozi wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea chuki katika jamii ya watanzania. 

Kwa kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea nchini, Kamati Kuu:
1)    Tunalaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao za kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na amani ya nchi .
2)    Tunatoa wito kwa watanzania wote waipendao nchi yao kusimama kidete katika kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa na utawala wa CCM.
3)    Tunatoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi waliopita, hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika nchi yetu wavae ujasiri wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake za kuchochea chuki katika jamii yetu ya watanzania zitasambaratisha Taifa letu. 

  1. Hitimisho
               Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na kujenga uwajibikaji nchini. 

Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi. Tunasisitiza kuwa mtu yeyote, wa kawaida au kiongozi, anayesema kwamba anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sharia, mtu huyo ni mwongo na kwa kweli ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!

Tunasisitiza kuwa msingi wa uchumi wetu ni kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi. Kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa kuvutia uwekezaji. Juhudi za hivi karibuni za serikali ya CCM za kujaribu kuua utawala wa sheria ni juhudi ovu za kuua uchumi wa nchi yetu. TUZIKATAE juhudi za kuua utawala wa sheria kwa kuwa zitaangamiza taifa letu, kiuchumi, kisiasa na kijamii.


Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb

Kiongozi wa Chama

Post a Comment

Previous Post Next Post