Wednesday, January 20, 2016

Askofu Pengo ahamishiwa Taasisi ya Moyo

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amehamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), lililoko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kardinali Pengo amehamishiwa katika taasisi hiyo akitokea katika wodi ya wagonjwa wa dharura ambako alilazwa mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo juzi.
Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa MNH, Neema Mwangomo, alisema hata hivyo afya ya Askofu Pengo imeimarika tofauti na walivyompokea.
“Askofu amehamishiwa JKCI na amelazwa katika wodi ya wagonjwa wa kawaida kwa mujibu wa madaktari wake, alitakiwa kurudi hospitalini siku tisa baada ya kupewa ruhusa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake,” alisema.
Juzi saa nne asubuhi, Askofu Pengo alirudishwa hospitalini hapo na kulazwa katika wodi ya wagonjwa wa dharura ikiwa ni siku tisa tangu aliporuhusiwa kurudi nyumbani Januari 8, mwaka huu.
Januari mosi, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli pamoja na mkewe Janeth walikwenda kumjulia hali askofu huyo.
Wakati huo huo, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), imerejesha wodi za Mwaisela na Sewahaji kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo awali walikuwa wakizitumia kulaza wagonjwa wao.
Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa MOI, Patrick Mvungi, alisema tayari wamewahamishia wagonjwa wao katika jengo lao jipya na siku yoyote watayakabidhi rasmi kwa uongozi wa Muhimbili.
“Jana (juzi) tulimalizia kuwahamisha wagonjwa 33 katika wodi ya wanawake kuwapeleka kwenye jengo letu jipya, tumeamua kuwahamishia huko ili tuwaachie wenzetu wa MNH nafasi ya kuwahudumia wagonjwa kwa sababu hivi sasa tuna wodi za kutosha hivi sasa na vitanda ambavyo tulipatiwa na Rais Dk. John Magufuli,” alisema.

Meya mpya Dar kupatikana Jumamosi
NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
UCHAGUZI wa kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam atakayemrithi Dk. Didas Masaburi unatarajiwa kufanyika Januari 23, mwaka huu.
Msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe, aliiambia MTANZANIA kwa simu jana kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika.
“Tupo katika maandalizi ya kuhakikisha meya wa jiji anapatikana katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii, na vyama vyote tunatarajia kuvitumia barua ya mwaliko muda si mrefu,” alisema Makwembe.
Alisema uchaguzi huo utafanyika katika Ukumbi wa Karimjee, huku akisisitiza kuwa vyama vyote vyenye uwakilishi wa madiwani katika jiji hilo vitashiriki.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kati ya vyama vinavyounda na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 Hata hivyo, Ukawa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ambapo wanaizidi CCM kwa jumla ya madiwani 13.
Iwapo Ukawa watafanikiwa kutwaa jiji hilo, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa wapinzani kuongozakuliongoza tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alitoa wito kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia uchaguzi huo kwa amani na haki.
“Uchaguzi huu wa meya wa jiji usifanyike kama ule wa kumtafuta meya wa Ilala na Kinondoni uliokuwa na mizengwe mingi iliyochangiwa na CCM kutokubali kushindwa na wapinzani,” alisema Makene.
Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita (Chadema) ndiye atapeperusha bendera ya Ukawa huku mgombea wa nafasi ya naibu meya akitarajiwa kutoka chama cha CUF.

CCM YATEGEMEA MUUJIZA
Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abillahi Mihewa, alisema kuwa licha ya uchache wao lakini inaweza kutokea miujiza ya Mwenyezi Mungu wakaibuka washindi  kwa kumpata meya. Watawakilishwa na Diwani wa Kinondoni,  Yusuph Omary Yenga.
“Unajua Mwenyezi Mungu ni mkubwa, pamoja na wingi wao wanaweza kuamka wakaongozwa na maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ‘rais anaweza kutoka chama chochote lakini rais bora atatoka CCM’, na inaweza kuwa hivyo kwa meya,” alisema Yenga.

Tuesday, January 19, 2016

Semzaba alianza kuigiza akiwa na miezi miwili Dada zake Edwin semzaba


MWANDISHI wa kitabu cha tamthilia ya ‘Ngoswe Kitovu cha Uzembe’, Edwin Semzaba aliyefariki dunia juzi jijini Dar es Salaam alianza kuigiza miezi miwili baada ya kuzaliwa.
Semzaba ambaye kitabu chake cha Ngoswe kinatumika katika shule za sekondari nchini, akiwa na umri wa miezi miwili alitumiwa kuigiza kama mtoto Yesu katika sherehe za Krismasi kanisani.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam nyumbani kwa marehemu huko Mbezi Temboni, mdogo wa marehemu, Fred Semzaba, alisema kaka yake tangu akiwa katika umri huo mdogo waumini walikuwa wakimchukua na kufanya naye maigizo kama mtoto Yesu.
“Tuna imani kipaji cha ndugu yetu kilianza kujidhihirisha kanisani tangu akiwa na miezi miwili hadi mitatu, waumini walikuwa wakija nyumbani na kumwomba mama ambapo walimchukua na kuigiza naye maigizo katika mkesha wa Krismasi kama mtoto Yesu,” alisema Fred.
Alisema kifo cha ndugu yao kimeacha pengo kubwa kwakuwa alikuwa ni tegemeo ndani ya familia ambapo ameacha watoto watatu aliokuwa akiwalea.
“Tutamkumbuka marehemu kwa ucheshi wake na sisi kwetu tunaweza kusema alikuwa mlezi kwakuwa tulizaliwa wanane na wenzetu watatu wakubwa walikwishatangulia mbele ya haki na yeye ndie alikuwa tegemeo la familia,” alisema.
Semzaba alizaliwa mwaka 1951 Magila Muheza mkoani Tanga na alisoma Shule ya Msingi Temeke na baadaye Kasulu, Mwibuye na Living Stone za mkoani Kigoma.
Alijiunga na kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Mkwawa, Iringa na baadaye alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baadhi ya vitabu na maagizo aliyowahi kutunga ni pamoja na Ngoswe, Tende Hogo na Tausi Alfajiri.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam ambapo ibada fupi ya mazishi itafanyika nyumbani kwake Temboni na baadaye katika Kanisa la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alikuwa akifanya kazi hadi umauti unamkuta.

Wahariri Mawio waachiwa kwa dhamanaJESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewaachia kwa dhamana ya Sh milioni 40 wahariri wa gazeti la Mawio, Jabir Idrisa, Simon Mkina.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Wakili wa wahariri hao, John Kibatala, alisema wateja wake walifika kituoni hapo juzi baada ya jeshi hilo kuwataka wajisalimishe.
Kibatala alisema baada ya kujisalimisha walifanyiwa mahojiano  kuhusu  habari iliyochapishwa na gazeti hilo, lakini waliachiwa kwa dhamana ya Sh milioni 20 kila mmoja pamoja na wadhamini wawili, huku wakitakiwa kuripoti  kituoni hapo kila siku saa 2:00 asubuhi na polisi wakiendelea na upelelezi.
“Taratibu za kipolisi zimefanyika tumepewa dhamana, hivyo tumeona ni busara tuwape muda polisi wafanye uchunguzi na mambo mengine yatakayoendelea tutawafahamisha,” alisema Kibatala.
Mhariri Mkuu wa Mawio, Mkina, alisema baada ya kujisalimisha juzi kwa agizo la jeshi hilo walilala kituoni hapo hadi jana saa 6:40 mchana ndipo waliachiwa kwa dhamana.
“Tumehojiwa na askari  na tumetolewa kwa dhamana, lakini tunatakiwa kuripoti kituoni hapa kila siku saa 2:00 asubuhi huku wakiendelea na upelelezi,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Idrisa alisema baada ya kujisalimisha askari walianza kumhoji kuhusu habari  iliyoandikwa katika gazeti la Mawio yenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
“Tumetoa maelezo yetu na  tumeachiwa kwa dhamana,  askari wanaendelea na upelelezi,” alisema Idrisa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alitangaza gazeti la Mawio kufutwa kwenye orodha ya magazeti iliyopo kwa msajili kwa kutumia sheria ya magazeti ya mwaka 1976.


Monday, January 18, 2016

Wahariri Mawio Wajisalimisha Polisi


Kutoka kushoto ni Mmiliki wa gazeti la Mawio (Saed Kubenea), Mwenyekiti wa Jukwaa la WAhariri Tanzania (Absalom Kibanda), Jabir Idrisa (Mhariri wa Gazeti la Mawio) na wa Mwisho ni wakili wa anaeisimamia kesi hiyo Fredrick Kiwelo.
Kutoka kushoto ni Mmiliki wa gazeti la Mawio (Saed Kubenea), Mwenyekiti wa Jukwaa la WAhariri Tanzania (Absalom Kibanda), Jabir Idrisa (Mhariri wa Gazeti la Mawio) na wa Mwisho ni wakili wa anaeisimamia kesi hiyo Fredrick Kiwelo.


Sunday, January 17, 2016

Kubenea kutinga na Escrow BungeniMBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amesema anatarajia kufufua hoja ya kujadiliwa upya kwa ripoti ya fedha zilizokwapuliwa za Tegeta Escrow zaidi ya Sh bilioni 200.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, alisema sababu za kutaka mjadala huo kurejeshwa ni kutaka kujua iwapo fedha hizo ni za umma au ni mali ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Sababu nyingine aliyoitaja Kubenea ni kutaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa sakata hilo, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Mapendekezo ya Taarifa ya PAC
Iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, iliwasilisha bungeni mapendezo zaidi ya 10 likiwemo azimio namba moja la kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kumkamata Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP) Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ukwepaji kodi.
Kamati inaelekeza Serikali kutumia sheria za nchi, ikiwamo sheria ya Proceeds of Crime Act, kuhakikisha kuwa Singh Sethi anarejesha fedha zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG iliyothibitishwa na TAKUKURU, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu binafsi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe, alisema kamati yake ilijiridhisha kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu (BoT).
Historia ya Escrow
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya IPTL.
Fedha hizo zilizua mjadala mkubwa bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka msimamo wa Serikali kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, akisema kuwa fedha hizo hazikuwa za umma na hivyo kuzidisha mjadala.

WADAU WA MITINDO NA UREMBO WAALIKWA KUSHIRIKI MAONESHO UCHINA

Makamu wa Rais wa Maonyesho ya Wachina Maharufu kama China International Beauty Expo African Hall,Rex Chan akizungumza na Waanddishi w...