Saturday, February 6, 2016

DK SLAA KUFUNGA NDOA NCHINI CANADA NA JOSEPHINE MSHUMBUSHI


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, anatarajia kubariki ndoa na mkewe Josephine Mshumbusi siku chache zijazo.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa watu walio karibu na familia ya Dk. Slaa, zimedai kuwa kasisi huyo wa zamani na mkewe Josephine, watabariki ndoa yao nchini Canada kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.
Ingawa taarifa hizo hazikuthibitisha siku ambayo harusi hiyo itafanyika, zimeeleza kuwa maandalizi yako katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuhudhuriwa na watu wachache.
“Dk. Slaa na mkewe Josephine Mshumbusi wapo katika maandalizi ya kubariki ndoa yao huko nchini Canada, taarifa nilizonazo harusi yao wataifunga kabla ya Sikukuu ya Pasaka,” alisema mmoja wa watu walio karibu na familia hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi.
Alipoulizwa Josephine kupitia simu yake ya kiganjani, alithibitisha kuwa taarifa hizo ni za kweli na kwamba wapo katika hatua za mwisho za maandalizi ya tukio hilo.
MTANZANIA Jumapili lilipomuuliza siku ambayo ndoa hiyo inatajiwa kufungwa alicheka kisha akasema atatoa taarifa rasmi siku moja kabla ya harusi.
“Ha ha ha ha… wachawi wengi, okay (sawa) nitakuambia ikiwa imebaki siku moja kabla ya shughuli,” alisema Josephine.
Wawili hao wanaishi pamoja kwa takribani miaka sita sasa na waliwahi kuanza maandalizi ya kufunga ndoa wakiwa hapa nchini, lakini walikwama baada ya mke wa ndoa wa Dk. Slaa, Rose Kamili kupeleka pingamizi mahakamani.
Baada ya pingamizi hilo, wawili hao waliendelea kuishi pamoja hadi hivi karibuni wakiwa uhamishoni Canada zilizopatikana taarifa za kufunga ndoa yao hiyo.
Wakati hayo yakijiri, taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili hivi karibuni zilieleza kuwa Dk. Slaa na Josephine waliondoka nchini mwaka jana na kukimbilia nchini Canada ambao waliomba hifadhi ya kisiasa.
Taarifa hiyo ambayo ilichapwa na gazeti hili toleo la Jumamosi ya wiki iliyopita, ilieleza kuwa Dk. Slaa aliomba hifadhi ya kisiasa nchini Canada kwa sababu ya kuhofia usalama wa maisha yake hapa nchini, baada ya kuanza kutishwa na watu ambao hawajapata kujulikana kutokana na uamuzi wake wa kujiondoa Chadema wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu.
Katikati ya hayo, zipo taarifa za kupigwa mnada kwa nyumba yake iliyopo Mbweni jijini Dar es Salaam baada ya mkewe Josephine anayedaiwa kuitumia kuchukua mkopo benki moja iliyopo maeneo ya Mwenge, kushindwa kuurejesha.
Josephine mwenyewe amekuwa akikanusha madai hayo na mumewe Dk. Slaa ambaye alifanya mahojiano na gazeti hili mapema wiki hii alimuunga mkono kwa kueleza pamoja na mambo mengine kuwa ni umbea.
Katika mahojino hayo, Dk. Slaa alieleza kuwa yeye na mkewe Josephine tangu walipoanza kuishi pamoja hawajapata kuchukua mkopo benki na tangu alipoacha kuwa mbunge hajawahi kuchukua hata senti moja benki ukiachilia mbali propaganda ya kuchukua mkopo wa sh milioni 300.

KIKWETE ATOA ONYO KWA MAMLUKI NDANI YA CCM

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt. Jakaya Kikwete mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Namfua mkoani Singida kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM.

 

NA WAANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, ametangaza kung’atuka kwenye wadhfa wake huo huku akiwanyoshea kidole mamluki walio ndani ya chama hicho.
Akihutubia maelfu ya wanachama na wafuasi wa CCM wakati wa maadhimisho ya miaka 39 tangu kuanzishwa kwa chama hicho yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida jana, Kikwete alisema siku za kundi la mamluki walio ndani ya CCM zinahesabika.
Kikwete ambaye ni rais mstaafu wa awamu ya nne, aliueleza umati uliohudhuria sherehe hizo kuwa katika maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 40, atakuwa amekwishang’atuka kumpisha Rais Dk. John Magufuli kukiongoza chama hicho.
“Kipindi cha uchaguzi chama kilikuwa katika majaribu, wale waliotabiri anguko pia walikuwepo. Tunajua wapo watu waliobaki kama mamluki, lakini haikusadia, wanajisumbua bure na siku zao zinahesabika, hatuwezi kuwa na mamluki wanyonya damu,” alisema Kikwete.
Alisema chama hakiwezi kuendelea kukaa na wale aliowataja kwa jina la ‘kikulacho’ ambao wanaweza kuepukwa.
Akizungumzia mwenendo wa uchaguzi wa mwaka jana, alisema baadhi ya wana CCM walikasirika na kuhama chama kwa sababu ya kutokubaliana na taratibu zilizofuatwa.
“Niliahidi chama kitawaletea wagombea wazuri pande zote na nilisema hakuna kitakachoharibika, nilijua CCM ina utaratibu mzuri, maadili na kanuni za vikao.
“Mchakato wa uchaguzi umeisha bado CCM ipo imara, nampongeza Mangula (Katibu Mkuu Bara, Phillip Mangula) kwa kufanya kazi nzuri ya kufuatilia wagombea 38 na kuwachuja hadi kufika watano,” alisema Kikwete.
Aliwataja pia viongozi wastaafu wanaounda Baraza la Ushauri la CCM kuwa walitumia nafasi zao kutoa ushauri mzuri wenye hekima na busara.


Alisema baada ya kupatikana kwa wagombea hao, kikao cha Kamati Kuu ya CCM (NEC) nacho kilitawaliwa na vurugu, huku baadhi ya wana CCM wakidhani mambo yangeweza kuharibika.
Kikwete alisema suluhisho lilipatikana baada ya kura za wanachama kumpa ushindi Rais Magufuli na makamu wake, Samia Suluhu Hassan.
Mbali na kuzungumzia mwenendo wa Uchaguzi Mkuu, Kikwete pia alitangaza kuachia uenyekiti wa CCM kabla ya chama hicho kutimiza miaka 40 na kumpisha Rais Magufuli kukiongoza.
“Ninashiriki kwa mara ya mwisho katika sherehe hizi kama mwenyekiti, sherehe za mwaka ujao rais wetu Magufuli ndiye atakayekuwa mwenyekiti,” alisema Kikwete.
Alisema amefurahishwa na wazo la kufanyika kwa maadhimisho hayo mkoani Singida kwa kuwa ndiyo eneo alipoanzia kazi akiwa katibu wa TANU.
“Nimeanzia kazi Singida na ndipo ninapomalizia. Aprili 1975 ndiyo niliingia Singida kama katibu wa TANU, barabara zilikuwa mshikemshike.
“Mkoa huu ndipo ilipopandwa mbegu yangu ya utumishi wa chama na umma, na nina hakika ilikuwa nzuri ndiyo maana nikapata nafasi ya urais na ingekuwa mbaya ningeishia hapo hapo,” alisema.

AMPONGEZA MAGUFULI
Kikwete pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya na kudai kuwa kiongozi huyo ameanza vizuri.
“Nakupongeza mheshimiwa rais, umeanza vizuri, Watanzania wanafurahi kuona ukiishi kwenye kauli na ahadi zako, mimi na viongozi wengine tunakuunga mkono, unachofanya ndicho CCM inataka kifanyike,” alisema Kikwete.
Alisema katika kipindi kifupi cha siku 90 Rais Magufuli amethibitisha kuwa yeye ni mtekelezaji mahiri wa ahadi.
Kikwete alisema Rais Magufuli amekuwa akichukua hatua kali za haraka kwa wote wanaoendeleza rushwa katika ofisi za Serikali na taasisi za umma.
Alisema amekuwa akiendelea na mchakato wa kuendesha mahakama ya mafisadi kama ilivyo katika ilani ya CCM.

AMPIGIA DEBE SAMIA
Kikwete pia alimzungumzia Makamu wa Rais, Samia kuwa CCM imepiga hatua kubwa kwa kuwa na kiongozi wa nafasi hiyo mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.
“Hatua ya kuwa na makamu wa rais mwanamke inaonyesha nchi yetu imepiga hatua, mnajua kazi ya makamu wa rais ni msaidizi wa rais hata akisafiri, sasa kupata rais mwanamke inawezekana, kwanini baada ya Magufuli Samia asiwe rais, eti Samia, simama kwani huwezi,” alisema Kikwete huku akimshika mkono Samia.

ALIVYOMBEMBELEZA KINANA
Kikwete alirejea jinsi alivyomshawishi Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kushika wadhifa huo kwa kutumia wazee kumbembeleza.
“Kinana nilimuombaga awe katibu mkuu akakataa, nikatumia wazee akanikatalia, nikasema sawa kama hutaki baadaye nikamfuata nikamwambia sikiliza Abdul, hapa tulipofikia kama kweli unaipenda CCM basi usikatae kuwa katibu mkuu,” alisema Kikwete.
Alisema Kinana amefanya kazi nyingi ya kutembea jimbo hadi jimbo kwa ajili ya kukiimarisha chama.

AWAPONGEZA VIJANA WA MITANDAO
Kikwete alisema  vijana wa mitandao wapatao 46 walifanya kazi saa 24 na walikuwa wakipokezana kwa awamu katika kipindi cha kampeni.
“Tunao vijana wetu wa mitandao walifanya kazi masaa 24 wakipokezana ‘shift’ (zamu) tatu kuhakikisha hatunyanyaswi  katika mitandao ya kijamii, maana wao walituweza katika magazeti, sisi tuliwabana katika mitandao,” alisema.
Alimtaka Rais Magufuli alitizame kundi la vijana hao na aangalie  namna ya kuwashukuru kwakuwa walifanya kazi nzuri mitandaoni.

UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR
Kuhusu marudio ya uchaguzi wa Zanzibar, Mwenyekiti Kikwete alisema alisikitishwa na hatua ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana kwa sababu CCM ilikuwa na uhakika wa ushindi.
“Uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi umetusikitisha kwa kuwa umeenda kinyume na matarajio yetu, sisi tulikuwa tunajiandaa kushangilia ushindi, tumekubali uamuzi huo kwa sababu walisema kulikuwa na matatizo,” alisema Kikwete.
Alisema hawakutamani kurudia uchaguzi kwa sababu zoezi hilo lina usumbufu na aliwataka wana CCM wa Zanzibar wajiandae kurudia uchaguzi.

RAIS MAGUFULI
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaasa watendaji wa Serikali kutambua kuwa kipaumbele katika utendaji wao ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM.
“Mtumishi yeyote wa Serikali kama hatatekeleza kwa bidii na maarifa makubwa ilani ya uchaguzi ya CCM, huyo akae pembeni tuweze kuwapa watu ambao watatekeleza ilani ya CCM kwa tija.
“Mimi mwenyewe kiongozi wao navaa mavazi ya kijani na natekeleza ilani ya CCM kwa nguvu zote, hivyo watumishi wa ngazi zote hawana budi kufuata nyayo zangu,” alisema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti Kikwete jana alipokea wanachama wapya wa CCM zaidi ya 35,000 wakiwamo waliokuwa wabunge wa Bunge la kumi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Christowaja Mtinda na Rachel Mashishanga.


 
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wanachama wa CCM pamoja na wakazi wa Singida kwenye uwanja wa Namfua waliohudhuria kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wanachama wa CCM pamoja na wakazi wa Singida kwenye uwanja wa Namfua waliohudhuria kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt. Jakaya Kikwete kulia pamoja na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoani Singida.

 Rais  wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Abruhamani Kinana
 Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt. Jakaya Kikwete akihutubia mamia ya wanachama wa CCM mkoani Singida
 
Rais  wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa katika sherehe hizo mkoani Singida.
 
Rais  wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akipongezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Abrahamani Kinana pamoja na Makamu mwenyekiti wa CCM Taifa  Philip Mangula mara baada ya kuhutubia wakazi wa Singida

Rais  wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt. Jakaya Kikwete wakiondoka mara baada ya kuisha kwa sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa chama cha Mapinduzi CCM Mkoani Singida-Picha na IKULU


UJENZI WA NJIA NNE MOROGORO ROAD ENEO LA MBEZI WASHIKA KASI

Wakandarasi wakiendelea na ujenzi wa Roound about ya Msigani kama inavyoonekana katika picha Barabara ya Morogoro Road katika Mfumo wa nj...