Mbunge
wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe jana walichafua hali
ya hewa bungeni na kusababisha mzozo mkubwa katika mjadala uliokuwa
ukiendelea.
Wawili
hao walihamisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais Tamisemi
na kurudisha suala la Richmond lililotokea mwaka 2008, huku Nasari
akimtuhumu Dk Mwakyembe kuwa hakutenda haki katika ripoti yake na
kumuondoa bila kumpa nafasi ya kujitetea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward
Lowassa.
“Huyu
Mwakyembe ndiye aliyeongoza ripoti ya Richmond na hakumpa nafasi
mheshimiwa Lowasa ajitetee, leo tena kapewa dhamana ya kuongoza Wizara
ya Habari, Nape (Nnauye) ameondolewa lakini hakuna nafasi ya kumhoji
Mkuu wa Mkoa... hakuna haki hapo,” alisema.
Kauli za Nasari zilimfanya Dk Mwakyembe kuomba mwongozo na aliposimama alisema: “Nilikuwa
naongoza kamati na utaratibu mzuri wa kisheria ni kuwa, kama utaona
kuna ushahidi wa kutosha hakuna sababu ya kumuita mtu, unaleta taarifa
bungeni halafu Bunge linakuja kuamua.”
Dk
Mwakyembe alisema katika taarifa yao, waliona hakuna sababu ya kumuita
Lowassa kuhojiwa kwani ushahidi ulikuwa wazi na ndiyo maana hakutakiwa
kuitwa mbele ya kamati badala yake walikuja kumshtaki bungeni.
“Huyu
mtu wanayekuwa na mahaba naye kwa sasa, nasema wamlete hata leo waone
kama hatutamnyoa kwa chupa, kanuni za kibunge zinaruhusu anaweza
kuirudisha tena taarifa ya Richmond na ikaanza upya,” alisema Dk Mwakyembe.