NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
HEDHI ni mzunguko wa kila mwezi ambao huleta kutokwa na
damu ukeni, hali hiyo hutokea pale ambapo yai la mwanamke linakuwa halijakutana
na mbegu ya kiume ili kulirubutisha kutengeneza mtoto.
Kila mwanamke ana mzunguko wake wa hedhi, ingawa kwa
kawaida hedhi ya kwanza hutokea katika umri wa miaka 12 na 13 hata hivyo wapo
ambao huanza kupata hedhi katika umri mdogo wa kati ya miaka tisa hata 10.
Mzunguko wa hedhi hudhibitiwa na homoni zinazozalishwa na
mwili wenyewe, hedhi hutokea pale ambapo tishu za ukuta wa mji wa mimba
hubomoka na kutoka kama damu ukeni.
Hedhi ni kipindi maalumu katika maisha ya mwanamke
aliyefikia umri wa kuzaa.
Kwa kawaida mzunguko wa hedhi hutokea kila mwezi na kila
mwanamke anao mzunguko wake ni hapo ambapo mwili hujiandaa kwa hali ya kupata
ujauzito.
Jinsi
inavyotokea
Mwanamke ana ovary mbili (vifuko vya mayai) katika mwili wake,
moja upande wa kushoto na nyingine kulia ambazo hutengeneza mayai ya uzazi.
Kila mwezi, ovary moja huachilia yai kitendo hicho
kitaalamu huitwa ‘ovulation’ yai husafirishwa hadi katika mji wa mimba kupitia
mirija ya uzazi.
Wakati huo mabadiliko ya homoni huuandaa mji wa mimba
(uterusi) kutengeneza ukuta mpya uitwao ‘endometrium’ kwa ajili ya kujiweka
tayari kwa mapokezi ya mimba inayoweza kutungwa.
Yai linalofika katika mji wa mimba (uterasi) iwapo
halitarutubishwa na mbegu ya mwanamume, ukuta huo humeguka na kutoka nje ya mji
wa mimba kupitia ukeni ukiwa pamoja na damu.
Kitendo hicho ndicho huitwa hedhi (menstruation) au
mzunguko wa hedhi (menstruation cycle). Mara nyingi mwanamke hukoma hedhi
anapotimiza umri wa kuanzia miaka 45
hadi 50.
Ingawa ni kipindi muhimu katika maisha ya mwanamke lakini
huwa kimejaa changamoto ambazo huzipitia, changamoto hizo hutofautina kati ya
mwanamke mmoja na mwingine.
Wapo ambao hupata hedhi kwa siku tatu na wengine huenda
hadi saba na miongoni mwao wapo pia ambao hupata hedhi nyepesi na wengine
nzito.
Wapo pia ambao hupata hedhi pasipo kukabiliana na matatizo
yoyote lakini wengine hupata hedhi kwa uchungu na masumbufu mengi, kama kuumwa
tumbo, mgongo, kichwa, kiuno na mengineyo.
Usafi
muhimu
Pamoja na yote hayo, suala la usafi ni jambo la muhimu
mwanamke anapaswa kuzingatia kipindi chote maishani mwake, hasa kipindi cha
mzunguko wa hedhi.
Ili kujiitiri katika kipindi hicho muhimu, mwanamke
hulazimika kutumia kifaa maalumu ambacho hukinga damu ya hedhi ili asichafuke.
Inawezekana ikawa ni kitambaa kilichotengenezwa kwa ajili
ya kazi hiyo iwe kwa njia ya asili au kisasa, hujulikana kama pedi au taulo za
kike.
Enzi za mabibi zetu njia iliyokuwa ikitumika zaidi ni ile
ya asili, walitengeneza vipande vya kanga au kitenge kujisitiri.
Lakini kukua kwa teknolojia kukapelekea kutengenezwa taulo
za kisasa za kutumia na kutupa ambazo huuzwa kwa bei tofauti tofauti madukani.
Daktari
Akizungumza hivi karibuni na MTANZANIA, Daktari Bingwa wa
magonjwa ya kinamama na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Belinda
Balandya anasema kipindi cha hedhi ni cha muhimu kwa afya ya mwanamke.
“Mwanamke anapokuwa katika siku zake hulazimika kutumia
taulo hizo ambazo kazi yake kuu ni kupokea ile damu inayotoka, kama hatavaa
maana yake ni kwamba itapitiliza kuchafua nguo zake.
“Taulo za kutumia na kutupa jinsi zilivyotengenezwa zina
‘layer’ maalumu kwa ndani ambayo hufyonza damu ya hedhi, hulazimu kubadili mara
nyingi (kiasi cha kila baada ya saa nne) hasa inapokuwa inatoka kwa wingi,”
anasema.
Madhara
ya kuvaa taulo muda mrefu
Daktari huyo ambaye pia ni muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya
na Sayansi Shirikishi (Muhas) anasema kuna athari kubwa iwapo mwanamke
hatazingatia usafi akiwa katika kipindi hicho katika via vyake vya uzazi.
“Kwa kuwa inanyonya damu maana yake ni kwamba hufika wakati
unakuwa kama vile umevaa kitu kibichi, hivyo ngozi huanza kupata michubuko. Kwa
wale ambao ngozi yao ni ngumu kidogo huwa si rahisi kuona michubuko hiyo lakini
wanapojisafisha kwa maji na sabuni huhisi maumivu,” anasema.
Bakteria
huzaliana
Anaongeza “Damu ni sehemu ambayo bacteria huota kwa urahisi
kwa sababu wanakuwa wanapata chakula wanachohitaji kwa urahisi, mtu anaweza
kuendelea kuvaa kwa sababu hajui jambo hili lakini ni hatari.
“Kwa sababu bakteria wanakua kwa urahisi husababisha pia
muhusika kupata maambukizi katika sehemu zake za siri,” anasema.
Wanaotumia
vitambaa
Anasema iwapo mtu anatumia vitambaa alivyovitengeneza
kujisitiri navyo vinapaswa kukauka ili bakteria wasipate nafasi ya kuzaliana.
“Kumbuka kwamba nimesema bakteria huzaliana kwa urahisi
kwenye damu, kitambaa kisipokauka na kubaki na unyevunyevu maana yake ni kwamba
bakteria waliozaliwa watabaki hawajafa kwa hiyo wataendelea kukua hivyo
muhusika atakuwa amejiweka kwenye ‘risk’ ya kupata ‘infections,” anasema.
Anaongeza “Kuna pedi fulani...zimetengenezwa mfano wa
unene wa kidole na imewekwa kamba
kidogo. Wapo wanawake wanazitumia, zinauzwa huko madukani, huingizwa ndani ya
uke ili kufyonza damu na huitoa kwa kuvuta kamba hiyo inayokuwa imebaki nje ya
uke.
“Sasa hizi ni taulo mbaya zaidi, wengine wanapoweka wakati
wa hedhi chache, hujisahau kuzitoa na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kupata
madhara,” anasema.
Mfumo wa uzazi wa mwanamke
Athari yenyewe
Athari yenyewe
Anasema bakteria hao huenda kutengeneza kovu katika mirija
ya uzazi na mwisho huziba kabisa na kwamba huweza kupenya na kuingia hadi
katika mfumo wa damu na kuleta athari zaidi.
“Kama mwanamke huyu hatawahi hospitalini anakuwa yupo
kwenye hatari hata ya kushindwa kushika ujauzito kwa sababu bakteria hao
huendelea kushambulia mfumo wake,” anasema.
Kauli
za wanawake
Julieth Masinga Mkazi wa Mbezi Luis anasema awali hakuwa
anajua iwapo taulo ya kike inaweza kusabisha madhara makubwa namna hiyo.
“Najua suala la usafi ni la msingi lakini sikuwahi kujua
nini madhara ambayo yanaweza kujitokeza iwapo mwanamke atakaa muda mrefu akiwa
amevaa taulo moja kwa muda mrefu,” anasema.
Anaongeza “Binafsi huwa sipendelei kukaa na taulo moja muda
mrefu lakini kuna wakati unashindwa jinsi ya kufanya kwa mfano ukiwa safarini
unatumia muda mrefu barabarani, ni changamoto kwa kweli.
“Kuna siku nilikuwa kwenye mizunguko yangu ya kibiashara
nilitumia muda mrefu mno, nilikuwa kwenye siku zangu, kusema ukweli nilijihisi
vibaya kukaa muda mrefu bila kujisafisha, nililazimika kutafuta bafu la kulipia
nikaoga na kubadili pedi nyingine.
“Lakini itabidi tuzingatie ushauri wa daktari ili tuweze
kujilinda afya zetu tusipate maambukizi,” anasema.
Mkazi wa Sinza Kijiweni, Pelina Yesaya anasema bado elimu
kuhusu hedhi inahitajika hasa kwa kundi la wasichana wadogo.
“Kwa mfano huko vijijini bado kuna maeneo ambayo wasichana
wanahitaji kuelimishwa zaidi kuhusu hedhi, jinsi inavyotokea na namna ya
kujisitiri na hata kuepukana na mimba za utotoni,” anasema.
Anaongeza “Kule wengi hawajafikiwa angalau huku mjini watu
wanao uwezo wa kutumia taulo ya kutumia na kutupa, kule wengi wanatumia taulo
za asili, kwa hiyo kuna ulazima mkubwa wa kuwapelekea elimu kama hii ili wawe
salama,” anasema.