KAIMU JAJI MKUU WA TANZANIA AFANYA ZIARA YAKE YA KWANZA BABATI-MKOANI MANYARA


Na Mary Gwera, Mahakama
KAIMU Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma amesifu kasi ya uondoshaji wa Mashauri katika ngazi za chini za Mahakama nchini akitaja kuwa ni Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya.
Alisema hayo mapema Mei 9 katika ukumbi ya mikutano ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara alipokuwa akiongea na Watumishi wa Mahakama Mkoani  humo,akiwa katika ziara yake ya kwanza kufanya tangu kuteuliwa kwake Januari, mwaka huu.
Mhe. Jaji Mkuu amewapongeza Mahakimu wote nchini ikiwa ni pamoja na Mahakama- Manyara kuhusiana na kasi ya kuondosha mashauri katika Mahakama za ngazi za chini licha ya idadi kuonekana kuwa kubwa.
Mhe. Jaji Prof. Juma alisema kuwa wananchi wengi bado wana Imani na Mahakama yao, hivyo idadi kubwa ya mashauri imeendelea kufunguliwa katika Mahakama zetu hususani Mahakama za Chini ambazo ni Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Hakimu Mkazi.
“Kwa takwimu tulizo nazo Mahakama kwa mwaka jana, asilimia 71 ya mashauri yalifunguliwa katika Mahakama za Mwanzo, huku Mahakama ya Wilaya ikiwa na asilimia 14 ya kesi zilizofunguliwa kwa mwaka jana, Mahakama za Hakimu Mkazi asilimia 7, Mahakama Kuu asilimia 5 na Mahakama ya Rufani ikiwa na wastani ya asilimia 0.5,” alieleza Kaimu Jaji Mkuu.
Aliendelea kusema kuwa takwimu hizo zinaonesha dhahiri kuwa wananchi bado wana Imani kubwa na Mahakama zetu na hivyo kuwataka Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kuongeza bidii katika kuwatumikia wananchi.
Mbali na pongezi hizo, Mhe. Kaimu Jaji Mkuu amewataka Watumishi wa Mahakama-Manyara kufanya kazi kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Mahakama ambao ndio dira ambayo itawawezesha kufikia azma ya kuwa Mahakama bora yenye kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Wengi wenu mnafahamu kwa sasa, Mahakama ipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano, wenye lengo la kuboresha maeneo mbalimbali Mahakamani ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma ya utoaji haki nchini pamoja na kurejesha imani ya wananchi kwa chombo chao,” aliwaambia watumishi hao akiwataka kila mmoja kushiriki kikamilifu katika utekelezaji huo.
Aidha, Mhe. Jaji Prof. Juma aliwataka watumishi wa Mahakama pia kujikita katika Matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi huku akitilia mkazo kwa Watumishi pia kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Awali akisoma hotuba yake mbele ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora alisema kuwa Mahakama katika mkoa huo zimekuwa zikifanya kazi ya uondoshaji mashauri kwa jitihada ili kuhakikisha kuwa inaondokana na mlundikano wa kesi.
“Mhe. Kaimu Jaji Mkuu, kwa upande wetu, Mahakama kanda ya Manyara tumejiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa kesi yoyote inayoletwa katika Mahakama ya Mwanzo/Wilaya isizidi miezi mitatu mpaka kukamilishwa kwake, na hili tunalisimamia kuhakikisha tunaondokana na mlundikano wa mashauri katika Mahakama zetu,” alisema Mhe. Kamuzora.
Ziara ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu imelenga katika kuangalia utendaji kazi wa Mahakama hizo, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo na hatimaye kushughulikia changamoto hizo kwa ustawi wa Mahakama.
Mhe. Kaimu Jaji ametembelea Mahakama kadhaa mkoani humo ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Wilaya Babati, Mahakama ya Mwanzo/Wilaya Hanang, pia kukagua Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na anaendelea na ziara katika Mkoa wa Arusha.
 Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Juma akiongea na Watumishi wa Mahakama mkoani Manyara (hawapo pichani), miongoni mwa vitu alivyzungumzia ni pamoja na kuzingatia maadili katika ufanyaji kazi, utoaji wa taifa sahihi kwa manufaa ya umma, na matumizi ya TEHAMA.
 Mhe. Prof.Ibrahimu Juma akiendelea kuzungumza na Watumishi wa Mahakama-Manyara, aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Sekela Moshi, kulia ni Mhe. Rumisha, Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora (aliyeketi pembeni wa kwanza) pamoja na baadhi ya Watumishi wengine wa Mahakama mkoani humo wakimsikiliza Mhe. Kaimu Jaji Mkuu pindi alipokuwa akizungumza nao.
Miongoni mwa Watumishi wa Mahakama waliohudhuria kikao hicho pamoja na Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.
 Mmoja wa Watumishi akiuliza swali.
Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, akifafanua jambo.
 Kaimu Jaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Juma (wa tatu kushoto), Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Sekela Moshi (wa tatu kulia), Katibu wa Mhe. Kaimu Jaji Mkuu, Mhe. Eliazar Luvanda (wa pili kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama wa mkoani Manyara.
 Mhe. Kaimu Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama walioshiriki katika kikao cha Watumishi na Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.
Mhe. Kaimu Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama walioshiriki katika kikao cha Watumishi na Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.
Mhe. Kaimu Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu aliowahi kuwafundisha chuoni, wa kwanza kulia ni Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Mhe. Kaimu Jaji Mkuu akikagua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi/Wilaya Manyara lililopo katika ujenzi, kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama hiyo kutasaidia kuondokana na changamoto ya uchakavu wa jengo wanayokabiliana nayo katika Mahakama ya sasa. (Picha zote na Mary Gwera wa Mahakama)

Post a Comment

Previous Post Next Post