MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU AWAPA SHAVU WAKANDARASI WA NDANI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwa miradi yote yenye thamani isiyozidi bilioni 10 wapewe Wakandarasi wa ndani hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani kwani wakandarasi hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuongeza uwekezaji ndani ya nchi. Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati anafungua mkutano wa siku Mbili wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi mwa mwaka 2017.

Makamu wa Rais amesisitiza wakandarasi hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na sheria pamoja na kumaliza kazi wanazopewa ndani ya muda uliopangwa kwa kuzingatia ubora wa kazi na gharama zilizokubalika kwenye mikataba na sio vinginenevyo. Makamu wa Rais amewataka wakandarasi kote nchini kuacha mara moja tabia ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wanayopewa.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa ili wathubuti kujitosa na kumudu zabuni za ujenzi kwani kwa kufanya hivyo kutaleta faida mbalimbali ikiwemo fedha watakazopata watawekeza ndani ya nchi na kutoa ajira za kutosha kwa vijana wa Kitanzania.

“Hatuwezi kuwa na Tanzania ya Viwanda huku tukiwanufaisha Makandarasi wa nje pekee ni lazima Makandarasi wa ndani wanufaike pia.”

Kuhusu madeni ya wakandarasi, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Wakandarasi kuwa Serikali haijawasahau na bajeti ya Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano ambayo imepitishwa na bunge imezingatia kilio hicho cha Wakandarasi.

Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kulipa madeni inayodaiwa na wakandarasi ili kujenga mahusiano mazuri ya wakandarasi hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesisitiza kuwa Wizara hiyo inaendelea kusimamia sheria na maadili kwa wakandarasi ili kuhakikisha miradi ya ujenzi inayotekelezwa kote inakuwa na ubora unaotakiwa.

Waziri Profesa Mbarawa amekiri kuwa kuna baadhi ya wakandasiri ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo hivyo kujenga miradi jinsi ya kiwango hivyo ni muhimu kwa wakandarasi hao kufanya kazi kwa ubora ili waweze kuaminiwa na Serikali na kupewa kazi.

Amesema kuwa Wizara yake itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakandarasi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa viwango vinavyotakiwa.

Nae, Msajili wa Bodi ya Wakandarasi Nchini Rhoben Nkori amesema bodi hiyo imefuta usajili wa wakandarasi 3,000 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Usajili wa Wakandarasi ya mwaka 1997 na kwa sasa bodi hiyo inawakandarasi 9,000 kote nchini.
 
Msajili huyo pia amesema kuwa katika kuratibu mwenendo wa kazi za makandarasi bodi hiyo ilikagua miradi 3,813 ambapo kati ya miradi hiyo miradi 2714 sawa na asilimia 71.2 haikuwa na kasoro na miradi mingine ilikuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo miradi hiyo kutofanywa na wakandarasi waliosajiliwa na kutozingatia usalama wa wafanyakazi.

Kasoro nyingine ni wakandarasi kufanya kazi zaidi ya viwango vya madaraja yao,miradi kutosajiliwa na miradi kutokuwa na bango.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mashauriano Wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa Mwaka 2017 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kikwete mkoani Dodoma.
Wajumbe wa Mkutano wakimsikiliza kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mashauriano Wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa Mwaka 2017 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kikwete mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi Mhandisi Consolata Ngimbwa akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mashauriano Wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa Mwaka 2017 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kikwete mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa,Viongozi wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi na Wajumbe waliohudhuria mkutano wa Mashauriano Wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa Mwaka 2017 nje ya ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kikwete mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Wakandarasi Wanawake mara baada ya kufungua Mkutano wa siku mbili wa Mashauriano Wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa Mwaka 2017 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kikwete mkoani Dodoma.

Post a Comment

Previous Post Next Post