Na Humphrey Shao Globu ya Jamii
BODI ya
Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imesema kuwa udahili wa wanafunzi
wanaofanya mitihani ya bodi hiyo umepungua kutokana na woga wa wanafunzi hao na
kwamba somo la hesabu limekuwa tatizo kubwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa bodi hiyo,
Godfred Mbanyi alisema kuwa lengo la bodi hiyo ni kudahili wanafunzi
waliochukua kozi ya ununuzi na ugavi 2,000 lakini tangu mwaka 2016, udahili
umekuwa ukishuka.
Amesema kuwa
katika mtihani uliofanyika mwaka 2016, walifanya udahili kwa wanafunzi 1,519,
waliofanya mtihani ni 1,442, waliofaulu 660 na wanafunzi 745 wanarudia mitihani
huku wanafunzi 37 ambayo ni sawa na asilimia 2.6 walifeli.
Alifafanua
kuwa udahili wa mwaka huu ulifanyika kwa wanafunzi 1,964 na kwamba wanafunzi
1,578 ndio waliofanya mitihani na 653 wamefaulu mitihani hiyo.
‘’Kutokana
na masomo ya ugavi kuhusisha somo la hesabu, kumekuwa na matokeo hafifu kwa
wanafunzi wetu wanaofanya mitihani hii ya bodi na tatizo hili limetokea hata mwaka
jana. Sababu za watu kufeli masomo haya ni kwa sababu hawapendi hesabu,’’
alisema Mbanyi.
Aliongeza
kuwa ‘’Wanafunzi wengi wanaofanya mitihani wanakuwa na background mbaya katika
somo la hesabu hivyo tunaendelea kuweka msisitizo kwenye vituo vya maandalizi.
Lakini woga wa wwanafunzi unachangiwa na kuwa na mtaala mpya wa mitihani
ulioanza Novemba 2016 ambao haukuwepo na
unautaratibu mpya wa ufaulu hivyo wanafunzi waliogopa.’’
Pia alisema
kuwa somo la viashiria vya hatari katika ununuzi na ugavi ambalo linalenga kutambua na kuainisha
viashiria ili kuviepuka wakati wa mchakato wa ununuzi na kwamba masomo ya
kujifunzia (case studies) watahiniwa walifeli.
‘’Udahili
umepungua lakini tumeweka mikakati ya kutembelea vyuo vyote vikuu na vinavyotoa
masomo ya ugavi na ununuzi kwa ngazi ya shahada na stashahada kuwahamasisha
kufanya mitihani ya bodi ili watambuliwe na waongezeka,’’ alisisitiza Mbanyi.
Alieleza
kuwa bodi hiyo imewataka wanafunzi wanaotaka kufanya mitihani hiyo kupitia
katika vituo vya kutolea mafunzo vilivyosajiliw na bodi kwa kuwa sababu za
wanafunzi kufeli mitihani hiyo inachangiwa na kutojiandaa vizuri.
Kwa mujibu
wa Mbanyi, PSPTB imeweka mkakati wa kuwa na vitabu maalumu ya kufundishia vya
aina moja vitakavyotumika katika vyuo vyote nchini na mitihani ijayo
itakayoanza wawe wameanzisha vitabu hivyo ili kuondoa mkanganyiko katika
kufundishia.
Mbanyi
alisema watahakikisha kuwa wataalamu wanaozalishwa wanakuwa na mtazamo wa
kufikia uchumi wa viwanda kwa kusoma masomo ya sayansi na hesabu na kwamba utaalamu
wa ununuzi na ugavi utaleta matokeo chanya kufikia uchumi huo.
‘’Vyuo
vinavyoongoza kwa kuleta wanafunzi wengi ni Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo Kikuu
cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Chuo cha Biashara (CBE)
na vyuo vinavyochangia ni Chuo cha Jordan Morogoro na Chuo cha Usafirishaji
(NIT),’’ alifafanua.
Alisema kuwa
vyuo vilivyopo Zanzibar pia vimekuwa vilileta watahiniwa kwa ajili ya kufanya
mitihani hiyo ya bodi ili kuingizwa katika orodha ya wataalamu wa masuala ya
ununuzi na ugavi.
Kaimu Mkurugenzi wa bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wanatangaza matokeo ya wanafunzi waliofanya mitihani ya bodi hiyo mwezi wa Novemba mwaka jana.Waandishi wa Habari wakifatilia kwa makini Mkutano huo ambao ulikuwa wa kutangaza matokeo na mwenendo wa matokeo ya Mitihani kwa wanafunzi wanaokuja kujiandikisha.