WANANCHI wa Kijiji cha Magasa, Kata ya Mrijo wilayani
Chemba, wamekosa huduma za afya kwa muda mrefu, licha ya jengo la zahanati yao
kukamilika kwa zaidi ya miaka minne sasa.
Wakizungumza na Ripota wa Jijiletu mwishoni mwa wiki, wananchi hao
walisema wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita saba hadi vijiji vya Soya na
Mrijo kufuata huduma za afya, jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwao.
Jengo hilo ambalo limejengwa kwa nguvu za wananchi na
baadae Serikali kumalizia, linadaiwa kukaa kama pambo kijijini hapo bila huduma
zozote, licha ya ujenzi wake kukamilika tangu 2014.
“Jengo letu tangu limekamilika linazaidi ya miaka minne,
pia tumeletewa daktari hapa alikuja kuripoti, tuliambiwa baada ya mwezi mmoja
atakuja kuanza kazi, tumesubiria hadi leo hatujamwona,” alisema Ramadhan
Rajabu.
Mwananchi mwingine Hamisi Kijaji alisema kinachowaumiza
zaidi ni pale wajawazito wanavyopata shida, kwani wanatumia usafiri wa baiskeli
na mikokoteni na wakati mwingine wanapoteza maisha njiani kutokana na ubovu wa
barabara.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Mussa Ninga, alikiri
kukosekana kwa huduma hiyo na kueleza watumishi wawili wameripoti kijijini
hapo, lakini waliondoka katika mazingira ya kutatanisha.
Ninga alimtaja daktari mmoja kwamba aliripoti kijijini hapo
Novemba 28, mwaka jana akitokea Kituo cha Afya Makorongo, lakini aliondoka bila
taarifa ambapo hadi sasa haijulikani alipo.
“Awali tuliletewa mtumishi anaitwa Prisca alikuja
28/10/2016 na saini yake ipo ofisini kwenye kitabu alipokuja kuripoti, baadae
tuliambiwa ameondolewa kwa sababu ya vyeti feki,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Idd Baba, alisema zahanati
hiyo imegeuka mzigo kwake, kwani amefanya jitihada kufuatilia ngazi za juu
lakini hajapata majibu ya kuridhisha.
“Kila siku mara leo mara kesho, naletewa daktari mara
tunaambiwa ni feki, naanza tena kufuatilia nikaletewa mwingine mara nikasikia
naye amehamishwa,” alisema.
Diwani wa Kata ya Mrijo, Hamisi Msakati (CCM), alikiri wananchi
hao kupata shida licha ya jengo kukamilika muda mrefu na kueleza kuwa
alipofuatilia wilayani kuhusu watumishi aliambiwa zahanati hiyo haijasajiliwa.
“Mwaka jana walileta doctor mwingine alikuja akaripoti
nikapata na barua, lakini mazingira aliyoondokea ni ya kutatanisha.
Nilipofuatilia wilayani Mganga Mkuu wa Wilaya akaniambia hii zahanati
haijasajiliwa.
“Nilimwambia kuna watumishi wawili mmewaleta kule, wakati
mnafanya hayo hili la usajili mlikuwa hamlijui? Kwa kweli sikupata majibu ya
kuridhisha, hayatoshelezi hata kwa akili za kawaida,” alisema.
Mwandishi alilazimika kumtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dk. Semistatus Mashimba, ambaye alishangazwa na taarifa hizo na
kuahidi kuchukua hatua mara moja ili wananchi hao wapate huduma.
“Hili ndiyo nalisikia kutoka kwako, kwanza nikushukuru kwa
kunipa taarifa hili nalifuatilia kuanzia sasa, yaani hata diwani ameshindwa
kufika ofisini kwangu hata simu ameshindwa kunipigia tukalimaliza?
“Miaka minne watu hawapati huduma na jengo limekamilika
kama ni usajili taratibu zake zipo wazi kinachokwamisha ni nini? Uzembe huu
hauwezi kuvumiliwa,” alisema Dk. Mashimba.