HUSSEIN BASHE ANAPOTUHUMIWA UNAFIKI?


Bashe

Bashe Mohamed Bashe, ambaye ni Mbunge wa Nzega Mjini CCM, mara kadhaa amekuwa akiibua mijadala katika mitandao ya kijamii kwa kuandika akieleza misimamo na mitazamo yake kuhusu mambo mbalimbali yanayotokea hapa nchini.
Watu wengi na hasa wana CCM wenzake wamekuwa wakiitafasili misimamo na mitizamo yake kuwa yenye sura au vimelea vya upinzani dhidi ya chama chake.
MIKITO BLOG imeanza kufuatilia mijadala inayotokana na misimamo na mitizamo ya mwanasiasa huyo machachari wa CCM kwa lengo la kuibua mjadala mpana zaidi kuhusu aina ya siasa zinazofanywa na Bashe.
Hapa chini ni andiko la Mwanasheria Albert Msando linalojadili barua inayodaiwa kuandikwa na Bashe kwenda kwa Katibu wa Bunge.
Msando

Kabla ya chochote niseme kwamba kuwekeza kwenye matukio ya UHALIFU ambayo yamesababisha vifo vya watu ni UNAFIKI.
Vitendo vya kutekwa kwa baadhi ya watu, kuuawa kwa makusudi kwa  viongozi wa kisiasa na kizembe kwa mwanafunzi ni VITENDO VYA KIHALIFU NA JINAI. Uchunguzi wake ni wa KIUHALIFU na JINAI.
Kamati ya Bunge sio chombo chenye uwezo na utaalamu wa kufanya uchunguzi wa makosa ya kihalifu na jinai!
Nimebahatika kuisoma barua inayosemekana imetumwa kwa Katibu wa Bunge na Mh. Bashe M. Bashe (MB). Ameweka wazi nia yake kutaka Bunge la Jamhuri ya Muungano liunde Kamati Maalumu kwa sababu zifuatazo;
a) Kusinyaa kwa demokrasia na haki za Raia
b) Kupotea, kutekwa na kuuawa kwa Raia katika chaguzi mbalimbali na matukio ya uhalifu katika siasa
c) Kupigwa risasi na kuumizwa Raia ndani ya nchi na kikundi cha watu kinachoitwa 'wasiojulikana'
d) Mauaji ya viongozi wa kisiasa wanaotokana na vyama halali vya kisiasa
e) Ukandamizwaji wa uhuru wa Raia kutoa maoni, kukosoa na kushauri
f) Matumizi mabaya ya sheria na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya nchi
g) Haki za kikatiba na kisheria za vyama vya siasa kutoheshimiwa
h) Tuhuma dhidi ya vyombo vya usalama na matumizi ya silaha za moto kwa Raia
 Niseme wazi tu hii ni HAKI na WAJIBU wake kufanya alichofanya. Ameitumia HAKI yake na ametekeleza WAJIBU wake. NI HOJA BINAFSI kwa hiyo ina ubinafsi ndani yake. Siasa.
Ila najiuliza, je amewezaje kuitumia HAKI yake na kutimiza WAJIBU wake kwenye nchi yenye mazingira ya kusinyaa demokrasia, ukandamizaji na matumizi mabaya ya sheria?
Barua hiyo inayosema hayo yote wengi tumeisoma. Je imetufikiaje sisi? Amewezaje kuisambaza barua hiyo na kuthibitisha hilo kwenye ukuta wake wa Twitter kwenye nchi inayotumia sheria vibaya? Sheria ya Makosa ya Mtandao ipo na alishiriki kuipitisha!
Je mbona haijatumika 'vibaya' dhidi yake kiasi kwamba ameweza kujibizana na Mh. Lema ambaye amefikia hatua ya kumuita MNAFIKI hadharani?
Nimetumia muda kidogo kusoma alichojibiwa Bashe na baadhi ya watu. Wengi wamemshambulia na kumwambia waziwazi anatafuta 'kiki' na umaarufu. Nadhani anachotafuta anakijua mwenyewe. Na inawezekana amekipata.
Lakini hii sio mara ya kwanza Bashe anazungumzia hili suala. Alishaomba Bunge kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama liangalie hicho anachokirudia sasa. Spika alielekeza hilo kwa Mh. Adadi na Kamati yake. Bashe anaweza kueleza matokeo ya agizo la Spika yalikuwa nini?
Tukiliangalia hili suala kisiasa (kwa sababu Bashe ameamua kulifanyia siasa) utaona kile alichokiita Mh. Lema unafiki wa Bashe. Katika hali ya kawaida mtu mwenye akili timamu angetegemea Mbunge wa Upinzani tena Chadema aungane na Bashe kwenye hoja hiyo. Badala yake amemuita mnafiki. Bashe amepata fundisho lolote? Sidhani.
Ni nani atasimama na kuhesabiwa basi endapo hata wabunge wa upinzani hawasimami na Bashe katika hili? Sio kwamba Bashe alikuwa hajui kwamba hoja yake haitaenda popote wala haitaungwa mkono. Alikuwa anajua ila ameamua kufanya siasa ya matukio kufikia malengo yake binafsi ya kuidhoofisha serikali ya chama chake pamoja na vyombo vya usalama.
Naungana na Lema kuhusu tafsiri ya alichokifanya Bashe. Ni unafiki. Anachotaka Bashe ni kuonekana mkweli, asiyeogopa na mwenye ujasiri. Lakini anasahau ujasiri usio na busara ndani yake hauna maana yoyote. Kuunganisha matukio ya uhalifu na masuala mengine kwa lengo la kuonyesha usalama wa taifa letu uko hatarini ni unafiki tu.
Mwisho, wakati Bashe anatafakari majibu na muitikio alioupata baada ya kusambaza barua yake ni vyema akaufahamisha umma yafuatayo;

Bashe

1). Ni kwa kiasi gani demokrasia imesinyaa Jimbo la Nzega? Ni mikutano mingapi imezuiliwa au kukatazwa kufanyika kwenye Matawi, Vijiji/Mitaa na Kata za Nzega?
2). Ni wananchi wangapi katika Jimbo la Nzega wamenyimwa haki na uhuru wa kutoa maoni, mawazo na kukosoa?
3). Jimboni kwake Nzega ni sheria gani imetumika kukandamiza demokrasia ya wanaNzega?
4). Je yeye kama Mbunge wa Chama cha Mapinduzi amechukua hatua gani ndani ya chama kuhusu hayo yote ambayo amemuandikia Katibu wa Bunge?
5). Ni Raia wangapi wametekwa, kupigwa Risasi na kuumizwa Nzega?
6). Vyama vingapi (na vipi) ambavyo haki zao za kikatiba hazijaheshimiwa Nzega? Hatua gani vimechukua hapo Nzega?
Uwekezaji wa kisiasa kwenye matukio ya kiuhalifu ni uhalifu wa kisiasa. Tuisaidie nchi yetu kwa kushauri na kuchukua hatua ambazo hazitaleta mgawanyiko au mfarakano kati yetu.
Ni matumaini yangu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Ndg. Mwigulu Nchemba ataliangalia hili na kuchukua hatua. Kimsingi alichojaribu kuonyesha Bashe ni kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya kulinda Raia na mali zao pamoja na kuhakikisha usawa bila ukandamizaji wowote.

 Alberto .

Post a Comment

Previous Post Next Post