Jafo Aagiza Uanzishwa Wa ‘One Stop Center’ kwa ajili ya Wawekezaji

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya Nchini kuhakikisha wanaanzisha kituoa kimoja cha huduma ‘One Stop Center’ kwa ajili ya wawekezaji.

Mhe. Jafo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Warsha ya namna ya Uendeshaji wa  Mabaraza ya Biashara kwa Mikoa na Halmashauri zote Nchini iliyoandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mradi wa Local Investiment Climate (LIC) inayofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.
Katika Warsha hiyo inayowajumuisha viongozi wa Ngazi za Mkoa na Wilaya Mhe. Jafo amesema mazingira magumu ya upatikanaji wa taarifa za uwekezaji na urasimu uliopo katika Mikoa na Wilaya ndio unaowakwaza Wawekezaji katika harakati zao za kutaka kuwekeza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Imekuwa ni vigumu sana kwa Muwekezaji kupata taarifa sahihi na kwa wakati katika maeneo yetu na hii imekua ikiwakatisha moyo na kupelekea hata kusitisha mpango mzima na nia yao ya kuwekeza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, inatakiwa tubadilike na tuweke mazingira rahisi yatakayomuweza kila mdau anayetaka kuwekez kupata taarifa anazozihitaji kwa urahisi.

Hali hii inarudisha nyuma juhudi zetu za kuhamasisha uwekezaji sasa basi kila kiongozi wa Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanaanzisha kituo kimoja “One Stop Center” ambacho kitatoa huduma zote kwa Wawekezaji kama vile upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji, Leseni za biashara, Hati miliki, usajili wa kampuni, namna ya ulipaji wa kodi nk” alisema Jafo.

Aliongeza kuwa warsha hii imewakutanisha wadau kutoka Sekta ya umma na binafsi katika kila ngazi ya utawala ili kujadiliana namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji Nchini na hivyo basi ni wakati wa kukubaliana kwa pamoja namna mabaraza ya Biashara yatakavyosaidia katika kukuza Uchumi wa Viwanda ambao ndio muelekeo wetu kama Taifa kwa hivi sasa.

Sambamba na hilo Jafo aliwakumbusha viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa pamoja na majukumu mengine wanapaswa kutengeneza mazingira bora ya kufanyia biashara na uwekezaji, kuibua fursa za uwekezaji, kuzinadi fursa zilizoibuliwa kupitia Makongamano ya uwekezaji na kuandaa midahalo mahususi.

Pia Mhe. Jafo alisisitiza kuwa mara baada ya kikao hiki kila kiongozi akahakikishe kuwa Vikao vya mabaraza ya Biashara vinafanyika kwa mujibu wa Sheria na viongozi washiriki katika vikao hivyo na maazimio ya vikao hivyo yakashughulikiwe kwa wakati na kutoa mrejesho kwa upande wa sekta za umma na binafsi.

Aidha kila Halmashauri zikatenge bajeti kwa ajili ya uendeshaji wa Mabaraza ya biashara  na kwa upande wa Sekta binafsia ziandae utaratibu mzuri wa kuchangia gharama za uendeshaji wa vikao hivyo.

Alimalizia kuwa Mradi wa LIC kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Baraza la Taifa la Biashara kuandaa utaratibu wa kueneza uzoefu uliopatikana katika Mikoa miwli ya Dodoma na Kigoma ambapo mradi huu umetekelezwa ili mikoa mingine iweze kujifunza na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Mabaraza ya Biashara Tanzania yameanzishwa kwa mujibu wa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 691 la tarehe 28 Seot,2001.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akifungua warsha ya kujadili changamoto za Uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara Tanzania inayofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma
   Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge akizungumza na wadau wa baraza la biashara kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo.
   Kaimu Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa OR-TAMISEMI Beatrice Kimoleta(kwanza Kushoto) akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala bora na Huduma OR-TAMISEMI Angelista Kihaga (kwanza kulia) pamoja na wadau wa Baraza la Biashara katika warsha ya kujadili uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara.




1.      Mkurugenzi Msaidia wa Utawala toka OR-TAMISEMI Bw. Mrisho Mrisho akiongoza warsha ya Mabaraza ya Biashara Tanzania.

1Mshauri wa Majadiliano baina ya Sekta Umma na Binafsi wa LIC Bw. Donald Liya (Kwanza kushoto) akifuatiwa na Kiongozi Msaidizi wa Timu ya LIC Bw. Peter Laizer, Mshauri wa Mradi wa LIC toka Taasisi ya Sekta Binafsi Bi. Rehema Mbugi pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa TCCIA Bw. Gotfried Muganda wakifuatilia warsha ya kujadili changamoto ya Uendeshaji wa Mabraza ya Biashara.

Post a Comment

Previous Post Next Post